December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uzito uliozidi, kiribatumbo chanzo cha magonjwa sugu

Spread the love

 

TAASISI ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), imesema uzito uliozidi na kiribatumbo ni chanzo kikuu cha magonjwa sugu na yasioyakuambukiza. Anaripoti Selemani Msuya, Tabora … (endelea).

Hayo yamesemwa leo Jumatatu, tarehe 18 Oktoba 2021 na Mkurugenzi Mtendaji wa TFNC, Dk. Germana Leyna wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kilele cha maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa yatakayofanyika katika viwanja vya Sabasaba mkoani Tabora 23 Oktoba 2021.

Dk. Leyna amesema kuongezeka uzito uliozidi na kiribatumbo kunasababishwa na ulaji duni pamoja na mitindo ya mibaya ya maisha kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, figo na baadhi ya saratani.

Amesema mikoa ambayo imeathirika na uzito uliozidi na kiribatumbo ni Kilimanjaro, Arusha, Mbeya na mingine hivyo ameashauri wananchi kufuata mfumo bora wa lishe.

Aidha, Leyna amesema uzito uliokithiri kwa wanawake walio katika umri wa uzazi limeongezeka kutoka asilimia 29.7 mwaka 2014 hadi asilimia 31.7 mwaka 2018.

Amesema kwa upande mwingine tatizo la upungufu wa damu miongoni mwa wanawake walio katika umri wa uzazi miaka 15 hadi 49 limepungua kutoka asilimia 44.8 hadi asilimia 28.8.

“Vilevile kiwango cha ukondefu kimepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2014 hadi asilimia 3.5 mwaka 2018. Pamoja na kupungua kwa kiwango hicho bado kuna takribani watoto 600,000 wa na utapiamlo mkali na wa kadiri, huku tatizo la uzito pungufu likiongezeka kutoka asilimia 13.4 mwaka 2014 hadi asilimia 14.6 mwaka 2018,” amesema

Mkurugenzi huyo amesema kwa ujumla kiwango cha utapiamlo kimepungua kutoka asilimia 34.7 mwaka 2014 hadi asilimia 31.8 mwaka 2018.

Amesema licha ya kupungua huko Shirika la Afya Duniani (WHO 1995), lilisema kuwa kiwango hicho bado kinaashiria hali mbaya ya lishe na inakadiriwa kuna watoto zaidi ya milioni 3 wamedumaa.

“Idadi kubwa ya watoto waliodumaa wapo katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Mara, Dodoma, Geita, Tanga, Ruvuma, Mbeya, Morogoro na Tabora,” amesema.

Dk. Leyna alisema ili kukabiliana na matatizo hayo Serikali imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuboresha hali ya lishe ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Pia, amesema Serikali kwa kushirikiana na TFNC wanaongeza madini joto kwenye chumvi, kutoa virutubishi vya nyongeza kwa makundi maalum hususani wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

“Tunahimiza huduma za ulishaji sahihi kwa watoto wadogo na wachanga, kutoa chakula dawa kwa ajili ya kutibu watoto wenye utapiamlo mkali na wa kadiri na kuanzisha siku maalum ya kuadhimisha mafanikio jitihada zinazoendelea.

Halikadhalika tunatoa elimu kuhusu faida za lishe bora na athari za utapiamlo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia siku ya lishe,” amesema.

Dk. Leyna amesema katika kilele cha maadhimisho ya siku ya lishe ambacho kimeanza jana hadi Ojtoba 23 mwaka huu, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dorothy Gwajima.

error: Content is protected !!