April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya vigogo wa Chadema, yamuibua Waitara mahakamani

Spread the love

WAKILI wa upande wa utetezi katika kesi ya jinai inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na baadhi ya viongozi wenzake, Peter Kibatara, amehoji sababu ya kutokuwapo mahakamani kwa Mwita Mwaikabe Waitara, mbunge wa Ukonga (CCM). Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Hatua ya Kibatara kuhoji sababu za kutokuwapo kwa Waitara kwenye orodha ya washitakiwa, ilitokana na kutajwa kwake na upande wa Jamhuri, kwamba alikuwa mmoja wa watu waliohudhuria mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni na kuhutubia mkutano huo.

Waitara ambaye alikuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Ukonga, jijini Dar es Salaam, kwa sasa ni naibu waziri, ofisi ya rais (TAMISEMI). Aliondoka Chadema na kujiunga na CCM, tarehe 28 Julai 2018.

Uchaguzi mdogo katika jimbo la Kinondoni, ulifanyika Jumapili ya tarehe 7 Februri mwaka 2018.

Mbowe na wenzake –Vicent  Mashinji, katibu mkuu wa Chadema; John Mnyika, naibu katibu mkuu (Bara); Salum Mwalimu, naibu katibu mkuu (Zanzibar), Ester Matiko, mbunge wa Tarime Mjini; Halima Mdee, mbunge wa Kawe; Ester Bulaya, mbunge wa Bunda Mjini; John Heche, mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa, mbunge wa Iringa Mjini – wanatuhumiwa kwa makosa matatu.

Miongoni mwa makosa hayo, ni kula njama, kusababisha vurugu zilizomsababishia kifo mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo cha taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwiline Akwilina; kuhamasisha hisia za chuki na kushawishi wananchi wa Kinondoni, kutumia silaha.

Mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa mahakama ya Kisutu, Thomas Simba, wakili Kibatara alisema, ameshangazwa na upande wa mashitaka kutomjumuisha Waitara kwenye kwenye kesi hiyo, wakati naye kupitia mkanda wa video uliowasilishwa mahakamani, anaonekana kuhutubia.

Ushiriki wa Waitara katika kesi hiyo Na. 112/2018, umetajwa na shahidi wa sita wa upande wa mashitaka, Koplo Charles, kutoka kituo cha polisi cha Ostabay.

Afisa huyo wa jeshi la polisi, alieleza mahakama kuwa Waitara alikuwa mmoja wa watu waliohutubia mkutano huo ambao baadaye ulisababishia kifo cha Akwiline.

Binti huyo wa miaka 22 alikutwa na mauti baada ya kushambuliwa kwa risasi kichwani na maofisa wa jeshi la polisi. Shambulizi dhidi ya Akwiline, lilifanyika tarehe 7 Februari 2018, eneo la Mkwajuni, wilayani Kinodoni, mkoani Dar es Salaam.

Akihojiwa na wakili Kibatara, Koplo Charles alikiri kuwa Waitara alihutubia mkutano na alikuwa mmoja wa viongozi wa Chadema, waliomnadi mgombea wa CCM.

Shahidi huyo alikuwa akitoa ushahidi wake, kufutia mahakama kuridhia ushahidi wa video iliyorekodiwa na askari huyo, kuonyeshwa mbele ya mahakama.

Kwenye video hiyo inayolenga kuishawishi mahakama kuwatia hatiani washitakiwa hao, Mbowe anaonekana akielekeza wananchi waliohudhuria mkutano huo wa kampeni, ambapo mgombea wa Chadema alikuwa Salum Mwalimu, kuchochea uhasama kwenye jamii.

Ushahidi wa shahidi huyo ulioneshwa mahakamani hapo kwa kutumia Projector.

Katika mahojiano hayo makali mbele ya Hakimu Simba, leo tarehe 19 Agosti 2019, Wakili Kibatala alimuhoji Koplo Charles kama anakumbuka maneno aliyosema Waitara katika mkutano huo.

