Friday , 19 April 2024
Home Kitengo Maisha Afya Vifaa tiba visivyofaa vyakamatwa mitaani
AfyaTangulizi

Vifaa tiba visivyofaa vyakamatwa mitaani

Dk. Faustin Ndungulile
Spread the love

SERIKALI imesema kuwa imefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali ambavyo ni dawa na vifaa tiba ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu, katika vituo vya tiba za asili. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mafanikio hayo yalitokanana Operesheni iliyoandalikwa kutokana na kuwepo kwa taarifa za matumizi ya vifaa tiba aina ya Magnetic Quantum Analyzer na vingine vinavyofanana na hivyo kwenye vituo vya tiba asili na tiba mbadala kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa na matangazo ya vifaa hivyo yanayopotosha umma.

Amesema kuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliandaa na kufanya ukaguzi maalum wa kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 na Sheria ya Dawa Asili na Mbadala ya mwaka 2002 hususan uuzaji, usambazaji, matumizi na matangazo ya vifaa tiba vinavyotumika katika tiba ya kuchua, uchunguzi wa magonjwa na vifaa vingine vinavyodaiwa kuondoa sumu mwilini.

Akitoa taarifa hiyo Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia na Watoto Dk. Faustin Ndungulile amesema kuwa Kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 vifaa tiba kwa ajili ya matumizi nchini, ni lazima viwe vimesajiliwa au kutambuliwa na Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) baada ya kufanyiwa tathmini ya taarifa za kisayansi za kuthibitisha ubora, usalama na ufanisi wake.

Amesema Operesheni hiyo ilifanyika sambamba katika mikoa kumi na moja ambayo ni Dar es salaam (Kinondoni, Ilala, Temeke, Ubungo, Kigamboni), Morogoro (Kilombero), Singida (Manispaa), Arusha (Manispaa), Kilimanjaro (Moshi), Mbeya (Jiji, Mbalizi, Tukuyu), Rukwa (Manispaa), Kigoma (Kasulu, Manyovu), Mwanza (Nyamagana, Ilemela), Kagera (Bukoba) na Mtwara (Manispaa) kwa muda wa siku mbili, kuanzia 6 hadi 7 Machi, 2018.

“Operesheni ililenga kukagua vituo vyote vilivyosajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na vituo vingine kadri ilivyopatikana kwa kuzingatia taarifa za kiintelijinsia zilizofanyika awali,” amesema Dk. Ndungulile.

Amesema jumla ya maeneo 115 yalikaguliwa wakati wa operesheni hiyo ambapo vituo 39 vikiwa vya mkoa wa Dar Es Salaam, 6 Morogoro, 6 Singida, 10 Arusha, 5 Kilimanjaro, 15 Mbeya, 5 Rukwa, 6 Kigoma, 14 Mwanza , 3 Kagera na 6 Mtwara.

Akiendelea kutoa ufafanuzi wa Operesheni hiyo Dk. Ndungulile amesema jumla ya vifaa tiba 395 vyenye thamani ya shilingi 51,116,000/- na dola za kimarekani 2,768 vilikamatwa.

Amevitaja vifaa hivyo vilivyokamatwa kuwa ni Quantum Magnetic Analyser 53, Massagers 40, Detoxifier 18, Cybrow Urinary Stick 1, BP Machine 19, Blood Glucose Meter 2, Ultrasound 1, Acupuncture needles 176, Ion Cleanse 2, Elecromagnetic Bed 20, Homeopathic Electronic Radionic Machine 4, Stetoscope 2 na vifaa vingine 57.

Amesema sambamba na bidhaa hizo kukamatwa operesheni hiyo imebaini kuwepo kwa mapungufu makubwa katika utekelezaji wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba mbadala ya mwaka 2002 pamoja na Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 katika vituo vingi vilivyokaguliwa.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa ukaguzi huo umebaini kuwepo kwa matumizi makubwa ya vifaa vinavyojulikana kama Quantum Magnetic Analyzer katika kupima magonjwa mbalimbali na Detoxifier inayodaiwa kuondoa sumu mwilini.

