June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uvinje wampigia kelele Rais Kikwete

Spread the love

WAKAZI wa kitongoji cha Uvinje wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani wanamlalamikia Rais Jakaya Kikwete kwamba anaondoka madarakani bila ya kutatua mgogoro wa ardhi uliopo kwa zaidi ya miaka kumi sasa kati ya kitongoji na Hifadhi ya Taifa ya Saadani. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Malalamiko hayo yametolewa leo kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Uvinje, Hussein Akida mbele ya waandishi wa habari.

Kitongoji cha Uvinje, kimoja cha vitongoji vinane vinavyounda kijiji cha Saadani, kilikuwa ni sehemu ya pori la akiba ambalo mwaka 2005 kupitia tangazo la serikali “GN 281 la Septemba 16” lilitangazwa kuwa ni Hifadhi ya Saadani (Saadani National Park – SANAPA).

Ni eneo linalotazamana na fukwe za Bahari ya Hindi, kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, likikutana na uoto wa asili wa nchi kavu. Kusini yake ipo ranchi ya Mkwaja na kaskazini ni pori la akiba linaloambatana na fukwe pamoja na akiba ya Msitu wa asili wa Zaraninge.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa Rais Kikwete anaufahamu mgogoro huo hata kabla hajawa rais lakini ni jambo la kusikitisha kuwa anafikia kung’atuka madarakani mwishoni mwa mwezi ujao na hakujali kusaidia upatikane ufumbuzi.

Kabla ya Oktoba 2005 alipoteuliwa kugombea urais na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kikwete alikuwa mbunge wa Bagamoyo, nafasi aliyoitumikia kwa vipindi vitatu vya miaka mitano mitano.

Akida amesema kuwa licha ya kuwahi kuwa mbunge, Kikwete ni mzaliwa wa jimbo la Bagamoyo ambaye ameshashika nyadhifa mbalimbali ngazi ya taifa lakini ni kama vile hakushughulika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

“Wakazi wa Uvinje hatuna amani kwa miaka mingi sasa hatujasikia hatua zinazotaka kuchukuliwa na serikali yetu wala hali ya kwamba wanajua kuwa wao ndio wenye mamlaka,’’ amesema Akida.

Amesema amechukua hatua mara nyingi za kukutana na baadhi ya viongozi katika serikali ili kuhakikisha kuwa mgogoro huo unakwisha lakini ungali vilevile pamoja na kueneza barua ofisi mbalimbali za kiserikali kama vile Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na hata Ikulu kwa Rais.

Akida amesema watumishi wa Hifadhi ya Saadani wamekuwa wakitoa vitisho kwa wananchi kwa kutumia askari walioshika bunduki hatua inayozusha fadhaa kwa wananchi kwa kuhofia maisha yao.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa wakati Kikwete anazunguka nchi kufanya kampeni Oktoba 2005, aliacha kwenda kijijini Saadani lakini msimamo wake umekuwa kwamba kwa kuwa wananchi wamekuwepo hapo kwa karne, wakitumia ardhi waliyoirithi kwa wazazi wao, ni haki yao kulipwa fidia iwapo serikali inataka kutumia eneo hilo kama hifadhi.

Wakati fulani alisema kwamba ni makosa serikali kuwatisha wananchi hao au kutafuta kisingizio wakadhulumiwa. Mawaziri mbalimbali wa ardhi na walioshika sekta ya maliasili, wameshughulikia mgogoro huo lakini hakuna aliyefanikiwa kuumaliza.

 

error: Content is protected !!