Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Habari Vifo vilivyoitikisa dunia 2021
HabariTangulizi

Vifo vilivyoitikisa dunia 2021

Spread the love

 

HATIMAYE zimesalia siku tatu 2021 kufika ukingoni usiku wa Ijumaa, tarehe 31 Desemba mwaka huu, huku dunia ikitikiswa na vifo vya watu mashughuli. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam, kwa msaada wa mitandao…(endelea).

MwanaHALISI Online imekuandalia makala ya orodha ya baadhi ya watu mashughuli duniani, waliopoteza maisha 2021.

Rais John Magufuli

Kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Hayati John Magufuli, kilichotokea katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam, tarehe 17 Machi 2021, kiliitikisa dunia kutokana na misimamo pamoja na utendaji wake.

Kifo cha Magufuli kilikuwa gumzo ndani na nje ya Tanzania, kwa kuwa kabla umauti haujamfika, zilienea taarifa mitandaoni zilizodai kuwa amefariki dunia, kutokana na kutoonekana hadharani kwa siku kadhaa.

Taarifa hizo zilikanushwa na viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa sasa ni Rais wa nchi hiyo.

Kifo cha Magufuli kiliteka vichwa vya habari vya kitaifa na kimataifa, kwani ni Rais wa kwanza wa Tanzania, kufariki dunia akiwa madarakani. Aliongoza kwa muhula mmoja na nusu, baada ya kuingia madarakani Novemba 2015 hadi Machi 2021, alipofariki dunia.

Magufuli aliiteka dunia kutokana na misimamo yake, hasa ule wa kwenda tofauti na mataifa mengine katika kuukabili Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19), ikiwemo uamuzi wake wa kutowaweka Watanzania karantini, katika kipindi ambacho dunia nzima ilijifungia.

Kiongozi huyo aliwaongoza Watanzania katika mapambano dhidi ya UVIKO-19, kwa kuwahimiza waondoe hofu bali wazidi kumuomba Mungu, huku akisisitiza matumizi ya dawa za mitishamba na kutoweka mkazo katika matumizi ya chanjo zilizothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Magufuli aliyefahamika ulimwenguni kwa jina la tinga tinga ‘Bulldozer’ kutokana na utendaji kazi wake, mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Chato, mkoani Geita, tarehe 26 Machi 2021.

Viongozi mbalimbali wa kitaifa na wa kimataifa, walimlilia Magufuli, akiwemo Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro. Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson. Mkurugenzi wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus, pamoja na balozi mbalimbali nchini na jumuiya za kimataifa.

Kifo cha mume wa Malkia Elizabeth wa Pili

Tarehe 9 Aprili 2021, Ufalme wa Uingereza ulitikiswa kufuatia kifo cha Prince Phillip, aliyekuwa mume wa Malkia wa Taifa hilo, Elizabeth wa pili. Hata hivyo, chanzo cha kifo chake hakikutajwa.

Prince Phllip aliyefunga ndoa na Malkia Elizabeth 1947, alifariki dunia akiwa katika Kasri la Windsor nchini humo, miezi mwili tangu alazwe kwa ajili ya matibabu kwenye Hospitali ya King Edward VII, jijini London.

Mwili wake ulizikwa tarehe 17 Aprili mwaka huu, katika eneo la Windsor Castle, magharibi mwa Jiji la London, ambapo mazishi hayo yalihudhuriwa na watu 30, asilimia kubwa walikuwa wanafamilia. Idadi hiyo ndogo ya watu walioshiriki mazishi yake, iliwekwa ili kudhibiti maambukizi UVIKO-19.

Viongozi mbalimbali duniani walituma salamu zao za pole kwa familia ya Malkia Elizabeth, akiwemo Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis. Rais wa Marekani, Joe Biden, Rais wa China, Xi Jinping na Waziri Mkuu wa Australia, Scott Morrison. Na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Askofu Desmond Tutu

Tarehe 26 Desemba 2021, Ikiwa zimesalia siku tano kwa mwaka huo kufika tamati, Askofu Mkuu mstaafu nchini Afrika Kusini, Desmond Tutu, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 90, huku chanzo cha kifo hicho kikitajwa ni ugonjwa wa saratani ya tezi dume, alioupata mwishoni mwa 1990.

Kifo cha Askofu Tutu, aliyetwaa tuzo ya amani ya Nobel 1984, kimeacha simanzi Afrika Kusini na dunia nzima, kufuatia mchango wake mkubwa katika kutokomeza ubaguzi wa rangi nchini humo. Mwili wake unatarajiwa kuzikwa Jumamosi, tarehe 1 Januari 2022, Cape Town.


