Tuesday , 5 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Vigogo Chadema watua mzigo wa utetezi
Habari za SiasaTangulizi

Vigogo Chadema watua mzigo wa utetezi

Spread the love

KESI ya uchochezi namba 112/2018, inayowakabili vigogo tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  imekaribia kufika ukingoni. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Kesi hiyo ipo hatua za mwisho kumalizika kutokana na upande wa utetezi kufunga pazia lake la ushahidi, baada ya mashahidi wake kumaliza kutoa ushahidi wao mahakamani hapo, jana tarehe 24, Januari 2020.

 Baada ya mashahidi kumaliza kutoa ushahidi, Peter Kibatala, Wakili wa  utetezi amemueleza Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mkuu, kwamba wamemaliza kuwasilisha ushahidi na mashahidi wao.

Baada ya Wasilisho hilo, Hakimu Simba ameitaja tarehe 24 Februari 2020 kuwa ni siku ya kuanza kuwasilisha hoja za majumuisho kwa upande wa jamhuri, ili  kuishawishi mahakama hiyo kwamba ushahidi waliouwasilisha, unatosha kuwahukumu washtakiwa hao.

Vilevile,  siku hiyo upande wa utetezi utaanza kutetea ushahidi wao waliotoa mahakamani hapo, ili kuishawishi mahakama ione ina kila sababu za kuwachia huru washtakiwa hao.

Mahakama hiyo imejielekeza kupokea majumuisho hayo ya hoja, kutoka kwa mawakili wa pande zote kwa njia ya maandishi, kuanzia siku ya tarehe 24 Februari, 2020.  Na kisha kupanga tarehe ya kutoa hukumu kwa watuhumiwa hao.

Kwenye shauri hilo washtakiwa ni, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa, John Mnyika Katibu Mkuu Chadema-Taifa, Vicent Mashinji aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Chadema-Zanzibar.

Wengine ni, Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, John Heche, Mbunge wa Tarime Vijini, Peter Msigwa , Mbunge wa Iringa Mjini na Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini.

Awali shahidi wa 13, Lumola Kahumbi akiongozwa na Wakili Kibatala amedai kuwa, siku hiyo ya tarehe 16 Februari mwaka 2018, alikua akitokea chuoni DIT posta kwenda kwa Shangazi yake Kinondoni studio.

Na baada ya kushuka kwenye daladala aliyokuwa amepanda, zikikuja gari nyingi za polisi hali iliyopelekea yeye pamoja wa raia wengine kukimbia.

Kahumbi amedai kuwa, akiwa amekaribia eneo wanalouza vitanda, walikamatwa yeye pamoja na wengine na kuingizwa kwenye gari hiyo. Kisha kupelekwa kituoni ambapo waliwekwa nje kwenye mwembe.

Ameeleza kuwa alipokuwa chini ya ulinzi wa polisi, walipewa ngoma na askari na kuamuriwa kuimba, kisha askari mmoja akawaambia kuna ruhusa ya kwenda kukojoa. Akiwa anaelekea chooni, alifuatwa na askari wawili wa kituoni hapo, ambao walimwambia ajiongeze na kisha kumpekua na kuchukua 12,500 na kumwachia shilingi mia mbili, na kumwambia aondoke eneo hilo bila kugeuka nyuma.

Wakati huo huo, akihojiwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amedai kuwa akiwa chini ya ulinzi katika kituo cha polisi Oysterbay,  aliwasikia askari polisi wa kituo hicho wakizungumza kuwa, vijana waliotoka depo wamepiga risasi hovyo hovyo na kuua.

Shahidi wa 14, Ali Othmani amejitambulisha mahakamani hapo kwamba yeye alikuwa wakala wa Chama cha Chadema, kwenye uchaguzi wa marudio wa tarehe 17 Februari 2018, kwenye jimbo la Kinondoni.

Othamani ameieleza mahakama hiyo kuwa, alinyimwa kiapo cha wakala ingawa aliapishwa. Na kupelekea kuzuiwa kuingia kwenye kituo cha kupiga kura, kwa ajili ya kumuwakilisha mgombea wa chama chake.

Shahidi wa mwisho ni, Hassan Kimbau ambaye ameieleza mahakama hiyo kuwa, yeye alikuwa Wakala wa Chadema aliyemukilisha mgombea wa chama hicho kwenye kituo namba C2 cha Kinondoni ‘Biafra.’ ambapo yeye na mawakala wengine walichelewa kupata kiapo cha uwakala.

Kimbau amedai kuwa, yeye alipigiwa simu saa nane usiku na kiongozi wao aliyemtaja kuwa ni Ester Matiko, kwenda kuchukua kiapo chake.

Kimbau amedai  kuwa,  alifika kwenye kituo alichopangiwa kumuwakilisha mgombea wao ambapo alizuiwa kuingia ndani ya kituo. Sambamba na kuchaniwa vipande viwili nakala yake ya kiapo cha uwakala na askari .

Anadai kuwa, askari huyo ambaye hakumbuki jina lake, alishika binduki na kumpiga na kitako cha bunduki.

Wakati huo huo, Wakili Kibatala aliomba mahakama imruhusu shahidi wa tano, ambaye pia ni mshtakiwa wa tano,  Dk Vicent Mashinji kutoa ufafanuzi wake juu ya vidhibiti viwili vilivyotolewa mahakamani hapo, na upande wa Jamhuri kama ushahidi.

Vidhibiti hivyo ni p1 na p2 vilivyowasilishwa na askari PC Fikiri na Koplo Rahimu, waliodai kujeruhiwa kwenye maandamano ya tarehe 16 Februari 2018.

Kibatala amemtaka Dk. Mashinji atoe ufafanuzi wa kitabibu, kuhusu  kutojazwa kwa sehemu ya pili kwenye fomu ya matibabu ya askari hao,  kuna maana gani. Ambapo amejibu kuwa, kujazwa sehemu ya tatu bila sehemu ya pili, kunaathiri sehemu ya pili ya fomu hiyo.

Dk. Mashinji ameieleza mahakama hiyo kuwa,  kwenye fomu hiyo hakuna maelezo ya daktari yanayoeleza anatibu mgonjwa gani au ugonjwa gani.

Maelezo ya Dk Mashinji yalifunga pazia la ushahidi la upande wa utetezi,  ambao umewasilisha mashahidi 15 .

Washtakiwa hao wanadaiwa tarehe 16 Februari 2018, walifanya kusanyiko lililo kinyume cha sheria, lililosababisha kifo cha Mwanafunzi wa chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwelina Akwelin, na kutoa maneno ya uchochezi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Baba yake Ole Sabaya ashinda Uenyekiti CCM – Arusha

Spread the loveLoy Thomas Sabaya ambaye ni Baba wa aliyekuwa Mkuu wa...

Habari za Siasa

Serikali yaagiza uchunguzi chanzo maporomoko Hanang

Spread the loveSERIKALI imeagiza uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha maporomoko ya...

Habari za SiasaTangulizi

Maafa Manyara: Rais Samia akatisha ziara yake Dubai

Spread the loveRAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amekatisha ziara yake...

Habari za SiasaTangulizi

Wataalaam wa miamba watua Hanang

Spread the loveWaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na...

error: Content is protected !!