Mahojiano kati ya Kibatara na Koplo Charlesyalikuwa kama ifuatavyo:

Kibatala: Unakumbuka vizuri kilichosemwa na washtakiwa katika kielelezo namba tano? Nieleze Mwita alisema nini?

Shahidi: Maneno aliyosema Mwita Waitara siyakumbuki.

Kibatala: Hivi, Mwita Waitara sasa hivi ni nani?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Hufahamu kama Mwita Waitara, ni naibu waziri TAMISEMI?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Mwita Waitara unamuona hapa katika orodha ya washitakiwa?

Shahidi: Hayupo.

Licha ya jina la Waitara kuibuka katika mahojiano hayo, majina ya Ben Saanane, aliyekuwa msaidizi wa Freeman Mbowe, Mwanahabari Azory Gwanda, Mdude Nyagali, ambaye ni mwanachama wa Chadema pamoja na Tundu Lissu, aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), nayo yalitajwa ndani mahakama hiyo.

Kibatala: Shahidi unamfahamu Ben Saanane?

Shahidi: Simfahamu.

Kibatala: Unamfahamu Mdude Nyagali?

Shahidi: Simfahamu.

Kibatala: Unamfahamu Tundu Lissu?

Shahidi: Namfahamu.

Kibatala: Unafahamu Tundu Lissu ni mbunge?

Shahidi: Sio mbunge.

Kibatala: Unafahamu alikuwa mbunge?

Shahidi: Nafahamu alikuwa mbunge.

Kibatala: Unafahamu alishambuliwa kwa risasi karibu na eneo wanalokaa viongozi wa serikali pale Dodoma?

Shahidi: Ninafahamu alishambuliwa kwa risasi, sifahamu alishambuliwa wapi.

Kibatala: Jeshi la Polisi lilimkamata nani aliyehusika katika tukio la kumpiga risasi?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Kutokamatwa watu waliohusika kumpiga risasi Tundu Lissu kunalijengea heshima jeshi la Polisi?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Unamfahamu Simon Kanguye, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Kibondo, mkoani Kigoma?

Shahidi: Simfahamu.

Baada ya mahojiano hayo, wakili Kibatala aliendelea kumuuliza maswali shahidi huyo, ambapo alimtaka kueleza maeneo yafuatayo.

Kibatala: Unafahamu mpaka jioni ya tarehe 16 Februari 2018, msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni, hakutoa barua ya utambulisho kwa mawakala wa Chadema?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Hizi barua msimamizi anatakiwa kutoa kwa ajili ya wasimamizi wa uchaguzi, ni haki kisheria au hisani?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Unafahamu hizi barua zinatolewaje?

Shahidi: Sifahamu.

Baada ya mahojiano hayo, Kibatala alimuomba Hakimu Mkazi Simba anayesikiliza shauri hilo kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda, hadi kesho Jumanne. Hakimu Simba alikubaliana na ombi hilo.

Awali Koplo Carles alionesha video aliyoipa jina la “Mkutano wa Chadema wa mwaka 2018” ambako kumekutwa baadhi ya  viongozi na wabunge wa Chadema, wakihutubia mkutano wa kumnadi Mwalimu.

Video ya kwanza yenye dakika 56 na sekunde 37, ilionesha wabunge kadhaa wa Chadema, wakitoa hotuba za kumnadi Mwalimu na kuituhumu serikali kuvuruga misingi ya kidemokrasia.

Aidha, video inamuonyesha mshitakiwa wa kwanza – Freeman Mbowe – akihutubia wananchi waliohudhuria katika mkutano uliofanyika uwanja wa Buibui, Kinondoni.

Video inamuonyesha Mbowe akitaka wananchi kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Kinondoni, ili kumshinikiza kutoa hati za viapo kwa mawakala wa chama hicho. Video zote mbili, zina muda wa takribani saa moja.

Kabla ya Mahakama kuamuru video hiyo kutolewa kama kielelezo, Hakimu Simba ilibidi aombe dakika 30 kupitia sheria mbalimbali, kufuatia upande wa utetezi kuwasilisha pingamizi juu ya jambo hilo.

error: Content is protected !!