December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vifo vya ajali ya lori la mafuta vyaishtua serikali, vyama vya siasa

Spread the love

SERIKALI na vyama vya siasa nchini vimetuma salamu za pole kufuatia vifo vya watu 60 na majeruhi 70 vilivyotokea kwenye mlipuko wa lori la mafuta maeneo ya Msavu mkoani Morogoro. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Pia, serikali na vyama hivyo vimetoa wito kwa Watanzania kuacha tabia ya kukimbilia maeneo ya ajali hasa za vyombo vya moto vinavyobeba vifaa vya kuripuka, ikiwemo magari ya mafuta.

Dk. Hassan Abass, Msemaji Mkuu wa Serikali amesema serikali imepokea kwa masikitiko mkubwa mkasa huo, na kutoa wito kwa wananchi kukaa mbali na maeneo yanakotokea ajali hususan zinazohusisha magari yanayobeba vitu vya kuripuka kama mafuta..

“Tumepokea kwa masikitiko taarifa kuhusu ajali ya lori la mafuta, Morogoro iliyosababisha moto kuunguza watu kadhaa. Tunaendelea kutoa wito kwa wananchi kukaa mbali na eneo la ajali hasa yanapohusika magari yanayobeba vitu vya kuripuka,” amesema Dk. Abass.

Nacho Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu Mkuu wake wa Itikadi na Uenezi Taifa, Humphrey Polepole kimetuma salamu za pole kwa familia zilizoguswa na msiba huo mzito.

“Uongozi wa CCM umepokea kwa mshtuko taarifa za ajali ya lori ambayo imegharimu maisha ya Watanzania. Rai yetu kwa Jeshi la Polisi na zimamoto kuendelea kutoa elimu na kusimamia utii wa sheria. tunatoa pole kwa wafiwa na majeruhi kupona haraka,” amesema Polepole.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nao kupitia ukurasa wake wa Twitter kimetoa pole kwa Watanzania kufuatia vifo hivyo.

“Tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za awali za vyombo vya habari kuwa taribani watu 100 wameungua moto wengi wao wamefariki dunia wengine wengi wamejeruhiwa vibaya, chanzo kikidaiwa kuwa mlipuko wa lori lililobeba petroli ,” kimeandika chama hicho katika ukurasa wake wa Twitter.

Ado Shaibu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema chama hicho kinatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na vifo hivyo.

“Chama kimepokea kwa mshtuko mkubwa habari ya vifo vya watu zaidi ya 50 vilivyosababishwa na mlipuko wa gari la mafuta. Tunatoa pole kwa wote waliojeruhiwa na kw afamilia za waliofikwa na umauti,” amesema Ado.

Aidha, Ado ameitaka serikali kuimarisha utendaji kazi wa Jeshi la Zimamoto nchini kutokana na jeshi hilo kuchelewa kufika katika ameneo ya matukio ya ajali za moto, hali inayochangia kupoteza maisha na mali za watu.

“Katika video zilizosambaa mitandaoni imeonekana askari wa Jeshi la Zimamoto wakiwa wamechelewa kufika eneo la tukio, na walipofika wametumia muda mwingi bila kuchukua hatua ya upesi kuwanusuru watu waliokuwa wanateketea kwa moto. Hii ni taswira ya wazi ya udhaifu wa jeshi hilo hasa kuitikia upesi matukio ya ajali yanapotokea na nyenzo za kufanyia kazi,” amesema Ado na kuongeza.

“Tunalitaka Jeshi la Polisi na waziri wa mambo ya ndani ya nchi kuwajibika kutokana na udhaifu na uzembe huu. Serikali pia ihakikishe kuwa makampuni ya mafuta yanakatiwa bima dhidi ya ajali na majanga kama haya.”

Akielezea kwa undani tukio hilo lililotokea asubuhi ya leo tarehe 10 Agosti 2019, Kamanda Wilboard Mutafungwa, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Morogoro amesema moto huo ulizuka majira ya asubuhi baada ya lori la mafuta kupinduka.

“Baada ya kupinduka mafuta yalianza kumwagika, eneo hili kuna watu walikuwa jirani kuna waendesha pikipiki sababu liko karibu na makazi ya watu. Walijitokeza kwa ajili ya kuchota mafuta yaliyokuwa yanamiminika kwa kasi kubwa, ghafla ukajitokeza moto mkubwa,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Dk. Rita Lyamuya, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro amesema wamepokea majeruhi 60 ambao wanaendelea kupatiwa matibabu, pamoja na miili 60 iliyohifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.

“…Tunavyoongea sasa hivi tumeshapokea majeruhi 60, na bado tunaendelea kupokea. Kati ya hao walio ndani ya wodi wanaume ni 58 na wanawake ni wawili. Na pia tumepokea miili 60,” amesema Dk. Lyamuya.

error: Content is protected !!