April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Video ya Mbowe, wenzake sasa kuoneshwa kortini

Freeman Mbowe, Kiongozi wa Chadema (wa pili kulia) na wenzake wakiwa mahakamani Kisutu

Spread the love
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imeridhia kuoneshwa video inayodaiwa kubeba matukio yanayomuhusisha Freeman Mbowe na wenzake wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Kinondoni mwaka 2018. Anaripoti Faki Sosi…(endelea).

Kwenye kesi hiyo ya uchochezi, awali mahakama ilikubali kupokea video (tepu) hiyo, iliyowasilishwa na upande wa Jamhuri kama moja ya vielelezo muhimu kwenye kesi hiyo namba 112 ya mwaka 2018, hata hivyo upande wa utete ulipinga.

Uamuzi wa kuonesha video hiyo umetolewa leo tarehe 19 Agosti 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kupitia hoja za upande wa mashitaka na utetezi.

Video hiyo inadaiwa kubeba matukio yanayomuonesha Mbowe na wenzake tisa wakiwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi huo, na kwamba ina uhusiano na kesi hiyo.

Awali, upande wa mashitaka uliiomba mahakama hiyo kukubali kuonesha video hiyo, huku upande wa utetezi ukipinga ombi la kuoneshwa mahakamani hapo kwa kutumia vifaa vya nje.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba ameeleza kwamba uamuzi huo unatokana na hoja pingamizi za upande wa utetezi zilitolewa na Wakili Peter Kibatala na Profesa Abdallah Safari na zile za upande wa Jamhuri zilizojibiwa na Wakili Paul Kadushi na Dk. Zainab Mango.

Hakimu Simba amesema, kamera hiyo na mkanda wa video (Tape) zimeishapokelewa kama vielelezo mahakamani hapo kutoka kwa shahidi namba sita, Koplo Charles aliyedai kwamba kamera hiyo ili ichezeshe picha ni lazima iingizwe vifaa vya nje.

“Pingamizi za picha za tukio zisioneshwe mahakamani kwa kutumia vifaa vya nje, halina mashiko yoyote,” amesema Hakimu Simba.

“Kwa sababu hizo mahakama inaamuru hizo picha zioneshwe mahakamani. Na Mahakama ya Kisutu ina vifaa vya kuonesha video hizo. “

Hakimu Simba ameaharisha shauri hilo kwa dakika ambapo amesema, mahakama ikirejea itakwenda kuoneshwa video hiyo.

Kwenye kesi hiyo, viongozi tisa wa Chadema wanashitakiwa kwa madai ya uchochezi wa uasi na kufanya  maandamano bila kuwa na kibali, na kusababisha mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwelin.

Watuhumiwa kwenye kesi hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema – Taifa, Freeman Mbowe; Vicent Mashinji, Katibu Mkuu; John Mnyika, Naibu Katibu Chadema –Bara; Salum Mwalimu, Naibu katibu Mkuu Zanzibar.

Pia wamo Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

error: Content is protected !!