January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vigogo wamuaga Edson Kamukara

Mwenyekiti wa MOAT, Reginald Mengi akiaga mwili wa Marehemu Edson Kamukara

Mwenyekiti wa MOAT, Reginald Mengi akiaga mwili wa Marehemu Edson Kamukara

Spread the love

VILIO vimetawala katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakati wa kuaga mwili wa Edson Kamukara, Mhariri mwanzilishi wa MwanaHALISI Online. Anaripoti Sarafina Lidwino … (endelea).

Kila aliyesimama kuzungumza aliishia kuangusha chozi; wakikumbuka kazi nzuri iliyofanywa na Kamukara, mmoja wa wandishi wa habari mahiri nchini.

Kamukara aliyefariki dunia katika mazingira yaliyosheheni utata, Alhamisi 25 Juni mwaka huu, nyumbani kwake, Mabibo jijini Dar es Salaam, anatarajiwa kuzikwa Jumatatu wiki ijayo, nyumbani kwao Muleba, mkoani Kagera.

Miongoni mwa waliofika kutoa heshima za mwisho kwa Kamukara, ni pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), Reginald Mengi na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Wengine, ni Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Sued Kagasheki; Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa; Katibu wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Nevile Meena na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.

Aidha, walikuwapo pia maofisa Habari wa vyama vya The Civic United Front (CUF) – Silas Bwire; ACT- Wazalendo, Abdalah Khamisi na  Tumaini Makene kutoka Chadema. 

Alikuwa ni mkurugenzi mteandaji wa Hali Halisi Publishers Limited, Saed Kubenea, aliyeanza kububujikwa na machozi, pale Nevile Meena, alipoanza kueleza uadilifu, nidhamu na uchapakazi wa Kamukara.

Meena alisema, Kamukara ni miongoni mwa waandishi wa habari wa chache nchini, wanaofanya kazi zao kwa uadilifu na kufuata miiko ya uandishi.

“Sisi katika vyombo vya habari, tulikuwa tunamuona Kamukara kama mtu ambaye anaweza kukabidhiwa jukumu kubwa la kuongoza chombo cha habari siku zijazo. Lakini leo, mwenzetu huyu ametangulia mbele ya haki. Ni vema tukamuenzi kwa kufuata nyayo zake,” ameeleza Meena.

Amesema, tasnia ya habari imempoteza mtu jasiri na aliyekuwa na weledi mkubwa katika utendaji wake wa kazi.

 “Tumepoteza mtu jasiri, mahiri, asiyedanganyika na mwenye msimamo imara katika kazi yake,” alisisitiza Meena.

Naye Mbowe alisema, maslahi ya waandishi wa habari nchini, ni duni sana. Waandishi wengi hawana bima ambazo zingesaidia familia zao.

Amesema, “Nichukue nafasi hii, hasa kwa kuwa hapa yupo mwenyekiti wa MOAT, Reginald Mengi, nitoe ombi kwa wamiliki wa vyombo vya habari, tuweke utaratibu wa kuwawekea bima ili iweze kusaidia waandishi.”

Mbowe amesema, umuhimu wa kuwa na bima ni mkubwa kwa kuwa “maslahi ya waandishi ni madogo.” Amesema, ikiwa waandishi watawekewa bima, itawasaidia kuendesha familia zao, pale wanapokutwa na mauti.

Akimzungumzia Kamukara, Mbowe alisema, “Edson (Kamukara), alikuwa mwandishi wa habari asiyetegemea bahasha.”

Amesema, “…alikuwa mkweli, mwadilifu na mchapa kazi. Ni vema waandishi wakamuenzi kwa kufuata matendo yake.”

Kwa upande wake, Mengi aliwataka waandishi wa habari kusimamia maadili katika uandishi wao, ikiwa ni pamoja na kuepuka rushwa kama alivyokuwa Kamukara.

Amesema, “Mimi sitaki kutafuna maneno. Kamukara amekufa wakati akifuatilia habari moja kubwa. Katika siku za hivi karibuni, alikataa mamilioni ya pesa ambayo aliahidiwa kama angeacha kuchunguza kuandika habari hiyo, lakini yeye alikataa kupokea pesa hizo na akaandika habari na kuitoa.”

Mengi ambaye ni Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP amesema, waandishi hawapasi kuendekeza rushwa katika kazi zao.

“Rushwa ni tabia ya mtu, sio kwamba ukiwa na kipato kidogo ndio sababu ya kupokea rushwa.”

Makonda alitaka waandishi kupigania maslahi yao kwa kupewa mikataba ya kazi na waajiri wao. Alidai kuwa zaidi ya asilimia 80 ya waandishi hawana mikataba.

 “Mikataba ya waandishi ndiyo itamaliza bahasha kwa waandishi,” amesema Mkonda na kuongeza, “la sivyo bahasha hizo zitaendelea kuwepo.”

Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Balozi Kagasheki amesema, amemfahamu Kamukara kutokana na ushujaa wake kwenye tasnia ya uandishi.

Amesema, sifa na ujasiri wa Kamukara tayari umezungumzwa na watu waliotangulia na kwamba, kinachopaswa ni kumuombea marehemu ili Mwenyezi Mungu amuweke pema.

Naye Kubenea alisema, kampuni ambayo imekuwa mwajiri wa Edson Kamukara kwa miezi minne na siku tatu sasa – HHPLimited – “imepata pigo.”

Amesema, “Ni masikitiko makubwa. Ni uchungu usio na kiwango. Ni ukiwa usiozibika. Tumeondokewa na ndugu. Tumeondokewa na rafiki. Lakini zaidi, tumeondokewa na mchapapakazi. Tulimpenda sana Edson.  Tuseme kweli; naye alitupenda.”

Amesema, “Tulifanya naye kazi kwa uelewano mkubwa. Tulithamini mawazo yake kama yeye alivyothamini ya kila mmoja wetu. Kwa hakika, tutamkosa na pengo ambalo ametuachia, haliwezi kuzibika.”

Kubenea ambaye mara kwa mara hotuba yake ilikuwa inakatizwa na kilio, aliwashukuru wote walioungana na kampuni yake katika msiba huo mkubwa.

error: Content is protected !!