Askofu Tutu aliyezaliwa tyarehe 7 Oktoba 1931, Afrika Kusini, ameacha mjane wake, Leah aliyefunga naye ndoa 1955 na watoto wanne.

Viongozi mbalimbali ulimwenguni, walituma salamu za rambirambi kwa familia ya Askofu Tutu, kufuatia kifo chake, akiwemo Rais Samia, Malkia Elizabeth, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais Mstaafu wa Marekani, Barack Obama, Guterres na Papa Francis.

TB Joshua

Mhubiri wa Kimataifa, Temitope Balogun Joshua maarufu kama TB Joshua, alihitimisha safari yake ya hapa duniani, Jumamosi tarehe 5 Juni 2021, saa chache baada ya kuwahubiria waumini wake kupitia kituo cha Televisheni cha Emmanuel.

Mwanzilishi huyo wa Kanisa la Synagogue Church of All Nations (Scoan), alifariki dunia akiwa na miaka 58, alizaliwa 1963 nchini Nigeria. Mwili wake ulizikwa tarehe 9 Julai mwaka huu, katika viwanja vya kanisa hilo jijini Lagos, Nigeria mwezi mmoja baada ya kufariki dunia.

Ameacha mjane Evelyne na watoto watatu, Sarah, Promise na heart.

Kifo cha Baba wa Nyuklia Pakistan, Abdul Qadeer Khan

Tarehe 10 Oktoba mwaka huu, Taifa la Pakistan lilipotoeza muasisi wake wa kombora la nyuklia, aliyefariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kijeshi, baada ya kupata ugonjwa wa UVIKO-19.

Mhandisi huyo alijipatia heshima nchini Pakistan, baada ya kulifanya taifa hilo kuwa nchi ya kwanza ya Kiislamu duniani kumiliki kombora la nyuklia. 1998 ilifanya majaribio ya kwanza ya kurusha kombora hilo chini ya ardhi.

Mwanasayansi huyo aliifanya Pakistan kuwa nchi ya saba duniani, kati ya nchi zenye nguvu za nyuklia.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Algeria

Kifo cha Rais wa zamani wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika, kilichotokea tarehe 18 Septemba 2021, nacho kilitikisa vichwa vya habari ulimwenguni, kutokana na historia yake ya kuliongoza Taifa hilo kwa miongo miwili mfululizo (1999-2019).

Umaarufu wa Bouteflika ulichochewa na kitendo cha kung’ang’ania madaraka, licha ya kukumbwa na tatizo la kiafya baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi. Aliiongoza Algeria kwa miaka sita mfululizo (2013-2019), bila kuonekana hadharani kutokana na matatizo hayo.

Mwanasiasa huyo alijiuzulu 2019, baada ya jitihada zake za kutaka kugombea kiti cha urais kwa mara tano, licha ya kuwa na afya dhaifu, kugonga mwamba.

Kenneth Kaunda

Kenneth Kaunda, Rais wa Kwanza wa Zambia, alimaliza safari yake ya hapa duniani tarehe 17 Juni mwaka huu, akiwa na umri wa miaka 97 na mwili wake kuzikwa nchini humo, tarehe 2 Julai 2021.
Viongozi mbalimbali wa Afrika, walituma salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha muasisi wa Taifa la Zambia.

1 Comment

 • WHICH NAME ALWAYS PRODUCES NICE WOMEN FOR MARRIAGE AS REPARATION OF FIRST LADY!

  1. LISA
  2. MARGRATE
  3. MARRY
  4. CATHELINE
  5. QUADRIYAH
  6. ELIZABETH
  7. JOSEPHINE
  8. JANET
  9. SASHA
  10. PRISCA
  11. ADELA
  12. JOYCE
  13. NYAMWIZA
  14. MAYA
  15. ADELAH
  16. ZAWAD
  17. GIFT
  18. SALIMA
  19. HALIMA
  20 ESTER
  21. ANNA
  22. ANASTAZIA
  23. SARAH
  24.
  POWER OF WOMAN ON NAMES?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Bunge lalia msongamano wa mizigo bandari Dar es Salaam

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji...

Habari MchanganyikoTangulizi

Haya hapa majina 12 ya familia moja waliofariki kwenye ajali Tanga

Spread the love  MAJINA 12 kati ya 17 ya waliofariki dunia katika...

Habari za SiasaTangulizi

Vigogo wanaokwamisha mradi Liganga na Mchuchuma kitanzani

Spread the love  NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Zungu, watu wanaokwamisha utekelezaji...

Habari MchanganyikoTangulizi

Hii hapa kauli ya Sheikh mpya mkoa wa Dar

Spread the loveSAA chache baada ya kuteuliwa kukaimu nafasi ya aliyekuwa Sheikh...

error: Content is protected !!