WAZIRI wa Nishati, Januari Makamba, amesema ifikapo Desemba mwaka huu vijiji vyote vya mkoa wa Tabora ambavyo havijafikiwa na umeme vitakuwa vimeunganishwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tabora … (endelea).
Mkamba ameyasema hayo leo Jumatano tarehe 18 Mei 2022 katika hafla ya uzinduzi wa Barabara ya Tabora-Mpanda kilomita 342.9.
“Katika wilaya ya Sikonge vijiji vyote ambavyo havina umeme vimeingizwa kwenye programu ya kupatiwa umeme kwahiyo mkoa wa Tabora na Wilaya ya Sikonge itakapofika Desemba mwaka huu vijiji vyote ambavyo havina umeme vitapatiwa umeme.
Makamba amesema kumekuwa na changamoto ya Mkandarasi na kupanda kwa bei ya vifaa katika mwaka ambapo katika mwaka uliopita bei zilipanda kwa asilimia 140.
“Tumezungumza na wakadarasi ili kutupa unafuu wa bei na tumeingia mikataba mipya ili kuendana na uhalisia,” amesema Makamba.
Aidha amesema katika wilaya ya Sikonge kuna mambo matatu makubwa ikiwemo uhakika wa upatikanaji wa umeme “yaani umeme kufika bila kukatikakatika imekuwa ni changamoto ya muda mrefu lakini tumeishughulikia kwa kupunguza urefu wa waya unaoleta umeme katika wilaya zote za mkoa wa Tabora.”
Amesema wakati mkoa wa Tabora unategemea umeme kutoka katika kituo cha Kaloleni cha Tabora mjini waya unaotumika kusambaza umeme ni wa KV 33 ambao unapaswa kusafirisha umeme kwa kilometa 100 tu.
“Lakini hapa Tabora unasafirisha kwa kilometa 1,200 kwahiyo umeme kwa maeneo mengi unafika ukiwa unafifia na hauna nguvu,” amesema.
“Kazi ambayo tumeifanya kwa kipindi cha miezi sita ni kupunguza urefu wa waya unaopeleka umeme maeneo mbalimbali tumeanza na Kaliua na Sikonge kwahiyo wilaya hizo zitapata umeme kwa uhakika zaidi.”

Amesema kazi nyingine ni ujenzi wa kituo cha kupooza umeme Sikonge ambacho ni sehemu ya mradi wa kutoa umeme kutoka Tabora kupitia Sikonge kwenda Mpanda Katavi.
“Mradi huo tunaugharamia sisi Serikali kwa fedha zetu na tunashukuru sana Mheshimiwa Rais kutupatia Sh. 500 bilioni katika bajeti inayokuja,”
Amesema baada ya kupata fedha hizo ujenzi utaenda kwa haraka zaidi na watasimamia kwa karibu zaidi, “ukweli kilichopo sasa hivi hakiendani na thamani ya fedha ambayo imetumika.”
Leave a comment