January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uteuzi CCM, ni rushwa, uhasama

Viongozi wa juu wa CCM wakifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho

Spread the love

UHASAMA wa kuwania madaraka kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeanza kujionyesha wazi katika maandalizi ya chama hicho kupata wawakilishi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika 14 Desemba mwaka huu.

Wakati chama hicho kikiendesha kura za maoni ili kutafuta wawakilishi wake watakaoshindana na wagombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), sura halisi ya kuwania madaraka imejionesha.

Maeneo ya Soko Kuu; Uhindini; Azimio na Sisimba kumedhihirika wizi na udanganyifu mtupu. Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa Mtaa wa Soko Kuu, Anna Mwakabonga amepigwa na butwaa kuona utaratibu umekiukwa ili kulindana.

“Sisi wajumbe tuliofika katika uchaguzi tulikuwa 59 lakini tulishangaa tulipoingia kuhesabu kura kwa sababu mimi sikuweka mtu wa kuhesabu, bali nilienda mwenyewe baada ya kuzihesabu, kura ziligongana 33 kwa 33.

Hapo nikaweka alama ya kuuliza “hizo kura nyingine nane zimetoka wapi lakini kabla sijapata majibu yakatolewa matokeo kuwa mwenzangu ameshinda kwa kura 34 na mimi nikapata kura 33, kura tisa ziliongezwa,” alisema Anna.

Ametaja madai yake mengine ni kutokuwepo daftari la mahudhurio ya wanachama walioshiriki kupiga kura pamoja na  baadhi ya wanachama wa mtaa wa Azimio kufanya uchaguzi wa viongozi wao bila ya kushirikisha wanachama wa mtaa wa Soko Kuu lakini wameshangazwa kuona wanachama wa mtaa wa Azimio kushiriki kupiga kura ya viongozi wa mtaa wa Soko Kuu.

Filbert Sanga, mgombea aliyeshinda kura za maoni baada ya kuibuka kidedea kwa kura 34 na hivyo kumzidi mgombea mshindani wake kwa kura moja, amezungumzia uchaguzi huo kuwa ulikuwa wa haki huku mwanachama mkongwe ndani ya CCM, Marry Mkandawile kutoka Mtaa wa Azimio akisema kura za maoni zilikuwa za haki na kwamba asiyeridhika anayo haki ya kukata rufani kwenda ngazi za juu.

Viongozi wa Tawi na Kata akiwemo Katibu wa Tawi la CCM Sisimba Lazaro Mgonera, Katibu Kata wa Sisimba, Emily Mwaituka na Warden Mwakang’ata ambaye ni Mwenyekiti wa Kata hiyo nao kwa nyakati tofauti wamesema uchaguzi huo ulikwenda vizuri huku kukiwa na wajumbe 70 lakini hawakuwa tayari kuzungumzia sababu ya kutokuwepo kwa daftari la mahudhurio na kuwashirikisha wajumbe wa mtaa mwingine ambao hawakushiriki kwa pamoja kuchagua viongozi wao.

Wakati tukisubiri kujuwa nini kitaendelea ndani ya Chama hicho ambacho wanachama wake wamekipa majina mengi ikiwemo Chama dume, Ofisi ya CCM Wilaya ya Mbeya mjini iliagiza uchaguzi urudiwe kwa nafasi ya Mwenyekiti.

Agizo hilo linatokana na uchaguzi uliofanywa Novemba 3 wanachama wakimchagua Filbert Sanga kwa kujizolea kura 55 dhidi ya 35 za mshindani wake Anna Mwakabonga.

Baadhi ya wanachama wa Tawi la Sisimba wakiwemo Anastazia Lukamba, Rebeka Gibson na Isaya Konso walisema katika nyakati tofauti kuwa baada ya uchaguzi huo kinachotakiwa ni kuvunja makundi na kuunganisha nguvu moja ya kumfanyia kampeni mgombea aliyeshinda ili aweze kushinda tena katika chaguzi za serikali za mitaa.

Licha ya kauli hiyo, baadhi ya wanachama wamesema wanapenda asimamishwe mgombea atakayeuzika kwa wananchi wa itikadi zote na kwamba suala la rafu ndani ya uchaguzi linapaswa kukemewa, vinginevyo watakuwa hatarini kupoteza mtaa kwa wapinzani.

Mwakabonga alisema licha ya kutia saini kukubali kushindwa, ameshangazwa na baadhi ya wanachama waliokata kadi siku ya uchaguzi wakiwa na stakabadhi rangi ya njano ilhali “stakabadhi ya sasa ni ya rangi nyeupe, hayo yote tunawaachia viongozi wa ngazi za juu waamue.”

Ninachotaka kusema uchaguzi wa serikali za mitaa na kura za maoni ndani ya vyama vya siasa zizalishe na kuibua viongozi bora na siyo bora viongozi kwani huo ndio msingi wa kusimamisha viongozi kuanzia ngazi za vijiji, Kata na hatimaye wabunge na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Viongozi watakaowapigia kura waheshimiwa watakuwa wananuka rushwa basi hadi ngazi ya juu “itakuwa ni viongozi wanaonuka rushwa, mafisadi, waroho na wenye uchu wa kujilimbikizia mali badala ya kuwatumikia Watanzania walala hoi.”

Viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kuwa macho na kukemea mbinu chafu katika kupata mgombea.

Makala hii imeandikwa na Thompson Mpanji

error: Content is protected !!