Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Video ya mahojiano Mke wa Bilionea Msuya, Polisi zakataliwa
Habari MchanganyikoTangulizi

Video ya mahojiano Mke wa Bilionea Msuya, Polisi zakataliwa

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekataa kupokea kielelezo cha Tape iliyofikishwa mahakamani hapo na shahidi wa sita wa Jamhuri, Inspekta Alistides Kasigwa kwenye kesi inayomkabili Mke wa Bilionea Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Kilelezo hicho kilipingwa kupokelewa mahakamani hapo na upande wa utetezi ambacho kimeelezwa mahakamani hapo kina ushahidi wa video uliodaiwa kurekodiwa na shahidi huyo wakati wa mahojiano ya mtuhumiwa huyo na Polisi.

Leo Jumatano tarehe 9 Machi 2022, Jaji Edwin Kakolaki akitoa uamuzi huo anakubaliana na hoja moja kati ya tano za pingamizi zilizotolewa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kuwa kielelezo hicho kilichokuwa kinaombwa kupokelewa mahakamani hapo hakikuwahi kuorodheshwa wala kusomwa katika hati ya uhamishaji wa kesi hiyo kutoka mahakama ya chini kwenda Mahakama Kuu kama sheria inavyoelekeza.

Jaji Kakolaki amesema, upande wa mashitaka umekiuka kifungu cha 246 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kwa kushindwa kuorodhesha kielelezo katika nyaraka ambazo zilitakiwa kwenda kutolewa mahakamani.

Amesema hoja ya upande wa mashitaka ilisema walizingatia kifungu hicho kwani mahakama na washitakiwa walifahamishwa kuhusu kielelezo kinachoombwa kutolewa ni sehemu ya kielelezo halisi, pia kilitajwa wakati wa usikilizwaji wa awali na imeongelewa kwenye maelezo ya shahidi namba sita ambaye alieleza namna alivyopata kielelezo hicho.

“Ni takwa la kisheria kifungu cha 246 kifungu kidogo cha pili cha CPA, nyaraka yoyote ya ushahidi inayotakiwa kutumika mahakamani kwa upande wa mashitaka ni lazima iorodheshwe na kisomwe kwa washitakiwa katika hatua ya Commital na kutofanya hivyo kinaweza kufanya kielelezo hicho kisipokelewe mahakamani,’’ amesema Jaji Kakolaki.

Amesema kifungu hicho kinamaanisha pale mshitakiwa atakapofikishwa katika mahakama ya chini, atasomewa mashitaka yaliyopelekwa mahakama Kuu na kufafanuliwa mashitaka hayo kwa sababu maelezo yake yanatakiwa kusomwa na kuelezwa kwa kuwa yana ushahidi ndani yake yanayokusudiwa kutumiwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kama kielelezo.

Amesema mahakama hiyo ilijiuliza kama kielelezo hicho ni sahihi kwa mujibu wa kifungu namba 3(1) cha sheria ya ushahidi ambayo inaeleza nyaraka inayokuwa ndani ya kompyuta na kitu ambacho kinaweza kutunzwa kwa ajili ya matumizi ya baadae, kusomwa au kuangaliwa kinaweza kuwa nyaraka na kama inabishaniwa kitapaswa kuwa na kigezo.

Jaji Kakolaki amesema mahakama hiyo inaona kielelezo hicho ambacho ni min-video tape ni nyaraka kama zilivyo nyaraka nyingine na ilipaswa kusomwa na kuorodheshwa kwa mahakama za chini kama sheria inavyoelekeza.

Amesema kuhusu kusoma maelezo ya shahidi kutajwa kwa kielelezo hicho pekee hakujitoshelezi kwa sababu kielelezo hicho kilipaswa kuorodheshwa na kusomwa mahakamani.

“Hitaji la kuorodheshwa na kusomwa kwa kielelezo ni lazima kwa sababu linatoa uhakika kwa mshitakiwa na kumpa haki ya usawa na si kupokea ushahidi wa kushtukizwa. Mshitakiwa anapaswa kujua undani wa ushahidi uliotolewa juu yake ili kumsaidia kujua kwenye uandaaji wa ushahidi wa wake wakati wa kujitetea,’’ amesema Jaji Kakolaki.

Amesema mahakama haikubaliani na hoja za upande wa mashitaka kuwa waliorodhesha mintap video kama nyaraka hivyo, hakiwezi kuchukuliwa kuwa kielelezo halisi na hakiwezi kuwa ushahidi wa kielektroniki halali.

Kwenye shauri hilo, Mrita na Muyella wanatuhumiwa tarehe 25 Mei 2016 kumuua dada wa marehemu Msuya, Aneth Msuya nyumbani kwake Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Jana tarehe 8 Machi 2022, Shahidi wa serikali Inspekta Kasigwa ambaye ni mchunguzi wa picha mbalimbali zinazohusu matukio ya kihalifu na zile zisizokuwa na kihalifu aliwasilisha kielelezo hicho.

Kasigwa akiongozwa na wakili Mwandamizi wa wa serikali Genes Tesha huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Peter Kibala aliyesaidiwa na Nehemia Nkoko.

