April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uvunaji misitu hovyo wapoteza hekta laki nne kwa mwaka

Spread the love

UVUNAJI misitu kwa njia endelevu nchini unapaswa kuendelezwa ili kunusuru uharibifu wa misitu uliopo unaosababisha upotevu wa hekta zaidi ya 469,000 kila mwaka kutokana na ufyekaji misitu unaotokana na mahitaji makubwa ya ardhi ya kilimo. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la kuhifadhi misitu ya asili Tanzania (TFCG), Emmanuel Lyimo alisema hayo jana katika mafunzo kwa wanahabari ya uelewa juu ya mradi wa kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa Tanzania (TTCS) maarufu kama mkaa endelevu.

Alisema, uandaaji mashamba kwa ajili ya shughuli za kilimo cha kuhamahama na uwepo wa mahitaji makubwa ya ardhi kutokana na matumizi ya teknolojia hafifu za kilimo unachangia kwa kiasi kikubwa upotevu wa misitu nchini.

Lyimo alisema, mara kadhaa Serikali kupitia sera imekuwa ikisema matumizi ya mkaa kama nishati majumbani ndio chanzo cha uharibifu na upotevu wa misitu kwa kiasi kikubwa jambo ambalo alisema halina ukweli kutokana na TFCG kuendelea kutoa elimu ya uvunaji mazao ya misitu kwa njia endelevu ambayo inapaswa kufuatwa ili kulinda misitu.

Lyimo alisema, ikiwa wakulima watalima kwa kutumia teknolojia sahihi wanaweza kutumia eneo dogo kuzalisha mazao mengi na kuachana na kuongeza maeneo kitendo ambacho huharibu na kupoteza misitu.

Hivyo alisema, Serikali inapaswa kushirikiana na wadau kuendelea kutoa elimu ya mkaa endelevu na kusambazwa Tanzania nzima na kufanya kilimo hifadhi kuendelea kutumiwa na kupunguza au kuondoa uharibifu na upotevu wa misitu.

Alisema, hatua zisipochukuliwa kwa uharibifu huo wa misitu na mazingira kwa ujumla unaofanywa mapema ni wazi kwamba vizazi vijavyo vitakosa maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Hata hivyo alisema, kupitia utafiti uliofanywa na TFCG kuanzia mwaka 2010-2017 kupitia ufadhili wa mfuko rafiki ujulikano kama Critical Ecosystem Partnership Fund wameweza kubaini kuwa uharibifu wa misitu unatokana na kilimo.

Naye Afisa wa kujengea uwezo kutoka TFCG, Simon Lugazo alisema jumla ya hekta 114,883 za misitu zimehifadhiwa katika vijiji 30 vya wilaya za Mvomero, Kilosa na Morogoro  kupitia mradi wa kuleta mageuzi kwenye sekta ya mkaa Tanzania TTCS.

Lugazo alisema, mradi wa TTCS unalenga kuwasaidia kiuchumi watu maskini kwa kutumia rasilimali za misitu kupitia Serikali ikiwemo kuongeza thamani ya mkaa.

Alisema, kupitia mkaa endelevu wananchi wengi wamenufaika na kuona thamani ya misitu baada ya kufuata uvunaji wa 50 kwa 50 baada ya kutenga hifadhi misitu ya vijiji na uvunaji wa mtindo wa drafti utakaofanya mti kuvunwa tena baada ya miaka 24.

Hivyo alisema, uvunaji misitu kwa njia endelevu unauwezo mkubwa wa kusaidia uhifadhi wa misitu na mazingira kwa ujumla.

error: Content is protected !!