Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Vigogo wachambua vigezo Chato kuwa mkoa
Makala & UchambuziTangulizi

Vigogo wachambua vigezo Chato kuwa mkoa

Jengo la Wilaya ya Chato
Spread the love

 

MAPENDEKEZO ya kuundwa kwa mkoa mpya wa Chato, yametibua hali ya hewa na kuibua mjadala mzito. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Chato ni mahali alikozaliwa hayati John Pombe Magufuli, Rais wa awamu ya tano, aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, Dar es Salaam.

Mchakato wa kuifanya Chato mkoa, ulianzishwa na Hayati Magufuli mwenyewe na hivi sasa mjadala wa kutimiza ndoto yake, umeonekana kuligawa Taifa.

Siku ya maziko ya Hayati Magafuli, tarehe 26 Machi 2021, nyumbani kwao, Chato mkoani Geita, wazee wa Chato walimwomba Rais Samia Suluhu Hassan, kukamilisha mchakato huo.

Hata hivyo, Rais Samia, alisema mchakato huo uendelee kwa ngazi husika na ikiwa vigezo vya kuufanya kuwa mkoa vitatimia, hakuna tatizo.

Tayari mgawanyiko umeanza kuonekana kati ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Geita (RCC) na Baraza la Madiwani la Geita.

Wiki iliyopita RCC, ilipitisha mapendekezo ya kuundwa kwa mkoa mpya wa Chato, lengo likiwa kutaka kutimiza ndoto za Magufuli, lakini Baraza la Madiwani likapinga.

Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania

Mwenyekiti wa RCC ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule, alisema kamati imependekeza wilaya tano, Chato na Bukombe mkoani Geita. Biharamulo na Ngara mkoani Kagera na sehemu ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma zichukuliwe kwa ajili ya kuanzisha Mkoa mpya wa Chato.

Katika mitandao ya kijamii, kumekuwapo na maandiko mbalimbali ya viongozi wa dini, wanasiasa na wadau kadhaa wanaopinga mapendekezo hayo.

Mmoja wa wanasiasa maarufu nchini, Profesa Anna Tibaijuka, amesema bila kumung’unya maneno, kuwa Chato haina vigezo vya kuwa mkoa.

Profesa Tibaijuka, anaandika akisema: “Ramani inaonesha kuwa wilaya ya Chato ni sehemu ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera. Kiuhalisia na kihistoria. Mengine ni kulazimishalazimisha tu.

Hayati John Magufuli

Profesa Tibaijuka ambaye amepata kuwa mbunge na waziri, amesisitiza hakuna hoja yoyote ya kiuchumi ya kuunda mkoa wa Chato, vinginevyo wananchi wanahitaji kuelimishwa.
“Ila kama mnapenda siasa za upendeleo wa sehemu fulani ama kwa kuwa mkubwa aliwahi kuzaliwa pale, au mtu apewe nafasi kwa sababu ni mtoto wa kiongozi, basi endeleeni kuwabebesha wananchi mizigo ya kulipa kodi kusudi wateule wajichane,” anasema na kuongeza:

“Kwanza, ikumbukwe kuwa mkoa wa Geita ulianzishwa kusudi Chato iwe makao makuu. Ikakosa vigezo. Geita mjini ikaonekana ndiyo yenye sifa za kuwa makao makuu ya mkoa mpya wa Geita.”

“Hii ilikuwa mwaka 2010. Sasa miaka 11 imepita, Chato eti ina vigezo kuwa makao makuu ya mkoa wake yenyewe? Tuko makini na maendeleo yetu kweli?

Prof. Anna Tibaijuka

“Na Rais wetu mpendwa, Samia Suluhu Hassan, tunataka kweli kumtwisha zigo la kuamua jambo hili na utata wake? Elimu haina mwisho. Mimi kama kuna vigezo naomba viorodheshwe.

“Labda ndiye sina taarifa. Ila kwa maana ya hoja ya kuwaletea maendeleo watu wa Kakonko, Biharamulo, Ngara na Muleba inayokatwa vipande, hakika ninazikataa.”

Aliendelea kusema: “Mkoa unaweza kuleta maendeleo gani kwa wilaya yake, wakati mkoa unategemea bajeti ya Serikali Kuu? Mkoa una mapato gani zaidi ya kutumia kodi? Tuwe makini.

