Spread the love

MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, ametangaza kufungwa kwa baadhi ya barabara za katikati ya mji huo ili kutoa nafasi kwa wananchi kwenda kushuhudia uzinduzi wa filamu ya Tanzania: The Royal Tour. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Tukio hilo linatarajiwa kufanyika kesho Tarehe 28 Aprili, 2022 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha ambapo mgeni rasmi ni Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Jumatano tarehe 27 Aprili, 2022, Mongela ametaja barabara zitakazofungwa kuwa ni Barabara ya Afrika Mashariki kutokea mataa ya Sanawari hadi mzunguko wa Ngorongoro kwenda barabara ya Goliondoi.

“Barabara hizi zitakuwa zimefungwa kwaajili ya kuruhusu wananchi kuelekea eneo la tukio na kumpokea Mheshimiwa Rais,” amesema Mongela.

Mkuu huyo wa mkoa ametaja pia kufungwa kwa barabara ya kutoka mnara wa Azimio kupitia central polisi mpaka mzunguko wa Ngorongoro na kwenda Ofisi za jiji hadi mnara wa saa.

“Tunafanya hivi ili kuruhusu kuingia na kutoka eneo la tukio kwa urahisi zaidi bila kuwa na hali hatarishi zaidi za ajali au kubanana.

Mongela amewaalika wananchi wa Arusha kwenda kushuhudia uzinduzi huo lakini pia kujitokeza kwenda kumpokea Rais Samia katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro atakayewasili kesho saa 12 asubuhi akitokea nchini Marekani.

“Wananchi wote wanaalikwa kwasababu eneo la nje ni kubwa sana linaweza kuchukua watu 6000 hadi 7000 na limepangwa skrini nyingi ili kila mtu aone tukio sawasawa na yeyote yule.”

Amesema pia vyombo vyote vya habari nchini vitarusha tukio hilo mubashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *