TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), nchini Tanzania, inawahoji viongozi wakuu wa Kanisa la Evangelical Assembless of God of Tanzania (EAGT), kutokana na tuhuma mbalimbali zikiwemo za rushwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Miongoni waliokwisha kuhojiwa ni Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Abel Mwakipesile.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne tarehe 16 Februari 2021 na Doreen Kapwani, Ofisa Uhusiano wa Takukuru kwa niaba ya bosi wa taasisi hiyo, Brigedia Jenerali John Mbungo imesema, uchunguzi huo unatokana na malalamiko waliyoyapokea.
Amesema, malalakimo hayo yalitoka wachungaji “kwa ujumla wao ni zaidi ya 540, kwa pamoja wanalalamikia vitendo vya rushwa, ufisadi pamoja na wizi ndani ya kanisa.”
Mambo mengine yaliyolalamikiwa ni; uingizwaji wa vyombo vya moto yakiwemo magari zaidi ya 50 na pikipiki kwa jina la Kanisa la EAGT, “vyombo ambavyo inadaiwa viliingizwa nchini kwa kupitia jina la kanisa na kupata msamaha wa kodi lakini vyombo hivyo vya moto – kanisa halivitambui na wala halijawahi kuvipokea.”
Doreen amesema, lalamiko jingine ni ubadhirifu wa fedha na mali ya kanisa unaodaiwa kufanywa na viongozi wa kanisa hilo kuhusiana na mkataba ulioingiwa kati ya kanisa la EAGT na wapangaji wa Duka la Imalaseko Supermarket Investment, kwani inadaiwa mapato yanayotokana na majengo hayo hayajawekwa wazi hivyo kuashiria kuwepo kwa ubadhirifu.
“Ubadhirifu wa fedha za kanisa kwenye ununuzi wa shule iitwayo Oasis Education and Community Development iliyopo Kahama.”
“Kuwepo kwa TIN tofauti zaidi ya tano zilizosajiliwa kwa jina la Kanisa la EAGT na TIN hizo, kutumika kuingiza magari kwa jina la kanisa na kusamehewa kulipa ushuru wa forodha wakati magari hayo hayajanunuliwa na kanisa,” amesema
Ofisa uhusiano huyo amesema, lalamiko jingine ni “taarifa za mapato na matumizi ya kanisa, kutokuwekwa wazi wala Kanisa halina kitengo cha ukaguzi wa ndani.”
“Uingiaji wa mikataba mibovu na isiyo wazi inayoikosesha Serikali mapato yake halali,” amesema
Kutokana na malalamiko hayo, Takukuru inaendelea na uchunguzi kwa baadhi ya “tuhuma zinaangukia chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.”
Katika kusisitiza hilo, Doreen amesema “tumeshafanya mahojiano na baadhi ya walalamikaji, tumekusanya baadhi ya vielelezo na tunaendela kuwaita na kuwahoji walalamikiwa na leo hii 16 Februari 2021, tumemhoji Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Abel Mwakipesile.”
“Lengo la uchunguzi wetu huu pamoja na mambo mengine ni kutaka kufahamu ukweli wa malalamiko haya ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa,” amesema.
Leave a comment