“Maendeleo yanatokana na uwekezaji na uwezeshaji kwa wananchi. Si watumishi wa Serikali, tena baadhi bila maadili wanaweza kuishia kuwabughudhi wananchi badala ya kuwa msaada.”

Askofu Benson Kagonza, KKKT Dayosisi ya Karagwe

Anasema: “Njia pekee ya kumuenzi hayati Magufuli, aliyekuwa Rais, ni kurekebisha mambo ambayo kama binadamu hakufanya vizuri. Mengine yote ni ubinafsi. Na kufifisha sifa zake katika historia ya nchi hii. Tumwache apumzike.”

Anasema kuwa miundombinu iliyowekwa Chato si kigezo cha kuunda mkoa, hivyo ikamilishwe na kuitafutia matumizi mbadala ya kitaifa.

“Mfano uwanja wa ndege wa Chato, unaweza kufanywa kituo kikuu cha kilimo mkataba cha maua na mboga, ili tuwe na ndege za mizigo kuja kubeba. Na maziwa.

“Hospitali ya Kanda Chato. Naomba tutathmini kwanza maendeleo ya hospitali ya Mloganzila. Majengo ya kisasa yaliyopo umbali wa kilometa 40 tu kutoka katikati ya Jiji na Muhimbili. Mojawapo ya mafanikio makubwa ya Awamu ya Nne.
“Lakini angalia changamoto zake. Uhaba wa madaktari hadi leo. Sasa hao madaktari bingwa, watakaokubali kuishi Chato mtawalipa fedha kiasi gani?

“Hospitali si majengo pekee. Ni pamoja na rasilimaliwatu na uchumi mzuri kuzunguka eneo husika. Katika dhana ya mipango miji na maendeleo ya makazi, lazima vigezo vyote hivyo kuangaliwa. Kwa uelewa wangu, Chato haina vigezo. Tusidanganyane.” Profesa Tibaijuka aliwahi pia kufanya kazi katyiak Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat).

Askofu Severine Niwemugizi

Kwa upande wake, Askofu Severine Niwemugizi, alisema: “Tumesikia mapendekezo ya kikao cha ushauri cha mkoa wa Geita kuhusu uundwaji wa mkoa mpya wa Chato. Lakini ushauri wa mkoa wa Geita tu hautoshi kufanya uamuzi. Kagera zaidi inahusika katika hili, kama wilaya zake mbili zitamegwa.

Askofu Severine Niwemugizi, Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara

Askofu huyo anaongeza: “Ingetazamwa historia, mkoa usingeitwa Chato. Mtawala wa kijerumani aliweka ngome ya utawala wake Biharamulo, akiheshimu kuwa hapo palikuwa makao ya Chifu wa Rusubi, Chato ikiwa sehemu yake. Na hata hayati JPM (John Magufuli) alianza harakati za kisiasa ikiwa Chato ni sehemu ya wilaya ya Biharamulo, na jimbo la uchaguzi la Biharamulo.

“Kwa haki nionavyo mimi, kugawa Kagera na Kigoma ili kuunda mkoa ingekuwa ni kutazama mahitaji ya raia zaidi. Ukweli wazo la awali katika Awamu ya nne, ilikuwa kuunda mkoa kwa kutenga Kigoma na Kagera.

“Ukizingatia, Kanda ya Magharibi ya Ukaguzi wa Elimu ina mikoa hii miwili. Fikiria makao ya Kanda ni Kigoma. Mtu anapaswa kusafiri zaidi ya kilometa 700 kutoka Bukoba hadi Kigoma!

“Najua mazungumzo yalishaanza. Halmashauri za Kakonko, Biharamulo na Kibondo zilishapiga hatua za kuafikiana kuunda mkoa. Ngara ingepanda basi hilo. Nilisikia makao makuu huenda yangekuwa Nyakanazi.

“Awamu ya tano ikaupiga mkasi mpango wa mkoa ule na kuanza wa Rubondo. Huu ulikuwa na msukumo unaoakisi ubinafsi tu. Yaani kutoka Geita hadi Chato kilometa zisizofika 100, uwe mkoa, wakati mtu anapiga kilometa 700 kutoka Bukoba hadi Kigoma! Inashangaza tunavyowaza na kupanga, si kwa maslahi ya raia, bali ya watawala.”