Tesha alimuongoza shahidi huyo kuanza kutoa ushahidi wake kwenye mahakama hiyo na kwamba ushahidi wake ulibebwa na vielelezo viwili kimoja bahasha na cha pili ni tape aliyodai ndiyo iliyotumika kurekodi mahojiano yake na Ofisa wa Polisi kutoka kwenye Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaa SP Latifa Mohamed (42).

Inspekta Kasigwa alidai mahakamani hapo kuwa tarehe 8 Agosti 2016 alipewa jukumu la kurekodi video ya mahojiano hayo na kwamnba alitumia kamera yake aliyoitaja aina ya Sony, betri, tape za min-div, chaja ya kamera na standi yake.

Akieleza mahakamani hapo aliamuriwa kwenda kituo cha Polisi cha uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam, ambapo aliwakuta askari David Mhang’aya Jumanne Malaghahe na baadaye aliingia kwenye chumba cha mahojiano alimkuta mtuhumiwa wa kike pamoja na SP Latifa ndipo wakaanza mahojiano hayo huku yeye alikuwa akirekodi kupitia kamera yake na kwamba alidai kuwa alitumia dakika 40 kurekodi mahojiano hayo.

Alipoulizwa kwa huyu mtuhumiwa akimuona atamjua akadai kuwa atamfahamu na kwamba hapo mahakamani yupo ndipo akaamriwa na wakili Tesha akamuoneshe ndipo alipokwenda upande wa washtakiwa na kuonesha kwa kunyoosha mkono wake wa kushoto upande alioketi Mrita.

Inspekta Kasigwa alidai katika mahojiano hayo mtuhumiwa huyo alieleza angeweza kwenda nao Kibada-Kigamboni kuwaonesha eneo la tukio na kwamba walikwenda mpaka Kigamboni ambapo huko alirekodi mahojiano hayo yaliyotumia takribani dakika 10 mpaka 15.

Baada ya kumaliza mahojiano hayo Kasigwa alirejea Ofisini kwake na kuandaa Nakala mbili kwenye DVD, na tape moja akadai kuwa alizifunga k vizuri kishwa kuweka saini yake juu ya bahasha.

Inspekta Kasigwa aliiomnba mahakama hiyo kupokea bahasha hiyo kama kielelezo Jaji Kakolaki alipokea bahasha baadaye Wakili Tesha aliomba mahakama hiyo imrejeshee tena bahasha hiyo ambapo alirejeshewa na kumtaka Shahidi huyo aifungue na aeleze kilichopo ndani ya bahasha hiyo.

Shahidi huyo alifungua bahasha hiyo na kutoa tape ambayo alidai kuwa ndiyo aliyoitumia kurekodi mahojiano ya Mtuhumiwa na SP Latifa.

Wakili Tesha akamuhoji kwamba anataka mahakama iifanye nini Tape hiyo akajibu kuwa ipokelewe kama kilelezo.

Kibatala alisimama na kuomba mahakama hiyo isiipokee tape hiyo kama kielelezo kwa kuwa utaratibu uliotumika umekinzana na sheria ya ushihidi ambapo amedai ushahidi wa tape ni ushahidi ni wa kieletroniki ambao haujajitosheleza kwenye uwasiliwashwaji wake.

“Tulitegemea wakati shahidi anaongozwa angetueleza kuwa wakati anakwenda kurekodi kamare yake aliichaji au ilikuwa na chaji na hakueleza kama wakati anarekodi kamera hiyo ilikuwa ikifanya kazi vizuri au la.”

Katika hoja nyengine Kibatala amedai sheria ya ushahidi wa kieletroni kwenye kurekodi mpiga picha anatakiwa asiwe kwenye upande wenye maslahi na kesi hiyo ambapo ameeleza shahidi huyu yupo chini ya Mwendesha mashtaka wa Serikali DPP.

Hoja nyengine Kibatala amesema kuwa kuwasilisha ushahidi wa kieletroki unapaswa kuwasilishwa kwa kiapo juu ya ushahidi huo na kwamba upande wa Jamhuri ulipaswa kueleza kwenye maelezo ya mwenendo wa mashtaka (Commito).

Baada ya wasilisho hilo Wakili Tesha alijibu hoja hizo pingamizi kwa kudai kuwa shahidi huyo hakufanya kazi chini ya DPP alitekeleza majukumu yake chini ya Mkurugenzi wa Upelelezi pia amedai kuwa hitajio la kiapo linaulazima kwenye kesi za jinai na sio kwenye kesi za jinai.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NMB yafadhili ziara ya mafunzo machinga, bodaboda Dar nchini Rwanda

Spread the loveBENKI ya NMB imefadhili ziara ya siku nne ya mafunzo...

ElimuHabari Mchanganyiko

Waliopata Division one St Anne Marie Academy waula, Waahidiwa kupelekwa Ngorongoro, Mikumi

Spread the love WANAFUNZI wa shule ya St Anne Marie Academy waliofanya...

Habari Mchanganyiko

Wadau wataka kasi iongezeke marekebisho sheria za habari

Spread the love  WADAU wa tasnia ya habari wametakiwa kuongeza juhudi katika...

Habari Mchanganyiko

TEF yawatuliza wadau wa habari marekebisho vifungu kandamizi

Spread the love  JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limewataka wadau wa habari...

error: Content is protected !!