January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UVCCM yamkaanga Spika Ndugai

Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenan Kihongosi

Spread the love

 

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umehoji kwa nini makelele juu ya Serikali kukopa fedha za utekelezaji miradi ya maendeleo, yaibuke baada ya Rais Samian Suluhu Hassan, kuingia madarakani. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Swali hilo limehojiwa leo Ijumaa, tarehe 31 Desemba 2021 , mkoani Iringa na Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenan Kihongosi, akimjibu Spika Job Ndugai, aliyekosoa hatua ya Serikali ya Rais Samia, kukopa fedha kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo.

Katibu Mkuu huyo wa UVCCM amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia, sio ya kwanza kukopa, kwani hata awamu zilizopita zilikopa.

“Kumekuwa na matamko yasiyoeleweka, baadhi ya viongozi ambao tunawaheshimu katika Serikali hii, wameenda mbali wanakosoa na kuona mikopo hii haina tija. Sasa niseme, tangu Awamu ya Kwanza kwa Mwalimu Julius Nyerere na leo ya Rais Samia, hakuna awamu haikukopa fedha, kwa nini haya makelele yaanze baada ya Awamu ya Sita kuwa madarakani?” Amesema Kihongosi.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa, hakuna nchi na au mtu asiyekopa na kwamba hata wabunge bungeni wana mikopo mikubwa.

“Kubwa zaidi, duniani kote hakuna nchi ambayo haikopi fedha, hata ninyi kwenye familia zenu mnadaiwa. Watu mmekopa mabenki huko, mmeweka amana mbalimbali. Wabunge ndani ya Bunge wamechukua mikopo mikubwa, hili jambo linajulikana nani ambaye hakopi?” Amesema Kihongosi.

Kihongosi amesema “fedha ambazo zimekopwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ndiyo Serikali iliyokopa fedha ndogo kulikoa awamu zote tangu tupate uhuru wa nchi hii. Deni letu linakaribia Sh. 70 trilioni, Rais Samia amekopa Sh. 1.3 trilioni na fedha hiyo ameiweka wazi Watanzania wanajua inaenda kufanya kazi.”

Kihongosi amesema kuwa, UVCCM haitamvumilia mtu anayetaka kumkwamisha Rais Samia.

“Sisi UVCCM hatutamvumilia mtu anayevunja heshima ya Rais wetu, tutasimama, tutamlinda Rais wetu na tunasema wazi kabisa, yeyote anayetaka kumkwamisha Rais wetu atakwama yeye, kabla hajamfikia na huo ndiyo msimamo wetu kama UVCCM,” amesema Kihongosi.

Kiongozi huyo wa Vijana wa CCM, amesema kama kuna mtu ana malalamiko au hoja , anapaswa kuzifikisha katika mamlaka husika, kuliko kuzitoa hadharani.

Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM

“Ndani ya CCM tuna utaratibu wa kupeleka malalamiko yetu na hoja zetu, kama kuna jambo limekukwaza kama kiongozi nenda katika utaratibu wa chama, uende ukapeleke mawazo yako. Sio unaenda kuzungumza hoja ambazo zinaanza kuiletea Serikali au hoja zinazoleta ukinzani ambao hauna tija,” amesema Kihongosi na kuongeza:

“Kama kuna mtu anaamini yeye ni mkubwa zaidi kuliko CCM aseme hadharani, ili chama kiweze kuchukua hatua lakini sio unakaa sehemu unajifungia unamtweza Rais wetu, halafu sisi vijana wa CCM tukae kimya, hiyo dhambi hatutakubali kuifanya hata siku moja.”

Kauli hiyo ya Kihongosi ni muendelezo wa viongozi wa CCM, kupinga msimamo wa Spika Ndugai, wa kukosoa hatua ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kukopa kiasi cha Sh. 1.3 trilioni, kutoka kwa Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Job Ndugai

Kwa ajili kukabiliana na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19), ikiwemo kutekeleza baadhi ya miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya, elimu na miundombinu.

Tarehe 27 Desemba 2021 akiwa jijini Dodoma, Spika Ndugai alikosoa hatua ya Serikali kuchukua mkopo huo, akidai kuwa siku moja nchi itapigwa mnada kwa kuelemewa na madeni.

error: Content is protected !!