May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UVCCM yahofia mporomoko ajira za vijana

Kheri James, Mwenyekiti wa UVCCM

Spread the love

 

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umeiomba Serikali ichukue hatua za haraka, kumaliza tatizo la vijana kukosa ajira nchini. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumapili tarehe 23 Mei 2021, na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James, akizungumza kwenye kikao cha umoja huo kilichofanyika jijini Dodoma.

Mwenyekiti huyo wa UVCCM amesema, changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana inazidi kuongezeka, na kuishauri Serikali iboreshe mazingira ya uzalishaji ajira, hasa ajira za mtandaoni kwa kuweka bei rafiki za vifurushi vya intanenti.

“Wale vijana ambao ajira zao tumeshindwa kuwapa huko kwingine, wameamua kujiajiri kupitia hapa (mitandaoni) , biashara imehamia mtandaoni, kazi na masomo yamehamia mitandaoni, kijana aliyeamua kusoma, kufanya biashara mtandaoni kwa MB hizi atafanyaje biashara?” amesema James.

Mwenyekiti huyo UVCCM amesema“nafahamu Dk. Faustine Ndugulile (Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), anafanya kazi nzuri, lakini juhudi ziongezeke sababu mpromoko wa ajira za vijana unazidi kuwa mkubwa. Sisi UVCCM tusipoishauri Serikali tunakuwa hatuna maana ya kuwa hapa.”

James ameishauri Serikali iongeze juhudi katika kukabiliana na changamoto hiyo, ili kuwatengenezwea vijana mazingira mazuri ya kujiajiri mitandaoni.

“Hili jambo lisifanyiwe mzaha, tunaomba na tunajua juhudi zinazochukuliwa na Serikali lakini zifanywe maradufu na matokeo yaonekane.

Tunapozungumzia unemployment (ukosefu wa ajira), zipo ajira ambazo Serikali mnatengeza, lakini yapo mazingira mnayatengeneza ili watu wajiajiri wenyewe. Mazingira mnayopaswa kutengeneza kwa nguvu watu kujiajiri, ni kupitia njia mtandao,” amesema James.

James amesema kwa sasa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), inaajiri watu wengi, hivyo ni lazima Serikali iweke njia rafiki katika kukidhi matakwa ya teknolojia hiyo.

“Tehama inaajiri watu lakini hakuna Tehama bila mb bando, hatuwezi kuhubiri innovation kama njia ya kufikia innovation ina vikwazo, hatuwezi kuhubiri mabadiliko ya kiteknolojia kama njia ya kufikia zinavikwazo,” amesema James.

Aidha, James ameishauri Serikali iboreshe mazingira ya uwekezaji, ili nafasi za ajira ziongezeke nchini.

“Tunazungumzia habari ya uwekezaji na Mungu bariki iko chini ya waziri mkuu, tunapochelewa kwenye uwekezaji muhanga wa uwekezaji kutofanikiwa ni vijana, hao vijana ndiyo wanakwenda kujiajiri kupitia mazingira ya viwanda kufunguliwa,” amesema James na kuongeza:

“Tuna jukumu la kutengeneza mazingira wawekezaji kutafutwa, sababu wakija tunapunguza tatizo la uhaba wa ajira, uwekezaji tuusukume kwa nguvu kubwa lakini uwe uwekezaji unaowainua vijana.”

error: Content is protected !!