Friday , 29 September 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Uteuzi wa mawaziri, umesheheni matundu
Makala & Uchambuzi

Uteuzi wa mawaziri, umesheheni matundu

Rais John Magufuli akiendesha kikao cha baraza la Mawaziri muda mcheche baada ya kufanya mabadiliko
Spread the love

Na Mwandishi Maalum

RAIS John Pombe Magufuli, ametangaza mabadiliko katika baraza lake la mawaziri kwa kuondoa baadhi, wengine kuwahamisha na wapya kuingizwa.

Miongoni mwa waliondolewa, ni Prof. Jumanne Maghembe, aliyekuwa waziri wa maliasili na utalii, Gerson Lwenge, aliyekuwa naibu waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Annastazia Wambura na naibu waziri wa maliasili na Utalii, Ramo Makani.

Alisema, amefanya mabadiliko hayo kutokana na kuwepo na nafasi za wazi ambazo zinahitajika kujazwa. Ni kufuatia kujiuzulu kwa Prof. Sospiter Muhongo aliyekuwa waziri wa nishani na madini na George Simbachawene, aliyekuwa Tamisemi.

Mawaziri wapya, ni Hamis Kigwangwala, Issack Kamwele, Luhaga Joelson Mpina, Medard Kalemani na George Mkuchika.

Baraza la mawaziri lililotangazwa na Rais Magufuli, Jumamosi iliyopita, lina mawaziri 21 na naibu mawaziri 20.

Haya ni mabadiliko ya kwanza makubwa kufanywa na Rais Magufuli, tangu aingie madarakani Novemba 2015. Wapo wanaosema, huu ni mtego wa kwanza, kanasa kutokana na kauli yake kuwa “nitateua baraza dogo la mawaziri, lenye watu wasafi na wachapa kazi.”

Swali ambalo wananchi wanajiuliza ni hili: Mabadiliko haya yamezingatia hicho alichokisema? Mabadiliko yamezingatia uwapo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar? Mabadiliko yamepunguza gharama za uendeshaji wa serikali? Tujadili:

Kwanza, mabadiliko katika baraza la mawaziri limefanya idadi ya mawaziri kuongezeka kutoka watu 32 waliokuwapo katika baraza lililopita, hadi kufikia 41 waliotangazwa na kuapishwa Jumatatu wiki hii.

Hili ni ongezeko la watu tisa, takribani asimilia 28 ya mawaziri waliokuwapo. Ni kinyume na ahadi yake kwa wananchi aliyoitoa wakati wa kampeni na alipotangaza baraza lake la kwanza la mawaziri, tarehe 10 Desemba mwaka 2015.

Akihutubia taifa kutokea Ikulu jijini Dar es Salaam, siku hiyo, Rais Magufuli alisema, aliyekuwa mtangulizi wake – Jakaya Mrisho Kikwete – aliunda baraza lililobeba mawaziri na naibu mawaziri zaidi ya 59.

Lakini yeye ameamua kuunda baraza dogo lenye wizara 18 na mawaziri 19 ili “kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali.”

Alidai kuwa baadhi ya wizara ameziunganisha. Nyingine, amezipa mawaziri, lakini hakuteuwa naibu mawaziri.

Lakini sasa – miaka miwili baada ya kukaaa Ikulu – Rais Magufuli, hakuishia kupanua baraza la mawaziri kwa kuongeza manaibu mawaziri, ameimega wizara ya nishati na madini na kuifanya wizara mbili.

Magufuli ama kwa bahati mbaya au kwa makusudi, uteuzi wake umeibua hisia kali za ukanda na ukabila. Ameruhusu baadhi ya wapinzani wake wa kisiasa, kumtuhumu upendeleo na kudai kuwa anaangalia kanda fulani na kupuuza kanda nyingine.

Kwa mfano, wanataja kanda ya Ziwa Victoria, kuwa imeoa idadi kubwa ya mawaziri na naibu mawaziri, ukilinganisha na kanda nyingine.

Huko ndiko walikoibuliwa Dk. Medard Kalemani, Luhaga Joelson Mpina, Stanslaus Haroon Nyongo, Angelina Sylivester Mabula, Charles John Tizeba, Kangi Alphaxard Lugola, George Joseph Kakunda, Elias John Kwandikwa, Hamisi Andrea Kigwangalla na Charles Paul Mwijage.

Kanda nyingine iliobahatika kutoa idadi kubwa ya mawaziri na naibu mawaziri, ni Mbeya. Huko ndiko wameibuliwa Dk. Harisson Mwakyembe, Juliana Shonza, Merry Mwanjelwa na Josephat Ngailonga Hasunga.

Mkoa wa Kilimanjaro, haukupata bahati ya kutoa waziri na hata naibu waziri. Hii ni mara ya kwanza katika hostoria ya taifa hili.

Anayetajwa na baadhi ya watetezi wa rais kuwa ni kutoka Kaskazini, Angellah Kairuki, ni mbunge wa Viti Maalum jijini Dar es Salaam na anahudumu kama diwani katika halmashauri ya manispaa ya Kinondoni.

