NUSRAT Hanje, Mbunge wa Viti Maalum asiye na chama bungeni, ameihoji serikali ni kwanini haioni umuhimu wa kurekebisha mfumo wa elimu na kuingiza mbinu tete za stadi za maisha ili kuwajengea uwezo wa kiushindani vijana wanaohitimu. Anaripoti Nasra Bakari na Jemima Samweli, DMC … (endelea).
Hayo yamesemwa leo Ijumaa, tarehe 30 April 2021, bungeni jijini Dodoma, katika kipindi cha maswali na majibu.
“Je, ni kwanini serikali, haioni umuhimu wa kurekebisha mfumo wa elimu na kuingiza mbinu tete za stadi za maisha ili kuwajengea uwezo wa kiushindani vijana wanaohitimu na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira,” alihoji Hanje
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga alisema, Serikali inatambua umuhimu wa kuwawezesha wanafunzi kupata stadi za maisha na mbinu tete ili kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo swala la ajira.
Alisema, Serikali imekuwa ikiboresha mitaala kila kunapokuwa na hitaji la kisayansi, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kiteknolojia.
“Katika kipindi cha mwaka 2021/2022, Serikali itafanya mapitio ya mitaala ya shule za msingi na sekondari ili kuingiza stadi mbalimbali kama vile stadi za maisha hususani stadi za karne ya 21 na mbinu tete,” alisema Kipanga na kuongeza:
“Stadi za Karne ya 21 ni pamoja na tunduizi, ubunifu, ushirikiano, uongozi na stadi za teknolojia ya habari na mawasiliano stadi na mbinu hizi zitasaidia kuwajengea vijana uwezo wa kiushindani katika soko la ajira.” Alisema
Leave a comment