May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uwekezaji si lazima pesa nyingi – Dk. Kitila

Prof. Kitila Mkumbo

Spread the love

WATANZANIA wametakiwa kujenga utamaduni wa kuwekeza, kwa kuwa uwekezaji si lazima kuwa na pesa nyingi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Singida…(endelea).

Kauli hiyo imetolewa na Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Singida leo Jumanne tarehe 23 Februari 2021 wakati akizungumza kwenye Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini.

“Kwa sababu hiyo, nitoe wito kwa Watanzania kuanza kubadilisha mitizamo kuhusu uwekezaji, mwekezaji sio lazima awe na mabilioni mengi sana, hapana.”

“Uwekezaji unahitaji tu mtaji, na mtaji unaupata ama kwa kukopa benki ama kwa kuweka akiba yako ama kwa sisi Watanzani kudunduliza,” amesema Prof. Kitila.

Kwenye kongamano hilo, amesema katika taifa lolote, njia moja ya kuongeza shughuli za uchumi ni uwekezaji na kwamba, uwekezaji unaweza kufungua mradi mpya ama kuutanua mradi unaoendelea.

Amesema, si kweli kwamba uwekezaji lazima mtu ama taasisi kuwa na kiwango kikubwa cha fedha, lakini pia si lazima muwekezaji atoke nje ya nchi.

“Uwekezaji haimaanishi uwe mkubwa kwa kiwango kicho, kwamba lazima ije kampuni kubwa, na wala uwekezaji si lazima utoke nje. Muwekezaji ni mtu yeyote ambaye anaamua kununua au kuanzisha rasilimali fulani kwa lengo la kufanya baishara ili baadaye apate faida.

“Wewe mfanyakazi, wewe mkulima, wewe mfanyabiashara unaweza kuweka akiba kidogokidogo hatimaye unapata fedha, unafanya uwekezaji,” amesema.

Pia, ameshauri uongozi wa Mkoa wa Singida kujitangaza ili kuhamasisha wawekezaji kwenda kuwekeza kwenye mkoa huo.

“Ni lazima kuhamasisa uwekezaji. Fursa zipo sasa lazima uwahamasishe wawekezaji, inamaanisha suala la ushawishi, lazima mkoa ujipange kufanya ushawishi ili watu waje Singida na sio Arusha,” amesema.

error: Content is protected !!