Askofu aliongeza kuwa “Mama Samia Suluhu Hassan asishinikizwe na kauli za kumpima, kwa kutekeleza mipango iliyokuwepo ya JPM. Ashauriwe vizuri kwa kutazama uhalisia wa mahitaji ya kiutawala na maendeleo ya watu. Kutangaza mkoa kwa kuenzi watawala tu, si kigezo kizuri, vinginevyo aanze na mkoa wa Butiama kwa Baba wa Taifa!”

Tafakuri ya Askofu Bagonza

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani kagera, Benson Bagonza anasema: “Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Geita (RCC) imeridhia uundwaji wa mkoa mpya wa Chato, lakini Baraza la Madiwani la Geita limepinga uundwaji wa mkoa mpya wa Chato. Mgongano huu uko wazi.”

Askofu Bagonza anasema: “RCC ni jopo la wateule. Mkoa na wilaya mpya ni fursa ya uteuzi. Kwa madiwani uundwaji wa mkoa mpya ni kero na mzigo kwa wananchi na wapiga kura wao, ndiyo maana wamepinga.

Anasema: “Lakini mkoa mpya unaopendekezwa ni kama mimba iliyotungwa nje ya kizazi. Tusipokuwa wakweli tutahatarisha maisha ya mama (Kagera, Geita, Kigoma na Mwanza).”

Uwanja wa Ndege wa Chato wakati unajengwa

Anasema kwanza ilitakiwa, Chato uwe mkoa ndipo ujengwe uwanja wa ndege, hospitali ya rufaa, ofisi zingine za kitaifa na kadhalika. Kosa la kiufundi lilifanyika kukata mbeleko kabla mtoto kuzaliwa.

Pili, anasema kama lengo ni kuenzi jina Chato, mkoa wa Geita ubadilishwe jina na kuitwa Chato na mambo mengine yabaki kama yalivyo. Iliwahi kubadili jina la mkoa wa Ziwa Magharibi kuwa Kagera.

Tatu, Askofu Bagonza anasema shughuli za maendeleo zinafanywa na Halmashauri si mikoa na wilaya, hivyo si dhambi wilaya moja kuwa na halmashauri hata tatu, zinazopendekezwa kuwa wilaya, ziwe halmashauri na maisha yasonge mbele.

Nne, anaongeza, “mkoa mpya unadhoofisha kiuchumi mikoa ya Kagera, Geita, Kigoma na hata Mwanza. Mkoa mpya unaanza na wilaya nyingi kuliko mikoa inayouunda. Kama ni dhambi mkoa kuwa mkubwa, kwa nini tunaunda mkoa mkubwa?”

Tano, anasema: “Mikoa na wilaya mpya zinagawa watu na kuvuruga mshikamano wa kihistoria. Utambulisho unavurugwa bila utaratibu. Hiki ni kikwazo cha maendeleo kwa sababu maendeleo si majengo.”

Hospitali ya Chato

Sita, Askofu Bagonza anasema: “Tanganyika ina utete fulani katika mikoa ya mipakani. Umakini inahitajika kuliko kufuata mivuto na hulka za kisiasa.”

Saba, anasema kama lengo ni kumuenzi hayati Rais Magufuli, hata Karagwe siku moja itadai mkoa wa Karagwe wenye wilaya za Bushangaro, Nyaishozi, Burigi na Karagwe, kwa sababu hayati aliwekeza huko na kuweka makazi yake.

“Kabla ya kifo chake alitangaza atakuwa mkazi wa Karagwe atakapostaafu. Kuenzi watu kusiwe kwa gharama kubwa ya kugawa nchi,” alisema.

Alimalizia kwa kusema: “Naamini vigezo vya mkoa wa Chato bado havijatimia. Rais Samia ashughulikie mengine mazito ya kumuenzi hayati Magufuli. Yeye pia ana kazi ya kutengeneza alama yake itakayomtambulisha akimaliza muda wake.

“Ipo haja ya kuiangalia upya sheria inayounda maeneo mapya ya kiutawala na uwekaji wa majina, katika mitaa na majengo ya umma.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

error: Content is protected !!