March 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Utumiaji maji safi na salama, kinga kubwa ya kipindupindu

Spread the love

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesisitiza jamii ya Tanzania juu ya utumiaji wa maji safi na salama ili kuweza kupambana na ugonjwa wa kipindupindu kwa urahisi. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara ya Afya) Dk. Mpoki Ulisubisya wakati wa ufunguzi wa kikao cha siku tatu cha kujadili mikakati ya kukabiliana na ugonjwa kipindupindu nchini kinachoendelea jijini Dodoma.

“Ili kupambana na ugonjwa huu Watanzania wanatakiwa kutunza mazingira hasa kutumia vyoo bora pamoja na kutumia maji safi na salama katika jamii inayotuzunguka,” amesema Dk. Ulisubisya.

Aidha Dk. Ulisubisya amesema kuwa hadi sasa kwa takwimu iliyopo inaonesha kuwa watu elfu 32 wameugua na watu 600 wamepoteza maisha.

Dk. Ulisubisya amesema kuwa ili kuweza kutokomeza ugonjwa huo mpaka kufikia 2030 wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya maji, TAMISEMI, na wadau wengine wa afya wanatakiwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kuweka mikakati ya kupambana na ugonjwa wa kipindupindu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Prof. Faustine Kamuzora amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaweka pamoja wataalam mbalimbali kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa kipindupindu nchini Tanzania.

Aidha Prof. Kamuzora amesema kuwa tayari wameshaandaa madawati mbalimbali ya wataalamu katika ofisi yake ili kuwexa kuweka mifumo ya kushughulikia kwa uharaka magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu.

Naye Afisa wa kudhibiti na kukinga Magonjwa kutoka Shirika la Afya Duniani hapa nchini Dk. Grace Saguti amesema kuwa kutokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali Serikali ya Tanzania imeweza kufanikiwa kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu kwa sehemu kubwa ya Tanzania.

“Mpaka hivi sasa mikoa inayokabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo yake ni Rukwa, Songwe na Arusha lakini maeneo yote yaliyobaki tumefanikiwa kutokomeza ugonjwa huo,” amesema Dkt. Saguti.

MWISHO.

error: Content is protected !!