Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfley Kasekenya amesema Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), itaanza ujenzi hivi karibuni kwa sababu usanifu wa vibanda 950 vya wajasiriamali, katika barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya, ulishafanyika. Anaripoti Jemimah Samwel, Dar es Salaam…(endelea).
Hatua hiyo imekuja baada ya TANROADS kukamilisha usanifu wa vibanda 950 vya wajasiriamali, vitakavyojengwa pembezoni mwa barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya.
Naibu Waziri hyo amesema zabuni za ujenzi huo zipo katika hatua ya uchambuzi na ujenzi kwa awamu ya kwanza unatarajiwa kuanza Desemba, 2023 na utekelezaji umekadiriwa kuchukua muda wa miezi sita.
Kasekenya ametoa kauli hiyo leo Jumanne bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu (CCM), aliyehoji lini Serikali itaanza ujenzi wa vibanda vya wajasiriamali pembezoni mwa barabara ya Kimara hadi Kiluvya, ili kupunguza msongamano wa wafanyabiashara na watu barabarani.
Mbunge huyo alifafanua kuwa kumekuwa na msongamano wa magari pamoja na watu barabarani, kwa sabababu hakuna vibanda maalumu vya kupata huduma kitendo kinachosababisha msongamano.
“Serikali inapaswa kujenga vibanda hivyo, hiyo itasaidia kupunguza msongamano huo na pia itafanya wafanyabiashara wa eneo hilo kuwa wengi na kuongeza pato kwa taifa,”amesema Mtemvu.
Leave a comment