January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vijana waathirika wakubwa wa mitandao

Spread the love

TAKWIMU zinaonyesha kwa kila sekunde 18 watu watano wanaathirika na makosa ya kimtandao huku waathirika wakubwa wa mitandao wakiwa ni vijana ambao ni theluthi mbili ya wanaotumia mitandao hiyo. Anaandika Ferdinand Shayo, Arusha … (endelea).

Akitoa takwimu hizo Mwanasheria wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia, Yunusi Msigati amesema hayo katika semina ya kuwajengea uwezo wataalamu na watekelezaji wa Sheria ya makosa ya kimtandao iliyojumuisha Maafisa wa Jeshi la Polisi, Wanasheria pamoja na Mahakimu kujadili mambo muhimu yatakayozingatiwa katika utekelezaji wa sheria.

Yunusi amesema kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kumesababisha huduma za kifedha na huduma za kiserikali kutolewa kwa njia ya mtandao hivyo sheria hiyo itasaidia kupunguza na kudhibiti makosa ya kimtandao akitolea mfano kiasi cha Sh. 114 bilioni hupotea duniani kutokana na wizi wa kimtandao.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sayansi na Teknolojia, Prisca Ulomi amesema kuwa kimsingi Tanzania ilichelewa kuwa na sheria ya makosa ya kimtandao hivyo kutoa mwanya kwa baadhi ya watu kuifanya kama kichaka cha kujifichia wahalifu wa mitandao.

Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Johakim Tiganga amesema kuwa mahakama zimejiandaa vyema kupokea kesi za makosa ya kimtandao na kuzitolea hukumu ili haki ipatikane kwa pande zote mbili mlalamikaji na mlalamikiwa.

Mwanasheria wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Alfred Kahonga amesema kuwa tayari polisi ina kitengo maalum cha kushughulika na makosa ya kimtandao pamoja na maabara ya kisasa ambayo imeshaanza kazi ya kubaini makosa ya kimtandao.

Alfred amesema kuwa jeshi la polisi lina wataalamu wa kutosha waliobobea kwenye masuala ya mitandao ambao watazifanyia kazi kesi za kimtandao ikiwemo upelelezi na uchunguzi.

error: Content is protected !!