April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Video ya Zitto yaoneshwa kortini

Spread the love

MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imekubali kupokea na kuoneshwa kwa video ya Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Video hiyo ni ile inayomuonesha, Zitto akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari. Video hiyo iliwasilishwa mahakamani hapo na shahidi wa 14, Sajent James.

Kielelzo hicho kimepokelewa na mahakama hiyo, na hivyo kitatumika kama sehemu ya ushahidi katika kesi ya uchochezi inayomkabili kiongozi huo.

Uamuzi wa kupokea kielelezo hicho, umetolewa leo tarehe 4 Desemba 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi badala ya kupitia hoja za pande zote.

Jana tarehe 3 Decemba 2019, upande wa utetezi katika kesi hiyo ya uchochezi walipinga kupokewa kwa kielelezo hicho kwa madai, kuwa  shahidi anayetaka kutoa kielelezo hicho hajaeleza ni namna gani video hiyo ilirekodiwa.

Wakili wa utetezi, Jebra Kambole alidai nyaraka inayotakiwa kutolewa na shahidi wa 14 wa upande wa mashtaka, mwenye namba E 3234 Sajent James (52), ni ya kielektroniki hivyo inatakiwa kufuata maelekezo ya sheria inayohusu utoaji wa kielelezo cha kielektroniki.

Jebra alidai, rekodi (CD) ambayo inatakiwa kupokelewa mahakamani, haijarekodiwa na shahidi huyo hivyo ameshindwa kukithi matakwa ya kifungu 18 (2) (a) cha sheria hiyo ya kielektroniki.

Pia alidai shahidi huyo ameshindwa kuonesha machine iliyotumika kurekodi na kama ilikuwa inafanya kazi vizuri na kuomba mahakamani isipokee kielelezo hicho.

Akipinga hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga alikiri kuwa, kielelezo ambacho shahidi wao anataka kipokelewe na kitumike kama ushahidi mahakamani ni cha kielektroniki.

Katuga alidai, kitu ambacho shahidi alikuja kukielezea mahakamani hapo ni kuhusu uchunguzi walioufanya katika video kama ni halisi au la.

Alidai, hakuna kifungu ambacho upande wa utetezi wamekielezea kwamba, aliyerekodi video ndio anayepaswa kutoa kielelezo hicho.

Akitoa uamuzi huo, baada ya kupitia hoja za pande zote, hakimu Shaidi alisema, kwa kuwa Sajent James ndio alihusika kuifanyia uchunguzi CD hiyo, anao uwezo wa kuitoa mahakamani  hapo kama kielelzo.

“Kwa kuwa shaidi alipewa CD hiyo kuifanyia uchunguzi, anao uwezo wa kuitoa mahakamani hapa itumike kama ushahidi, hivyo kutokana na sababu hizo, mahakama hii inapoke kilelelzo hiki ili kitumike kama sehemu ya ushahidi katika kesi hii” alisema Hakimu Shaidi.

Awali, Sajent James ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa Kisayansi kutoka Makao Makuu ya Polisi, Sajent James (52), alidai alipata barua iliyoambatanishwa na CD kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ikielekeza kufanya uchunguzi wa picha iliyomo kwenye kielelezo hicho.

Alidai, barua hiyo ilipewa namba OB/IR/8291/2018 ya Oktoba 10, 2018 ililetwa na Koplo Faraji na baada ya kuipokea,  mkuu wake wa kazi, SP Tumaini alimpa jukumu la kufanya uchunguzi.

Wakati huo huo, mahakama hiyo imeonesha CD ya video iliyorekodiwa wakati wa mkutano wa waandishi wa habari na Zitto.

Katika video hiyo,  Zitto akizungumza na waandishi wa habari, na mada kuu zilikuwa mbili ambazo ni hali ya usalama nchini na hali ya zao la korosho.

Vile vile alizungumzia tuzo aliyopata mwanaharakati Rebecca Gyum.

“Tumefuatilia mauaji ya huko kijiji cha Mpeta, Nguruka. Tunajua wananchi pamoja askari polisi wameuawa na wananchi waliokuwa na silaha za jadi, lakini keshi la polisi bado halijatoa tamko lolote. Tunataka ieleze watu wangapi wameuawa katika mapigano hayo, baina ya wananchi wanaodiawa kuvamia Ranchi ya Taifa (Narco),” alisikika akisema Zitto katika video hiyo.

Katika video hiyo, Zitto alisikika akisema kuwa, tangu Tundu Lissu apigwe risasi, tangu Azory Gwanda apotee na tangu Ben Saa nane apotee, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na Jeshi la polisi.

Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi. Anadaiwa kutenda makosa hayo tarehe 28 Oktoba 2018, akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo.

Baada ya hakimu kusikiliza na kutazama video hiyo, kesi hiyo imeahirishwa mpaka tarehe 3 Januari 2020.

error: Content is protected !!