January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UVCCM “wamchome” Chegeni

Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) wa wilaya hiyo, Raphael Chegeni

Spread the love

MZOZO mkali unafukuta ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Lamadi wilayani Busega-Simiyu, hatua ambayo inamweka pabaya Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) wa wilaya hiyo, Raphael Chegeni, Anaandika Mwandishi wetu, Mwanza  (endelea).

Hali hiyo ni baada ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) katika kata hiyo, kukiomba chama, kimchukulie hatua ya kumvua uanachama, Chegeni, iwapo ataendelea na utovu wa nidhamu.

UVCCM wametoa tamko hilo kutokana na Chegeni `kudandia’ misaada iliyotolewa na taasisi mbalimbali wakati wa mafuriko yaliyotokea Aprili mwaka huu, kata ya Lamadi pamoja na kumkashifu mbunge wa Busega, Titus Kamani, kwamba aliwapiga mabomu wananchi wakati wa uchaguzi wa 2010. 

Wanasema kuwa, Chegeni amekuwa akimkashifu Dk. Kamani-aliye Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, kwamba maendeleo aliyoyafanya jimboni na misaada aliyoitoa wakati wa mafuriko kuwa si chochote bali analazimisha siasa.

Kutokana na hatua hiyo, wameiomba CCM imchukulie hatua kali pamoja na baadhi ya viongozi wanaotumia vibaya madaraka yao na kukidhalilisha chama, wakiwemo Mwenyekiti wa Wilaya, George Mshoni na Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya, Samuel Ngofilo.

Walitoa tamko hilo hivi karibuni wakati wa kikao cha Baraza la Vijana Kata na kumtaka Chegeni akawaombe radhi wana CCM na wananchi wa Lamadi ambao amekuwa akiwakashifu.

Wakichangia katika kikao hicho,Kaswalala Elisha, Yunis John, Priscar Maloba, Aron Dominic, Bujiku Mathias, Chares John na Makubu Joseph, walidai kitendo cha Chegeni kuhutubia wananchi wakati wa mafuriko na kumkashifu mbunge wao ni kinyume na maadili ya CCM.

“Siku hiyo akiwa na wenyekiti wa CCM na UVCCM wa wilaya, Chegeni alitoa kashfa kwa Mwenyekiti wa Chama mkoa na kutangaza kuwa mashina yote ya CCM aliyoyafungua ni batili, hawayatambui,hivyo lazima wayafungue upya. Huu ni utovu wa nidhamu,”alidai Moody Gimonge.

Gimonge ambaye ni Katibu Mwenezi wa UVCCM wa Kata hiyo, amesema mwanzoni mwa mwaka huu, baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Chegeni alifanya kikao cha chama Lamadi na kudai baadhi ya wenyeviti wa vitongoji na kijiji cha Lamadi hawakushinda kihalali, hivyo uchaguzi utarudiwa.

Shutuma nyigine walizomshushia Chegeni ni pamoja na kukataa kupokea kadi na wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani kwa madai kuwa hawezi kupokea makapi na kuwamba, Dk. Kamani ndiye alileta mabomu waliyopigwa Lamadi wakati wa vurugu za uchaguzi huo.

Wamesema wakati wa mafuriko, Aprili 9 mwaka huu, Chegeni akiambatana na taasisi za Bima ya Afya, Mamlaka ya Bima na Mfuko wa Benjamin Mkapa, alitangaza kwenye mkutano wa hadhara kuwa misaada waliyopeleka ni blanketi 100, magodoro 50, unga wa sembe tani 8, sukari tani 1 na maharagwe tani 1 lakini idadi hiyo haikuwa sahihi.

Badala yake, vijana hao wamesema, sembe ilikuwa tani 5 na maharage kg 500 na kwamba,Chegeni alipewa Sh. 5 milioni na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa kwa ajili ya waathirika wa mafuriko hayo lakini hakuzifikisha.

Chegeni ametafutwa kwa siku mbili kujibu tuhuma hizo, lakini simu yake ya kiganjani iliita na kukatwa; hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneo (sms) haukujibu.

Habari za kuaminika ambazo zimethibitishwa na Katibu wa CCM mkoa wa Simiyu, Hilda Kapaya, Chegeni na vigogo wengine watatu wa chama na UVCCM wilaya ya Busega, wamehojiwa kuhusiana na ukiukwaji wa maadili.

error: Content is protected !!