June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UVCCM wataka Askofu Gwajima asurubiwe

Askofu Josephat Gwajima

Spread the love

 

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umekitaka chama hicho kimuadhibu Mbunge wake wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima, kufuatia hatua yake ya kupinga mpango wa Serikali, wa kuwachanja wananchi chanjo ya Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumanne, tarehe 27 Julai 2021 na Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenan Kihongosi, siku mbili baada ya Askofu Gwajima kuibuka hadharani na kupinga mpango huo, akidai kwamba chanjo hizo sio salama kwa afya ya wananchi.

Askofu Gwajima alitoa msimamo huo Jumapili, tarehe 25 Julai mwaka huu, akihubiri katika Kanisa lake la Ufufuo na Uzima, Ubungo mkoani Dar es Salaam.

“Tunaomba chama kiwachukulie hatua kali na waache mara moja tabia ya kuropoka pasipo mipaka. Kwa sababu pia demokrasia ya kuongea ina uhuru lakini isipitilize, kwa hiyo hilo jambo limetukwaza tunaomba chama kichukue hatua za kinidhamu,” amesema Kihongosi.

Kihongosi amesema kuwa, msimamo huo wa Askofu Gwajima alioutangaza kanisani kwake, umepotosha wananchi dhidi ya chanjo hiyo.

“Juzi tumeona baadhi ya viongozi wakizunguzma matamshi yasiyofaa, mbunge wa Kawe ametoa maneno yasiyofaa kuhusu chanjo na chanjo imeshaletwa. Anatokea kiongozi mmoja wa mhimili anazungumza kanisani na kuhubiria waumini ambao wana watu wengine nje, anatuma ujumbe kwamba hiyo chanjo haifahi,” amesema Kihongosi.

Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenan Kihongosi

Katibu mkuu huyo wa UVCCM, amesema Askofu Gwajima alipaswa kupeleka hoja zake katika vikao vya chama, badala ya kuzimwaga hadharani kinyume na maadili ya CCM.

“Ile kauli tunailaani na tunazipinga vikali, sababu utaratibu wa CCM kama mbunge ana hoja anapeleka katika utaratibu wa vikao. Lakini unapokwenda kwenye umma ukawaambia Watanzania, atakayediri kuwaambia watu wachanje atakufa lazima atambue yeye sio Mungu,” amesema Kihongosi.

Akitangaza msimamo wake huo, Askofu Gwajima alisema si busara kuwapa watu chanjo ambayo haijafanyiwa tathimini, kubaini athari zake kiafya katika kipindi cha muda mfupi au mrefu.

Askofu Gwajima aliwataka Watanzania wasitumie chanjo hiyo kwa madai kwamba ina madhara.

Msimamo huo wa Askofu Gwajima, unakwenda kinyume na msimamo wa Serikali ya Rais Samia, wa kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa hiari kwa wananchi.

Tayari Serikali ya Tanzania imeingiza chanjo hiyo, ambayo inatolewa bure kwa wananchi wanaohitaji.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Serikali imekubali kuingiza chanjo hiyo, baada ya wataalamu wa afya nchini, kujiridhisha kwamba haina madhara.

error: Content is protected !!