December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Vigogo Serikali, CCM ‘wamkimbia Nyerere’

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (kulia), Dk. Salim Ahmed Salim – Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (katikati) na Joseph Butiku – Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo wakiwa kwenye mkutano wa kujadili amani nchini

Spread the love

VIONGOZI wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamefanya tukio la ajabu la kukwepa kuhudhuria mkutano wa kujadili amani, umoja na utulivu nchini ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Mkutano huo unafanyika leo na kesho katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Njerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu waandaaji wa mkutano huo, hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo hali tete ya dalili za uwepo wa viashiria vya vurugu na uvunjifu wa amani nchini.

Kiongozi pekee kutoka serikalini upande wa Zanzibar aliyehudhuria mkutano huo ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF).

Kutoka CCM, hakuna kiongozi yeyote aliyehudhuria huku vyama mbalimbali vya upinzani vikishiriki kwa ukamilifu kupitia viongozi wao wakuu.

Baadhi ya waliohudhuria ni Prof. Ibrahim Lipumba (CUF), Dk. Willibrod Slaa (Chadema), James Mbatia (NCCR–Mageuzi) na Anna Mughwira (ACT–Wazalendo).

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Joseph Butiku – Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, alisema “pia tumewaalika viongozi walioko serikalini.”

Aliwataja waalikwa hao kuwa ni Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu–Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na mawaziri.

Waalikwa wengine kwa mujibu wa Butiku ni wenyeviti na makatibu wakuu wa vyama vikubwa vya siasa.

Kufuatia kutooneka kwa viongozi wa serikali na CCM, Lipumba amesema “mara kwa mara amani ya nchi hii inavunjwa na serikali kwa kutoheshimu Katiba, haki za wananchi na utaratibu. Nimesikitika sana katika ufunguzi huu, sijawaona ndugu zangu wa CCM walio ndani ya madaraka na wawakilishi wa serikali.”

Prof. Lipumba amesema watu ambao wako katika mstari wa mbele kuhakikisha amani inaendelea kuwepo ni vyombo vya dola na serikali iliyoko madarakani.

“Kwa sababu huu ni mkutano muhimu ambao unaweza kutupa dira ya kuhakikisha hizi chokochoko ambazo zipo katika nchi yetu namna gani tunaweza kuhakikisha tunajenga mtizamo wa pamoja kuweza kujenga amani ya kweli kwa kutenda haki kwa kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi,”ameongeza Lipumba.

Akifungua mkutano huo, Dk. Salim Ahmed Salim – Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa taasisi hiyo, amesema “lengo kuu la mkutano huu ni kutafakari na kuzungumza wazi wazi kama Watanzania wazalendo viashiria vyote vinavyohatarisha na kutishia kuwepo kwa amani na umoja katika nchi yetu”.

Ametaja malengo mengine kuwa ni kutafuta njia sahihi ya kuhakikisha viashiria hivyo havioti mizizi na kusababisha vurugu nchini.

“Katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano. Watanzania tuache ubaguzi na kubaguana kwa hisia za itikadi, dini, ukabila, mahali mtu anakotoka, kazi anayofanya na uwezo wake kiuchumi,” amesema Dk. Salim.

error: Content is protected !!