January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vijana waaswa kuchagua kwa amani

Spread the love

VIJANA wametoa angalizo kwa wanaoshabikia vyama vya siasa kufanya ushabiki bila ya vurugu kufuatia siku chache zilizobaki kuelekea uchaguzi mkuu Octoba 25 mkwaka huu. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Hayo yamesemwa baada ya kujengeka kwa ari kubwa miongoni mwa vijana katika kushabikia siasa za kitaifa zilizosababisha mgawanyiko mkubwa wa utiifu kwa wanasiasa wakubwa wanaogombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.

Katika kuendeleza ushabiki huo unaogawika kwa kuzingatia mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.

Vijana wa jijini Dar es Salaam wamezidisha harakati za kuwashabikia wagombea hao kiasi cha kujipa kazi ya kuning’iniza bendera za wagombea hao kwenye makutano ya barabara kuu pamoja na barabara nyinginezo kuu.

Bendera nyingi zimekutwa kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma; barabara za Morogoro na Kawawa eneo la Magomeni, barabara ya Kawawa na Mwinjuma na eneo la Kimara.

Wakizungumza na MwanaHALISI Online kwa nyakati tofauti vijana hao wametoa rai kwa wananchi wa rika tofauti hasa wakilenga vijana ambao kwa mujibu wa taarifa za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndio wengi wa kiasi cha asilimia 65 ya wapigakura walioandikishwa nchini.

Vijana wengi ni wale waliotimia umri wa kupiga kura mwaka huu, ambao ni miaka 18 na kuendelea.

Brown Maheko, kijana mkazi wa Manzese amesema vijana wa Tanzania wanatakiwa kutambua kuna maisha baada ya uchaguzi hivyo ni vyema kushiriki katika kampeni kwa umakini wakiepuka vurugu zinazoweza kuchangia ukosefu wa amani.

Amewataka pia wagombea kujiandaa kisaikolojia kupokea matokeo na kusema “nawaomba wagombea wote wa kila ngazi kuwa wakubali atakayepita yeyote awe Rais, Mbunge hata Diwani ndiye atakayesimamia maendeleo ya wananchi wote… wajiandae kupokea matokeo mazuri na mabaya.”

Naye Hamza Kipanga, mkazi wa Magomeni amesema licha ya wananchi kutofanya vurugu pia watambue kuwa “uongozi unaokuja hautafanana na uongozi uliopita hivyo mabadiliko lazima yatakuwepo ingawa watu wengi wanashindwa kufuatilia tofauti baada ya uchaguzi.”

Ushabiki uliojitokeza siku chache kabla ya kura za wananchi kuongea ambapo itajulikana ni yupi kati ya Magufuli na Lowassa, ambao ndio wagombea wanaotoa ushindani mkubwa zaidi kati ya wagombea wanane wa nafasi hiyo, atakayepewa ridhaa ya kuongoza taifa.

error: Content is protected !!