January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vijembe vyatawala CCM Mtera

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde

Spread the love

WAPAMBE wa wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaowania kuteuliwa kugombea nafasi za udiwani na ubunge katika chama hicho, wameanza kupigana vijembe kwenye kinyan’ganyiro hicho. Anaandika Dany Tibason, Mtera … (endelea).

Ikiwa zimebaki saa chache kabla zoezi la kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kuwania nafasi hizo kufungwa, wagombea nafasi ya ubunge katika Jimbo la Mtera wameshambuliana kwa maneno makali na kejeli.

Mbunge wa sasa anaetetea nasi yake katika jimbo hilo, Livingstone Lusinde ameshambuliwa vikali na wapinzani wenzake ndani ya CCM wakidai hana elimu na ni bingwa wa matusi.

Watangaza nia katika jimbo hilo hadi sasa wamefikia wanane ambao kila mmoja kwa wakati wake wameonekana kumkebehi Lusinde ambaye ameliongoza jimbo hilo kwa miaka mitano sasa.

Hali ya kumshambulia Lusinde inatokana na kauli yake ambayo aliitoa wakati anachukua fomu ya kuomba ridhaa ya kutetea nafasi hiyo tena.

Lusinde akichukua fomu Alhamisi wiki hii huku akiambatana na wachungaji ambapo aliwabeza wenzake  na kusema, wanaCCM wengi ambao wanachukua fomu badala ya kumtanguliza Mungu wanaenda Bagamoyo kwa waganga wa kienyeji.

“Mimi nimemtanguliza Mungu ndio maana nimesindikizwa na viongozi wa dini sio kama wenzangu ambao wakipata nafasi kama hizi badala ya kumtanguliza Mungu wanaenda kwa waganga wa kienyeji” amesema.

Maneno hayo ya Lusinde yalionekana kuibua hasira zaidi kwa wapambe wa wagombea na kusema maneno ya Lusinde sio ya kweli kwani hawezi kujificha katika kivuli cha dini.

Miongoni mwa wakazi wa Kata ya Mvumi, Makulu walioshangaa kauli ya Lusinde ni Daniel Lewanga.

Lewanga amesema, kauli ya Lusinde kwamba anaongozana na viongozi wa dini ni ya kujifurahisha mwenywe.

Amesema, kwa sasa Mtera imevurugika kutokana na kuwepo kwa makundi makuu mawili ambayo yanasababisha kuwepo kwa machafuko na machukizo katika hilo.

Bila kuyataja makundi hayo Lewanga amesema, kwa sasa jimbo la Mtera limekuwa jimbo ambalo limejengewa chuki kwa kuwachonganisaha vijana wenyewe kwa wenyewe jambo ambalo linafikia hatua ya wao kwa wao kutoana ngeu.

“Kwa sasa jimbo la Mtera tunataka Magufuli mpya hatutaki mtu mwenye jina na wala Lusinde asijidai kuwa yeye ni mtu wa Mungu tumeona wapo viongozi ambao walikuwa na makundi ya watumishi wa Mungu lakini leo wamewekwa pembeni hivyo ni wazi kuwa Chaguo la Mungu katika jimbo la Mtera litaonekana wakati ukifika,” amesema Lewanga.

Mbali na hilo Lewanga amesema, kati ya majimbo ambayo yanatia aibu ni jimbo la Mtera kwani unapojitambulisha mahali popote unaambiwa kuwa unatoka katika jimbo la mtukanaji maarufu hali ambayo hatutaki ijirudie tena.

Kwa upande wake Lusinde alipoulizwa juu ya kauli zake za kutukana alisema, wana Mtera wanashindwa kutofautisha maneno makali na matusi.

Naye mtangaza nia ya kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya ubunge kupitia CCM katika jimbo la Mtera, Philipo Elieza amesema, si busara kufanya siasa za chuki, kashifa wala kuwatumia vijana kwa ajili ya kupigana na kutoana damu.

“Chama chetu kinaamini zaidi katika umoja, upendo na mshikamano, nilazima tujenge nyumba moja hata hivyo vyama vyote kufanya siasa ambazo zinatawaliwa na hoja na wala siyo fuji kashifa wala mapigano ambayo yanaweza kusababisha umwakikaji wa damu” alisema Elieza.

error: Content is protected !!