UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi UWT Kata ya Kivukoni jijini Dar es Salaam umeadhimisha Siku ya Wanawake duniani kwa kuendesha kampeni ya upimaji afya bure kwa wanawake wa jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni ishara ya kuthamini afya ya mwanamke katika maendeleo ya Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika juzi tarehe 8 Machi 2023 katika viwanja vya Karimjee, uliwavuta wanawake wengi waliofika kupima afya zao na kukutana na watalaamu mbalimbali wa masuala ya afya huku mgeni rasmi katika hafla hiyo akiwa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapunduzi Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu.
Huduma zilizotolewa ni pamoja na upimaji wa saratani ya matiti na kizazi, magonjwa ya moyo, kisukari, macho, meno, ushauri kuhusu lishe na uhamasishaji wa bima ya afya kwa wanawake.
Akizungumza kabla ya uzinduzi wa kampeni hiyo Mwenyekiti wa UWT Kata ya Kivukoni, Mariam Kimbisa alisema wameamua kuadhimisha Siku ya Mwanamke duniani kwa upimaji wa afya, kwa kuwa UWT Kata ya Kivukoni inaamini afya ndiyo mtaji katika shughuli za maendeleo na kueleza kampeni hiyo ni endelevu itakuwa ikifanyika kila mwaka Machi 8.

“Wanawake ni jeshi kubwa, sisi UWT Kata ya Kivukoni tunayofuraha kubwa ya kumshukuru Mwenyekiti wetu wa chama Mkoa wa Dar es Salaam ndugu Abbas Mtemvu ambaye amekuja kujumuika nasi na kutuunga mkono katika kampeni hii muhimu katika kuadhimisha siku ya mwanamke duniani
“Katika kutambua siku ya wanawake duniani UWT Kata ya Kivukoni tumeamua kuadhimisha siku hii kwa kutoa huduma ya afya bure kwa akina mama. Tunatumia siku hii kuhamasisha wanawake kutambua umuhimu wa afya bora na vile vile upatikanaji wa huduma za fya bora
“Hii inawezekana kwa kila mwanamke kuwa ana afya bora tukiunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wetu mpendwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikiha wanawake wote nchini wanapata huduma bora ya afya, kwani ukimponya mwanamke umeponya taifa, alisema Mariam.
Machi 8 kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ambapo katika siku hii, wanawake wanakutana na kujadiliana kuhusu mafanikio waliyopata katika sekta mbalimbali, changamoto wanazopitia na jinsi ya kukabiliana nazo.
Leave a comment