June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

UVCCM ‘kumchongea’ Ndalichako kwa Magufuli

Spread the love

DAKIKA chache baada ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) taifa, kutoa tangazo la kuwataka wanafunzi waliokosa mikopo wakati wana vigezo, kuandikisha majina yao kupitia barua pepe ya UVCCM, jumuiya hiyo imeahidi kupeleka orodha hiyo kwa Rais John Magufuli, anaandika Charles William.

Tangazo la UVCCM limesema vielelezo vya kuthibitisha sifa za mwanafunzi kupata mkopo ikiwemo vyeti vya kifo au vifo vya wazazi au hali ya familia anayotoka, vitumwe kupitia barua pepe ya jumuiya hiyo ambayo ni uvccm1978@gmail.com huku mwisho wa kutuma ni tarehe 4 Novemba 2016.

Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa njia ya simu Sylvester Yaredi, Kaimu Katibu Idara ya Uhamasishaji, Sera, Utafiti na Mawasiliano UVCCM, ametoa ufafanuzi wa tangazo hilo ambapo amesema watapeleka orodha ya majina hayo kwa rais kwani wanaamini ataingilia kati suala hilo.

“Hatutachukua fedha kutoka kwenye mfuko wa UVCCM ili kuwasomesha vijana waliokosa mikopo kama baadhi wanavyodhani, tutachofanya ni kuandaa orodha ya wanafunzi pamoja na vielelezo vinavyothibitisha sifa zao kupata mikopo.

Baada ya hapo tutapeleka documents (nyaraka) hizo kwa Rais Magufuli kwasababu yeye amekuwa akifuatilia suala hili kwa umakini, ndiyo maana amekuwa mkali mara kwa mara kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu pale inapochelewesha malipo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu,” amesema Yaredi.

Kuipeleka orodha hiyo kwa Rais Magufu huenda ikawa ni kumuweka kikaangoni Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwani ndiye msimamizi wa uwajibikaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu (HESLB).

Kwa kipindi cha wiki tatu sasa tangu vyuo vikuu hapa nchini vilipoanza kufunguliwa, vilio vya wanafunzi kukosa mikopo vimesikika vyuoni. Serikali imekuwa ikilaumiwa kwa kupunguza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo.

Vigezo vipya vya kupata mikopo vilivyotangazwa na serikali tarehe 12 Oktoba mwaka huu kupitia kwa Mhandisi Stela Manyanya, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ‘vimefinya’ wigo wa wanufaikaji. Hata hivyo, bado baadhi ya wale wenye vigezo tajwa wamekosa mikopo hiyo.

Wiki mbili zilizopita, Abdulrazaq Badru, Mkurugenzi wa HESLB aliwaeleza wanahabari kuwa kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mkopo mwaka huu, watakaopewa ni 21,500 tu. Siku nne baadaye Prof. Ndalichako alinukuliwa akisema, serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi 25,000.

Idadi hiyo ni pungufu ya zaidi ya wanafunzi 15,000 ya waliopata mikopo mwaka jana ambapo jumla ya wanafunzi 40,836 walipata mikopo.

Kama hilo halitoshi, mchana wa leo Jumapili ya tarehe 30 Oktoba, 2016 Badru amewaeleza tena wanahabari kuwa, HESLB itawapitia upya wanafunzi wanaoendelea na masomo vyuoni ili kubaini ambao hawakidhi vigezo vipya na kuwaondoa.

error: Content is protected !!