Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Uteuzi wa Dk. Bashiri utata mtupu
Habari za SiasaTangulizi

Uteuzi wa Dk. Bashiri utata mtupu

Spread the love

 

KATIBU Mkuu Kiongozi (CS) wa Tanzania, Dk. Bashiru Ally, ameibua utata mpya wa kisheria, kufuatia kuendelea kuhudumu katika wadhifa wake wa katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma, Na. 1 wa mwaka 2015, Dk. Bashiru; na au mtu mwingine yeyote mwenye nafasi kama yake ama inayokaribiana na yake, ni marufuku kuwa kiongozi katika chama cha siasa.

Dk. Bashiru aliteuliwa na Rais John Magufuli, kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, tarehe 26 Februari mwaka huu na tayari ameanza majukumu yake.

Amechukua nafasi ya Balozi John Kijazi, aliyefariki dunia, tarehe 17 Februari 2021, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa gazeti la kila wiki la Raia Mwema, mpaka jana Jumanne, Dk. Bashiru, alikuwa hajatamka hadharani kujiuzulu wadhifa wake ndani ya CCM.

Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma, umeeleza kuwa sababu za kuzuia watumishi wa umma kuwa wanasiasa, ni kuepusha kuwapo kwa mgongano wa maslahi.

Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma, umesainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, tarehe 2 Januari 2015. Umeanza kutumika, tarehe 1 Desemba 2014.

Anasema: “Baadhi ya watumishi wa umma wenye nafasi za uongozi wa kisiasa, wamekuwa wakitoa huduma kwa upendeleo, hususan pale ambapo anayehudumiwa ni mpiga kura wake au anatoka chama cha siasa tofauti na chake.”

Ikumbukwe kuwa uteuzi wa Dk. Bashiru kutoka kuwa Katibu Mkuu wa CCM hadi Katibu Mkuu Kiongozi, uliibua mjadala mzito ndani na nje ya chama hicho; kutokana na kuwa mtu wa kwanza kuteuliwa kushika nafasi hiyo, kutokea kwenye chama cha siasa, badala ya utumishi wa umma.

Kwa mujibu wa kifungu cha 3.1.6 cha waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma, ni kwamba “mtumishi wa umma, atakayeamua kugombea nafasi yoyote nyingine ya uongozi katika chama cha siasa, alazimike kuacha kazi na kulipwa mafao yake.”

Haijaweza kufahamika pia, ikiwa Dk. Bashiru aliacha kazi kwenye chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakati anateuliwa na kupitishwa kuwa katibu mkuu wa CCM, kuchukua nafasi ya kada mashuhuri wa chama hicho, Kanal Abdulrahaman Kinana, aliyekuwa ameomba kupumzika.

Ibara ya 115 (1) ya Katiba ya CCM, katibu mkuu hupatikana kwa kuchaguliwa na Halmashauri Kuu ya taifa (NEC), baada ya kupendekezwa na mwenyekiti.

Wanazuoni kadhaa wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, waliojiunga na vyama vya upinzani, walijikuta “wakisulubiwa” kutokana na uamuzi wao wa kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa, wakati wakiwa bado watumishi wa chuo hicho cha umma.

Baadhi ya wanaotajwa kuwekwa kiti moto, ni pamoja na Profesa Kitila Mkumbo, ambaye alishitakiwa kwenye kamati ya maadili na kutaka kumfukuza kazi. Kwa sasa, Profesa Kitila, ni mbunge wa Ubungo (CCM) na waziri wa uwekezaji.

Profesa Kitila alikuwa ametuhumiwa kushiriki kwenye uongozi wa kisiasa kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

1 Comment

  • Mwengine ni Prof Mwesiga Beregu

    Pia katiba ya nchi inasema katibu mkuu kiongozi anatakiwa atokane na utumishi wa umma (civil service), siyo mwanasiasa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!