Hata usawa kwenye mgawanyo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, haukuzingatiwa katika mabadiliko haya. Kati ya mawaziri na naibu mawaziri 21, Zanzibar ina mawaziri wawili – Prof. Makame Mbalawa na Hussen Mwinyi na naibu mmoja, Yusuf Masauni.

Katika wizara sita zinazojihusisha moja kwa moja na masuala ya Muungano – mawasilino na uchukuzi, mambo ya nje, fedha na mipango, Muungano, mambo ya ndani na ulinzi – zenye mawaziri sita na manaibu mawaziri saba, Zanzibar imeambulia mawaziri wawili na naibu waziri mmoja.

Hata ofisi inayoshughulikia Muungano wenyewe inaongozwa na watu kutoka Bara. Ni January Makamba na Lugola.

Haya yaliyotendwa na Magufuli, ni kinyume na dhamira ya uanzishwa wa Muungano na makubaliano ya kuundwa kwa Muungano wenyewe kulikofanywa na waasisi wa taifa hili, Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.

Kama rais haundi baraza lake kwa masuala mazito kama Muungano na ukanda, anawezaje kuangalia jinsia za watu? Anawezaje kuunda wizara ya walemavu, wazee na watoto na wasanii? Huku siyo kujenga matabaka?

Ni kweli kuwa siyo lazima kila mkoa utoe waziri au naibu waziri. Wala siyo lazima kila dini na kila kabila litoa waziri au naibu mawaziri.

Lakini kama katika maeneo hayo, wapo watu wenye sifa, ni vema uteuzi ukazingatia uwiano wa ukanda, ukabila na udini.

Hii ni kwa sababu, mawaziri wanaweza kupendelea wanakotoka, jambo ambalo litaingiza nchi katika mgogoro wa kisiasa na kiuchumi. Hili limeshawahi kufanyika katika tawala zilizopita.

Pili, kwa jinsi mabadiliko yalivyofanyika na aina ya watu waliongizwa serikalini, inathibitisha kuwa Rais Magufuli “hakujiandaa kuwa rais.”

Siyo kwamba alikuwa hautaki, la hasha! Hakuamini kama njia aliyoitumia kuwa rais inakubalika.

Alama ya haraka kwenye serikali ya Rais Magufuli ni kukataa kukosolewa wakati kukosolewa ni “kuambiwa ukweli mwingine” tofauti na ule ulioshikilia.

Ni kama alivyokuwa Kikwete. Aliutaka sana urais. Alijiandaa kwa muda mrefu; lakini hakwenda zaidi ya kuwa rais. Baada ya kuupata hakujua aufanyie nini.

Ndoto yake ilikuwa imetimia na alibaki hivyo kwa miaka yake 10. Ndivyo itakavyokuwa kwa Magufuli. Kila uchao Maguguli anaibua mjadala mpya. Safari hii ameibua mjadala wa upendeleo.

Mathalani, Rais Magufuli amepuuza madai kuwa Kalemani, ni mmoja wa watuhumiwa wakuu katika kuingiza nchi hii kwenye mikataba ya kinyonyaji wakati akiwa mwanasheria wa wizara ya nishati na madini.

Mikataba mibovu katika wizara ya nishati na madini, ndio sababisho kuu lililotajwa la kujiuzulu kwa aliyekuwa bosi wa Kalemani, Prof. Sospeter Muhongo.

Aidha, Rais Magufuli anaonekana kufanya kazi kwa orodha ya mahitaji. Siyo kwa kutumia vipaumbele.

Ndiyo maana kila kukicha ni kukimbizana na utendaji na mahitaji ya Dar es Salaam kana kwamba jiji hilo ndiyo Tanzania.

Pamoja na kutokamilika kwa uwanja wa ndege Mwanza na kuwapo msongamano mkubwa wa magari, kuna ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Chato.

Eneo hili lina viwanja vidogo Geita, Biharamulo na Kahama. Kama ni suala la usafiri wa rais kwenda nyumbani vingetumika hivyo.

Rais Magufuli anapaswa kufahamu kuwa yuko kwenye nchi yenye upungufu wa karibu kila kitu isipokuwa umaskini.

Anapaswa kufahamu kama ni harusi, basi sasa amemaliza fungati na amerudi nyumbani kuanza maisha mapya. Hakuna tena michango wala vigelegele.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Prof Mwafenga ulijiamini katika utendaji wako na degree zako 10 – Maige

Spread the loveKIFO cha Prof Hadley Mpoki Mwafenga- Afisa Usimamizi wa Fedha...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Hii ndio sura halisi ya Rais Samia

Spread the loveKILA zama na kitabu chake. Hizi ni zama za Rais...

Makala & Uchambuzi

Safari ya Siah Malle katika uhandisi inavyoibua vipaji vipya vya wanawake

Spread the loveSiah Malle ni mfano mzuri wa mwanamke ambaye amefanikiwa kuvunja...

Makala & Uchambuzi

Rekodi ya watalii kuandikwa Desemba 2023

Spread the love  WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema ifikapo Desemba 2023...

error: Content is protected !!