Spread the love

 

AWAMU ya Pili ya ‘shusha Tanga pandisha tanga’ ya Chama cha ACT-Wazalendo imetajwa kuwa na kishindo baada ya viongozi waandamizi kutoka chama cha Wananchi CUF kutajwa kujiandaa kutimkia Chama cha ACT Wazalendo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tarehe 19 Machi 2022, imetajwa kuwa ni siku ya kuwapokea viongozi hao ambao wanadaiwa wameshamaliza mazungumzo na viongozi wa ACT na kwamba watapata mapokezi ya heshima kutokana na uzito wa nafasi zao.

Chanzo cha uhakika kimemueleza Mwanahalisi Online kuwa viongozi hao wamechukua hatua hiyo baada ya kukasirishwa na kitendo cha Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kukififisha siasa ndani ya chama hicho.

CUF kilichokuwa chama kikuu cha upinzani Visiwani Zanzibar na cha pili kwa ukubwa Tanzania bara sasa nafasi yake imechukuliwa na ACT-Wazalendo.

Chanzo kimenukuliwa kikieleza kuwa wafuasi hao wa chama hicho wanaeleza kuwa CUF imeshindwa kushuka chini kufanya siasa.

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF

“Huko chini hatuna chama viongozi wa kata, matawi wametawanyika hawatembelewi na viongozi, tumejifungia Buguruni watu wetu hawajui mwenendo wa chama, hawajui mikakati wamekata tamaa wao wanadhani siasa ni kubishana na ACT tu!

“ACT wenzetu wanafanya kazi ya siasa wanafanya ziara, wanayasemea masuala ya wananchi, sasa wana baraza la mawaziri vivuli lengo kuyasema matatizo ya wananchi hiyo ndio kazi ya chama cha siasa” ameleeza mmoja wa makada wa CUF waliopanga kuhamia ACT Wazalendo.

Kada huyo amewataja baadhi ya wanachama hao kuwa ni pamoja Makamu Mwenyekiti CUF-Bara, Maftaha Namchuma; aliyekuwa Katibu wa Uenezi, na Mahusiano ya Umma, Abdul Kambaya na aliyekuwa Mgombea wa CUF katika Uchaguzi Mkuu 2020 Kigoma Kusini, Kiza Mayeye.

Wengine ni pamoja na Mahmoud Mahinda aliyekuwa Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa CUF(Juv-CUF), aliyekuwa Mbunge wa Chadema Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi.

Aidha, chanzo hicho kimeeleza wengine wameanza kufanya mazungumzo na uongozi wa ACT-Wazalendo wiki hii ili nao wajiunge kwa pamoja siku ya tarehe 19 Machi mwaka Manzese jijini Dar es Salaam ambapo ACT itakuwa inazindua rasmi Operesheni ya Tume Huru ya uchaguzi.

Aidha, akizungumzia madai hayo Kambaya alikanusha kufanya mazungumzo na viongozi wa ACT Wazalendo kwa lengo la kuhamia ndani ya chama hicho.

“Sijawahi kuzungumza na kiongozi yoyote wa ACT-Wazalendo kama tunahitajiana labda mazungumzo ya kawaida ya kijamii kwa sababu ndani ya ACT, wapo rafiki zangu na ndugu zangu kwenye siasa” amesema Kambaya.

Ameeleza kuwa anamazungumzo ya kawaida na Zitto Kabwe kama rafiki yake kwenye siasa na Ado kwa kuwa yeye alipokuwa kwenye idara ya uenezi kwa nafasi ya Ukatibu na Ado alikuwa kwenye nafasi hiyo kwenye ACT.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo

Amesema kuwa kwa sasa hajakuwa na uamuzi wowote kwa kuwa yeye ana malalamiko yake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa anayolalamikia kuondolewa kwake kwenye chama hicho.

Aidha, akizungumzia ujio wa makada hao wa CUF Katibu Mkuu wa ACT Wazalendi, Ado Shaibu amekiri kuwepo kwa operesheni ya shusha tanga awamu ya pili ambayo ameitaja kuwa itakuwa na kishindo

“Tangu tumemaliza uchaguzi Mkuu chama chetu kimepokea maombi ya wanachama waandamizi kutoka CUF wanaotaka kujiunga na chama chetu”.

Aidha, alipoulizwa juu ya majina ya wanachama na viongozi anaowadai kuwa atawapokea amejibu “Tusivuke mto kabla ya kuufikia tusubiri muda muafaka”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *