September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vijana ACT-Wazalendo, wamuomba Membe kujiunga nao

Spread the love

NGOME ya vijana ya chama cha ACT- Wazalendo, kimemuomba aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bernard Kamilius  Membe, kujiunga na chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya Ngome hiyo iliyosambazwa kwa umma kupitia mitandao ya kijamii, imeeleza kuwa Vijana wa chama hicho, wanamkaribisha Membe “kujiunga na chama chao, kwa mikono miwili.” 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ngome ya vijana wa ACT – Wazalendo, imeamua kumuandikia barua kwa Mwenyekiti wao wa kamati ya uongozi, Maalim Seif Sharif Hamad, ili kuonesha msimamo wao juu ya hamu na shauku ya kumkaribisha Membe kujiunga na chama chao.”

          Soma zaidi:- 

Mbali na kumuanidkia barua Maalim Seif, vijana hao wameamua kumuandikia barua rasmi, Membe kumuomba ajiunge na chama hicho ambacho kimekuwa kikikuwa kwa kasi nchini.

“Viongozi wengi wa chama chetu ni wahanga wa uvunjifu wa demokrasia kutoka kwenye vyama vyao vya awali, hivyo Act Wazalendo ni jukwaa la wahanga wa wote wa demokrasia, akiwamo Membe mwenyewe,” inaeleza taarifa hiyo.

Inasema, Membe ni muhanga wa demokrasia ndani ya CCM baada ya kuvuliwa uwanachama wake.

Kosa la Membe, vijana wa Ngome ya ACT- Wazalendo wanasema, ni kutumia uhuru wake wa kidemokrasia wa kutoa maoni, kukosoa na kushauri serikali iliyopo madarakani juu ya uminywaji wa demokrasia na haki nchini.

“Mheshimiwa Membe pia alivuliwa uwanachama wake baada ya kuonesha dhahiri dhamira yake ya kugombea urais  kupitia CCM. Hivyo kwa madhila haya Membe ni mhanga wa demokrasia ndani ya Chama Cha Mapinduzi na jukwaa lake rasmi la kuendeleza mapambano hayo, linapaswa kuwa ACT Wazalendo,” inaeleza taarifa hiyo.

Inaongeza: “Tunasisitiza msimamo wetu wa kumuomba Mh.Membe kujiunga na chama chetu kwasababu ni wajibu wetu kama vijana na wanachama kwani katiba yetu  ibara ya 12(4) inatoa majukumu kwa wanachama ‘kushawishi wananchi kujiunga na chama chetu’ hivyo tunaomba na kutamani Mheshimiwa Membe ajiunge na chama chetu ili kuendeleza mapambano hayo.”

Vijana wa ACT- Wazalendo wanasema, “hata kama Membe akiamua kutia nia ya kugombea nafasi ya ngazi yeyote katika uchaguzi huu mkuu wa Oktoba 2020, hakuna shida kwa sababu chama chetu kinaamini katika msingi wa usawa kwa wanachama wote bila kujali ana muda gani ndani ya chama.

“Katiba yetu Ibara ya 11(3) inatoa haki kwa kila mwanachama kuchagua na kuchaguliwa, na kwmaba Ibara ya 6(1) misingi ya chama, msingi wa 7 wa chama chetu ni  demokrasia.”

Ngome ya Vijana ACT- Wazalendo inaeleza kuwa hatua ya baadhi ya watu kumfananisha Membe na waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ni makosa makubwa sana.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe

“Kuna utofauti mkubwa sana kati ya wanasiasa hawa wawili. Lowasa aliondoka CCM akiwa na sababu moja tu ya kutafuta jukwaa la kugombea urais baada ya kutopitishwa na chama chake katika kura za maoni. Hivyo akaamua kuhama chama.

Membe amefukuzwa uwanachama kwa ujasiri wa kutoa maoni yake, ushauri na kukosoa serikali ya CCM.

“Pia Membe alinyimwa haki ya kikatiba baada ya kutangaza dhamira ya kugombea nafasi ya uras ndani ya CCM mwishowe alifukuzwa baada ya kuogopwa na CCM. Huyu ni muhanga wa Demokrasia ndio maana Ngome ya vijana tunamuhitaji ili apate jukwaa la kuendeleza mapambano ndani ya chama chetu dhidi ya CCM.

“Ngome ya Vijana ACT wazalendo tunaomba viongozi wa chama chetu kuchukua hatua ya kumkaribisha muhanga mwenzetu kujiunga na chama chetu,” inaeleza taarifa hiyo.

error: Content is protected !!