January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vijana wawalee wazee

Spread the love

VIJANA wametakiwa kuwa karibu na wazee ili kujifunza maadili mema yatakayowasaidia kujenga uelewa wa kuwajibika juu ya kuwahudumia ipasavyo wazazi wao kimaisha wanapoingia uzeeni. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Hayo yameelezwa katika tamko la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Wazee yanayofanyika duniani kote kesho.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donan Mmbando amesema katika tamko hilo kwamba wazee wanayo nafasi kubwa katika maendeleo ya Taifa laTanzania kwa kutoa ujuzi, mila na desturi na kufanya ushauri patanishi katika migogoro inayoikumba jamii.

Dk. Mmbando amesema kitaifa, siku hiyo ya wazee inayoadhimishwa Oktoba mosi kila mwaka, itaadhimishwa wilayani Kasulu mkoani Kigoma chini ya kaulimbiu ya “Umuhimu wa kuwashirikisha Wazee kwa ustawi endelevu mijini.”

Dk. Mmbando amesema Tanzania itashirikiana na mataifa yote duniani kutafakari nafasi ya wazee katika jamii na mahitaji yao, fursa zilizopo pamoja na changamoto za ushiriki wao katika kupanga namna vya kuwasaidia kumaliza maisha yao ya uzeeni.

Akieleza hali halisi ya maisha ya wazee nchini, Dk. Mmbando amesema wazee wanakabiliwa na umasikini na hali kuzidi kutokana na kukosa matunzo mazuri, lishe bora, ulinzi wa kisheria, uonevu na hata mauaji yanayotokana na imani potofu za kishirikina.

Amesema serikali imetekeleza baadhi ya mambo katika jitihada za kuwasaidia wazee kuishi maisha yaliyo bora kuliko ilivyo sasa. Baadhi ya mambo hayo ni kutoa msamaha wa kodi kwa majengo wanayoishi wazee wanaohudumiwa na serikali.

Amesema Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kama vile asasi za kijamii zinazosimamia malezi ya wazee pamoja na asasi za kimataifa zinazoshughulikia masuala ya wazee hususan shirika la HelpAge International.

Dk. Mmbando amesema ni vyema Watanzania wakaitumia siku hiyo kutafakari haki ambazo wazee wanastahili na kuweka mipango ya makusudi katika kupata haki hizo pamoja na kuthamini michango yao wakiwa kama rasilimali ya maendeleo ya Taifa.

error: Content is protected !!