September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

UVCCM Arusha kwazidi kuwaka moto

Spread the love

TUHUMA za Lengai Ole Sabaya, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Arusha, kufanya utapeli na kujipatia fedha kwa kujitambulisha kama ofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), limezidi kukivuruga chama hicho, anaandika Charles William.

Mapema leo asubuhi, baadhi ya wanachama wa UVCCM wametwangana makonde, baada ya baadhi yao kutaka kuifunga ofisi ya chama hicho, wakidai mwenyekiti wao, Sabaya ambaye pia ni diwani wa kata ya Samabashi wilaya ya Arumeru, hana tena uhalali wa kuungoza umoja huo.

Sabaya anadaiwa kujihusisha na vitendo vya utapeli mkoani Arusha kwa muda sasa huku akilindwa na baaadhi ya vigogo wa CCM sambamba na Jeshi la Polisi mkoani humo ambalo linalaumiwa kutomkamata wala kumfikisha mahakamani kila anaposhitakiwa.

Watoaji wa tuhuma hizo wamesambaza katika mitandao baadhi ya nyaraka zinazoonesha vitambulisho ‘feki’ vinavyomtambulisha Sabaya kama ofisa usalama wa taifa, lakini pia wameonyesha kile wanachodai kuwa ni ‘RB’ za Jeshi la Polisi ili kijana huyo akamatwe.

Hata hivyo, Sabaya amemwambia mwandishi waMwanaHALISI online kwa kifupi kuwa, tuhuma hizo zinasambazwa na wasiopenda kazi yake ya kukinyoosha na kukirudisha chama hicho katika misingi mkoani Arusha, hata hivyo hakufafanua undani wa tuhuma hizo.

“Wanaonituhumu wanafanya kazi kwenye karakana ya ibilisi, hivi karibuni ngano na magugu vitatengwa. Mimi sitoacha kupambana na rushwa za kihalifu ndani ya miradi ya UVCCM Mkoa na viongozi wote waliohusika na hili lazima wawajibishwe,” amesema Sabaya na kuongeza;

“Utasikia makubwa zaidi hadi nitakapomaliza kazi ya kuileta CCM anayoitaka Rais Magufuli hapa Arusha.”

Sabaya hakuwa tayari kueleza kuhusu kitambulisho cha idara ya usalama wa taifa kinachodaiwa kuwa chake, hakutaka pia kufafanua kiundani kuhusu watu mbalimbali kumshitaki kwa utapeli huku kesi hizo zikidaiwa kuzimwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha.

MwanaHALISI online limemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Charles Mkumbo kwa kumpigia simu zaidi ya mara nne ili atoe ufafanuzi wa suala hilo, hata hivyo simu yake iliita bila kupokelewa.

Alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi ‘SMS’ hakuweza kujibu ujumbe huo licha ya kumfikia.

Shaka Hamdu, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM taifa, amesema kuwa tayari yupo mkoani Arusha, kutafutia ufumbuzi wa vurugu baina ya vijana wa umoja huo ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa ofisi kwa nguvu na mwenyekiti wa umoja huo kudaiwa kukataa kumpokea Katibu wa UVCCM Mkoa aliyepangiwa kazi hivi karibuni.

“Nipo Arusha tayari, nashughulikia suala hili na nitalitolea tamko leo leo,” amesema Shaka kwa njia ya simu.

 

error: Content is protected !!