August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vijana wa Chadema waigaragaza serikali kizimbani

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)

Spread the love

VIJANA saba kutoka vyuo vikuu mbalimbali mkoani Dodoma ambao ni wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameibwaga serikali katika kesi Na. 127 ya mwaka 2016 iliyokuwa ikiwakabili, anaandika Dany Tibason.

Vijana hao walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za kufanya maandamao bila kibali, kinyume cha vifungu 43 (4) 45, 46 (1) vya Sheria ya Jeshi la Polisi ambapo Godfrey Pius, Hakimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ametupilia mbali kesi hiyo kutokana na serikali kushindwa kutoa ushahidi usiotiliwa shaka.

Awali ilidaiwa kuwa, tarehe 18 Juni, mwaka huu katika Barabara ya wajenzi, Area D mjini Dodoma vijana hao waliandamana bila kuwa na kibali huku wakijua kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Waliokuwa wakishitakiwa kwa kesi hiyo ni Pasco Mbele, Andrew Komba, Anna Joseph, Joseph Buretha, Andrew Mwambene, Lukile Stanslaus na Rosse Mruchu.

Akisoma hukumu ya kesi hiyo, Hakimu Pius amesema amepitia ushahidi wa serikali na kubaini kuwa walalamikaji wameshindwa kuithibitishia, mahakama pasipo kuacha shaka kuwa kulikuwa na maandamano yaliyofanyika na hivyo kuwaona vijana hao kuwa hawana hatia na kuwaaachia huru.

Amesema kuwa upande wa mashitaka ulipeleka mashahidi wanne ambao wote walieleza kuwa wanafunzi walikuwa ndani ukumbi wa hoteli ya African Dream walipokutana kwa lengo la kufanya mahafali ya Chaso na kwamba Polisi ndio walioenda kuwaondoa katika ukumbi bila kusema sababu za kufanya hivyo.

Pia imeelezwa kuwa menejimenti ya hoteli hiyo haikuwa imelalamika juu ya kuwepo uvinjifu wa amani katika eneo hilo kwahiyo hakukuwa na haja ya Polisi kufika na kusambaratisha kusanyiko hilo.

Hakimu Pius ameongeza kuwa upande wa mashahidi wa serikali, waliulizwa kama kuna mtu ambaye alifanyiwa fujo au kama waliwaelekeza wanafunzi hao njia ya kupita baada ya kuwafukuza katika eneo hilo lakini walikiri kuwa hakuna mtu aliyefanyiwa fujo wala polisi hawakuwaelekeza njia ya kupita.

Hakimu huyo ameeleza kuwa amri ya kuwatawanya wanafunzi hao kutoka katika hoteli husika haikuwa na mashiko yoyote na kwamba wanafunzi hao walikuwa wana haki ya kukusanyika katika eneo hilo kwa madhumuni husika bila kubughudhiwa na hoja kuwa waliondoka kwa mandamano haina mashiko pia.

Katika shauri hilo, serikali ilikuwa ikiwakilisha na mwendesha mashitaka Morice Sarara huku upande wa wanafunzi hao ukiwakilishwa na wakili wa kijitegemea Elias Machibya.

Itakumbukwa kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lilisambaratisha mahafali yaliyokuwa yameandaliwa na Umoja wa Wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni wanachama wa Chadema (Chaso), ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye huku vijana waliokuwa wakitawanyika wakikamatwa kwa tuhuma za kuandamana bila kibali.

error: Content is protected !!