Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Uteuzi wahadhiri serikalini waibua mjadala bungeni
Habari za Siasa

Uteuzi wahadhiri serikalini waibua mjadala bungeni

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania
Spread the love

 

ANATROPIA Theonest, Mbunge Viti Maalum asiye na chama bungeni, amehoji mkakati wa Serikali, katika kuziba pengo la wahadhiri wa vyuo vikuu, wanaoteuliwa kushika nafasi mbalimbali serikalini. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).

Theonest amehoji hayo leo Jumanne tarehe 1 Juni 2021, bungeni jijini Dodoma, baada ya Mbunge Viti Maalum (CCM), Dk. Thea Medard Ntara, kueleza changamoto ya uhaba wa wahadhiri vyuoni, akiitaka Serikali kuweka mazingira mazuri ya wahadhiri wa kigeni kufanya kazi nchini.

“Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia wasomi, wahadhiri na maprofesa wakiondoka katika taasisi za kufundisha na kuingia katika utumishi mwingine tofauti,” amesema Theonest na kuongeza:

“Je, upi mkakati wa Serikali kama uikimuondoa profesa katika chuo fulani, anaweza kuwa replaced (kubadilishwa), ili kuondoa pengo linajitokeza?”.

Baada ya Theonest kuuliza swali hilo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimjibu akisema wahadhiri walioteuliwa ni wachache.

“ Walioondoka wachache sana, Waziri wa Nchi majibu ya kina kuhusu wahadhiri wanapoondoka huko,” amesema Spika Ndugai.

Kufuatia mjadala huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amesema Serikali hufanya teuzi hizo kwa kuzingatia idadi ya wahadhiri waliopo, ili kukwepa upungufu wa wakufunzi hao.

“Ndani ya Serikali kupitia sheria za utumishi wa umma, ipo mipango kuhakikisha ikama za utumishi wa umma zinazingatia mahitaji tuliyonayo nchini.

Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu)

Kwa hiyo mbunge asiwe na wasiwasi, tutaendelea kusimamia mifumo tuliyoweka kuhakikisha upungufu haupatikani wataalamu watakapoteuliwa sehemu nyingine.,” amesema Mhagama.

Miongoni mwa wahadhiri walioteuliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati John Magufuli, ni waliokuwa Wahadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akiwemo Prof. Kitila Mkumbo, aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, mwaka 2017 .

Na Dk. Benson Bana, ambaye mwaka 2019 aliteuliwa kuwa Balozi.

Awali, Dk. Ntara alisema vyuo vingi vina uhaba wa wahadhiri na kuiomba Serikali iboreshe mifumo ya utoaji vibali vya wahadhiri wa nchi za nje, ili kukabiliana na upungufu huo.

“Niseme kwamba mpaka sasa vyuo vikuu vina shida ya wahadhiri na mfumo unachukua muda mrefu mno, mtu anaomba kibali inachukua zaidi ya siku sita. Lini watarekebisha na kuona huo mfumo unakuwa mwepesi ili tupate wahadhiri wa kutosha wa vyuo vikuu,” amesema Dk. Ntara.

Akijibu ombi hilo, Mhagama alisema Serikali imeanzisha Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Maombi ya Vibali vya Kazi na Ukaazi kwa raia wa kigeni, wanaokuja kufanya kazi nchini, ambao umeondoa changamoto ya vibali hivyo kuchelewa kutoka.

Mhagama alisema mfumo huo umeanza kufanya kazi kwa majaribio tarehe 23 Aprili 2021.

“Ili kuweka mazingira mazuri ya kuruhusu uwepo wa wafanyakazi wa kigeni nchini, Serikali imeanzisha Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Maombi ya Vibali vya Kazi na Ukaazi kwa raia wa kigeni , umeanza kutumika kwa majaribio (piloting) kuanzia tarehe 23 Aprili, 2021,” amesema Mhagama.

Waziri huyo mwenye dhamana ya masuala ya kazi, amesema mfumo huo unatoa vibali ndani ya siku mbili, baada ya kupokea maombi.

“Tulitambua kwamba mifumo tuliyokuwa nayo nyuma inaleta matatizo na kusababisha ucheleweshaji mkubwa sana wa utoaji vibali vya wageni, mfumo uliopo sasa ni mpya na tulipofanya majaribio kibali kinaweza kutoka ndani ya siku moja au mbili,” amesema Mhagama.

1 Comment

  • Wanatafua ulaji. Ndio maana yule profesa mmoja alimshukuru Rais kwa kumtoa pale jalalani (Chuo Kikuu cha Dar) na kumpa ulwa katika baraza la mawaziri
    Mapato ya waziri mmoja ni sawa na mishahara ya maprofesa kumi pale Mhimbili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kamati ya Bunge yaitaka Serikali kuchunguza dawa za asili

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo...

Habari za Siasa

Kada NCCR-Mageuzi aliyepotea aokotwa porini akiwa taabani, hajitambua

Spread the love  MWENYEKITI wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha NCCR-Mageuzi,...

Habari za Siasa

ACT Wazalendo yataka Jaji Mkuu, Jaji Biswalo wajiuzulu kupisha uchunguzi fedha za Plea Bargaining

Spread the love  CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimemtaka Jaji wa Mkuu wa Tanzania,...

Habari za Siasa

Kigogo ACT-Wazalendo: Vyama vya upinzani vilikosea kumpokea Membe, Lowassa

Spread the love  KATIBU Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema...

error: Content is protected !!