May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vijana ACT-Wazalendo walilia ushirikishwaji mpango wa maendeleo ya Taifa

Spread the love

 

VIJANA nchini Tanzania wameiomba Serikali kutowaacha nyuma katika utekelezaji wa Mpango wa Dira ya Maendeleo ya Taifa wa 2025 ili kujenga Taifa lililo bora. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Leonid Tairo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana duniani yaliyofanyika makao makuu ya chama hicho Kijitonyama jijini Dar es Salaam jana Alhamisi tarehe 12 Agosti 2021.

Alisema mpango wa Dira ya Maendeleo ya Taifa unaotarajia kufika kilele chake 2025 hauwezi kuwa na tija endapo vijana hawatashirikishwa ipasavyo katika nyanja mbalimbali.

Mbali na hilo, Mwenyekiti huyo alisema uandikaji wa Katiba mpya Tanzania ni moja ya takwa la msingi kwa vijana kwani itawahakikishia fursa mbalimbali kuanzia kizazi cha sasa na kijacho.

Tairo alisema ni jukumu la vijana kushikamana kuhakikisha Taifa linapata Katiba mpya pamoja na Tume huru ya Uchaguzi kwa kushirikiana na makundi mengine ya kijamii, zikiwamo asasi za kiraia, taasisi za dini na makundi mengine yanayopigania upatikanaji wa Katiba mpya na Tume ya Uchaguzi iliyoridhiwa na Watanzania.

“Sisi vijana wa Dar es Salaam tunapendekeza kwa Serikali ishirikishe vijana katika upangaji, utekelezaji, usimamizi na tathmini mbalimbali ya maendeleo katika jamii.”

“Hivi sasa robo tatu ya vijana nchini wamejiajiri katika sekta isiyokuwa rasmi wakiwamo wale wanaomaliza vyuo mbalimbali bila kuwa na uhakika wa ajira wala mitaji ya kuwaeezesha kujiajiri jambo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee na kupatiwa suluhisho la kudumu,” alisema

Katika hatua nyingine, Tairo aliwataka vijana nchini kujenga utamaduni wa kushiriki shughuli za maendeleo sambamba na kuhudhuria vikao vya kijamii katika maeneo yao pamoja na kipenda kujisomea vitabu na maandiko mbalimbali ili kujenga uelewa kwa mambo mbalimbali.

error: Content is protected !!