June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

UVCCM wakiri ngoma nzito Mwanza

Spread the love

UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Mwanza, umesema kuwa hautasahau mapambano magumu yaliyofanyika katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana ili kuking’oa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika majimbo ya Nyamagana na Ilemela, anaandika Moses Mseti.

Majimbo hayo yalikuwa chini ya wabunge wa Chadema, Ezekiel Wenje (Nyamagana) na Highness Kiwia (Ilemela), kwa kipindi cha 2010/2015 kabla ya kuangushwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana. 

Waliokuwa wagombea ubunge wa CCM, Stanslaus Mabula (Nyamagana) na Angelina Mabula (Ilemela) ndiyo walioibuka na ushindi licha ya Wenje na Kiwia kufungua kesi za kupinga ushindi huo hata hivyo Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilizitupilia mbali.

Hussein Kimu, Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Nyamagana, amesema, “Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulikuwa mgumu sana na kwa hakika vyama vya upinzani vilikuwa vimejipanga, kilichotuokoa sisi ni umoja wetu ndani ya CCM.

Majimbo ya Ilemela na Nyamagana ni kama Baba na Mama na isingewezekana kurudisha Jimbo moja halafu lingine likabakia upinzani ndiyo maana ilitulazimu kutumia nguvu kubwa na tubatoa shukrani kwa kila kijana aliyejitolewa kwa nafasi yake.”

Kimu alikuwa akiongea na wafanyabiashara ndogondogo (machinga, katika hafla iliyofanyika na kuhudhuriwa na John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Kwa upande wake Mongella,amesema kuwa ndani ya CCM kuna watu wengi wamekuwa wakitumia fedha kupata uongozi na kuahidi ya kwamba kama Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM katika mkoa huo hatakubali kupitisha jina la mtu aliyetumia rushwa kupata uongozi.

“Watu wengi sasa hivi wanaandaa mafungu ya kuwapa watu, labda niseme tu, utawala wa sasa hakuna rushwa na atakayetumia rushwa itakuwa imekula kwake,” amesema Mongella.

Mkutano huo ambao uliambatana na zoezi la kuchangia damu na mafunzo maalamu ya ujasiriamali kwa vijana wa UVCCM, washiriki waliohudhuria walikuwa wachache tofauti na matarajio ya wandaaji.

 

 

error: Content is protected !!