Aidha, kupitia matangazo yanayotolewa kwenye vituo husika, ukaguzi umebaini upotoshaji mkubwa kwa jamii, kuwa vifaa husika vina uwezo wa kupima au kutibu magonjwa makubwa kama vile saratani, hepatitis, ovarian cysts.

Alisema katika baadhi ya maeneo yaliyokaguliwa, wakaguzi walibaini huduma za upimaji wa HIV, Malaria, Sukari na Pressure zikitolewa huku kukiwa hakuna wataalamu wenye fani husika.

Amesema kutokana na matokeo ya Operesheni hiyo, hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ambapo jumla ya majalada 52 ya kesi tayari yamefunguliwa katika vituo mbalimbali vya polisi dhidi ya watuhumiwa na vituo 50 vimefungwa.

Dk. Ndungulile amevitaja idadi ya vituo, idadi ya kesi na vituo vilivyofungiwa kwa mkoa wa Dar es Salaam idadi ya vituo vilivyofungwa ni 16 na idadi ya madalada ya kesi ni 16.

Amesema mkoa wa Singida vituo vilivyofungwa ni vitatu na majarada ya kesi ni matatu kwa mkoa wa Arusha vituo vilivyofungiwa ni saba na majarada ya kesi saba, mkoa wa Kilimanjaro hakuna kituo kilichofungiwa lakini majarada ya kesi ni vituo mbili.

Vituo vingine alivitaja kuwa ni Mbeya vituo vilivyofungwa ni 11 na vyenye majarada ya kesi ni 11, katika mkoa wa Rukwa vituo vilivyofungiwa ni vinne na vyenye majarada ya kesi ni manne, mkoa wa Kigoma kituo kimoja kimefungiwa huku vituo vitatu vikiwa na majarida ya kesi, katika Mkoa wa Mwanza vituo vitatu vimefungiwa na hakuna kituo chenye jarida la kesi, mkoa wa Kagera vituo vilivyofungiwa ni viwili na vyenye majarida ya kesi ni mawili na Mkoa wa Mtwara vituo vilivyofungiwa ni vitatu na vituo vyenye majarida ya kesi ni manne na kufanya jumla ya vituo vyote vilivyofungiwa ni 50 na vyenye majarada ya kesi kuwa 52.

Aidha amesema baada ya uchunguzi wa makosa kukamilika hatua mbalimbali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani watuhumiwa na kutoa adhabu kulingana na Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 na Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya mwaka 2002.

Amesema adhabu hizo zinajumuisha kufuta leseni ya biashara, kuwafutia usajili wataalamu, kuondoa kwenye soko na kuharibu vifaa husika.

“Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa taasisi zilizoshiriki kwenye operesheni hii ikiwemo Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Chakula na Dawa, kwa kutambua umuhimu wa zoezi hili kwa maslahi ya Taifa.

“Aidha, napenda kuchukua nafasi hii kupiga marufuku uingizaji, usambazaji na matumizi ya vifaa vinavyodaiwa kupima magonjwa mbalimbali kama Quantum Magnetic Analyzer, Detoxifier n.k kutokana na ukweli kuwa usalama na ufanisi wa vifaa hivyo haujathibishwa. Waingizaji wanaagizwa kuwasilisha TFDA taarifa za kisayansi za kuthibitisha ubora, usalama na ufanisi kupitia mfumo wa usajili ili ziweze kutathminiwa,” amesema Dk. Ndungulile.

Katika taarifa hiyo Dk. Ndungulile alitoa wito kwa umma na wananchi kwa ujumla kuwa makini na taarifa za upotoshaji zinazotolewa hususan matumizi ya vifaa hivyo ambavyo havijathibitishwa na TFDA ili kulinda usalama wa afya zao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

error: Content is protected !!