October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vijana ACT-Wazalendo waomba ‘sapoti’ ajenda tume huru kuelekea katiba mpya

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT-Wazalendo Dar es Salaam, Felix Kamugisha

Spread the love

 

NGOME ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo, Mkoa wa Dar es Salaam, imewaomba vijana wa vyama vya siasa vya upinzani, waunge mkono ajenda ya chama chao ya upatikanaji tume huru ya uchaguzi, kuelekea katiba mpya. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Alhamisi, tarehe 7 Aprili 2022 na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT-Wazalendo Dar es Salaam, Felix Kamugisha, akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu.

“Lazima tuweke shinikizo la upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi, itakayowezesha kupatikana kwa katiba mpya. Tunaomba sana wenzetu watuelewe katika hili, lengo letu ni moja sena aina tunayopita ni tofauti,” amesema Kamugisa.

Kamugisha ametoa wito huo akisema, kumekuwa na mvutano kati ya vijana wa vyama vya siasa vya upinzani, juu ya nini kianze kupiganiwa ili kipatikane, kati ya tume huru ya uchaguzi na katiba mpya.

“Nimetoa wito huu kwa sababu sisi tunavutana sana, kuna wengine wanaamini kwenye katiba mpya kwanza, na sisi tunaimani kwenye tume huru itakayotueletea katiba mpya. Ni sawa na kusema wote mnaenda Dodoma, huyu anasafiri kwa treni na mwingine kwa basi lakini lengo letu sote tufike Dodoma,” amesema Kamugisha.

Mwenyekiti huyo wa vijana ACT-Wazalendo Dar es Salaam, amesema chama chake kimefanya tathimini na kuona kuna haja ya tume huru ya uchaguzi kupatikana kwanza, kwa kuwa ndiyo itakuwa msimamizi wa mchakato wa upatikanaji wa katiba hiyo.

“2020 hakukuwa na uchaguzi na sisi ACT-Wazalendo tukaulizana tunahitaji katiba kwa muundo na mfumo huu? Tukasema hapana, mazingira tuliyo nayo ambayo bunge la katiba litajumuisha wabunge ambao hawajachaguliwa na wananchi. Hivyo lazima twende na tume ili kuipata wawakilishi halali watakaounda Bunge la Katiba,” amesema Kamugisha na kuongeza:

“Haya ndiyo baadhi ya chama tuliyatizama, lakini tulitizama mpaka 2024 kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na 2025 kwenye uchaguzi mkuu, tukitizama kama tutakuwa na uwezekano wa kupata katiba, hakuna.”

error: Content is protected !!