May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Utembo’ wa rais umekuzwa na CCM

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku

Spread the love

NIMEGUSWA na kauli za wazee watatu, wanasiasa wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Joseph Butiku, Phillip Mangula, na Wilson Mukama – walipotoa mada mbalimbali kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Ijumaa iliyopita, anaandika Ansbert Ngurumo.

Akisisitiza miiko ya uongozi, Butiku, Mwenyekiti wa Mwalimu Nyerere Foundation, alisema:

“Miiko ilikuwa inasema ukitaka kuwa rais utambue na uwe na imani kuwa watu wote ni sawa usiwe wewe ni tembo. Lazima utambue kuwa unatokana nao na lazima kiongozi huyo atambue kuwa anaongoza watu, hivyo anapaswa kuwaongoza kwa heshima.”

Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM, naye alizungumzia miiko, lakini akasisitiza zaidi kwenye dhana ya uongozi bila rushwa.

Alisema: “Katika mkutano Mkuu wa CCM mwaka 2012 ambao ndio ulinichagua kuwa makamu mwenyekiti na nikapata uenyekiti wa kamati ya maadili, tuliazimia kuchukua hatua haraka kwa viongozi wala rushwa na ndiyo kazi anayofanya Rais Magufuli.”

Mukama, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, alisisitiza juu ya umuhimu wa kupata viongozi kwa haki na uwazi, na kwamba ni hatari kupata  viongozi kwa vitisho, ujanja, ulaghai, na rushwa.

“Asili ya uongozi ni watu, na viongozi lazima wapatikane kwa haki na uwaz,i na si kwa njia za ujanja ujanja, vitisho, ulaghai na rushwa na inapokuwa hivyo tunapoteza sifa ya uongozi.”

Wakati Butiku anazungumzia ubaya wa kuwa na rais mwenye tabia za tembo, anasahau kwamba tayari tunaye!

Bahati mbaya, naye ameshiriki kumpigania. Mzee Butiku, muumini wa katiba mpya itokanayo na maoni ya wananchi, alilazimika kupigania CCM isiyotaka katiba mpya.

Maana kama katiba mpya ingepatikana, leo tusingekuwa tunazungumzia “utembo wa rais.”  Katika katiba mpya, kwa mujibu wa rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba (rasimu ya Warioba), miiko ni sehemu ya katiba. Tusingehitaji makongamano kusisitiza umuhimu wa maadili ya uongozi.

CCM walipoungana kama chama kuikataa, walikuwa wanakwepa kuwajibishwa. Walikuwa wanakwepa uadilifu. Walikuwa wanatafuta rais tembo.

Ni kweli, wapo wana CCM walipinga rasimu ya Warioba kwa shingo upande, kwa ajili ya kulinda msimamo wa pamoja wa chama; lakini baada ya kuundwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), tulitarajia wasikilize dhamiri zao, wawe sehemu ya Ukawa.

Kwa hiyo, Butiku na wenzake wameshiriki kutuwekea rais mwenye “utembo,” ambaye anatumia utembo huo kuziba njia za wengine, ili yeye pekee ndiye aonekane, asikike, na asikilizwe.

Mwalimu Nyerere alipolazimisha CCM kukubali mfumo wa vyama vingi mwaka 1991, alilenga kudhibiti “utembo” huu. Alijua zama zilishabadilika, na kwamba chama kimoja kikipewa fursa peke yake bila kukosolewa na wengine, kinalewa madaraka, na kinatumbukia katika uharibifu.

Mwaka jana tulikuwa na fursa ya kudhibiti “utembo” huu, lakini wazee wakashindwa kushauri watawala wasichezee maoni ya wananchi mara mbili – katika Bunge Maalumu la Katiba, na katika uchaguzi mkuu.

Najua kwamba kuna watu wema ndani ya CCM – na akina Butiku, kwa mtazamo wangu, ni miongoni mwao – lakini wema wao unamezwa na mfumo wa chama chao. Mbali na mfumo, wema wao unamezwa pia na mapenzi yao kwa CCM.

Hilo linajitokeza pia hata wanapomjadili Mwalimu Nyerere, ambaye waliishi na kufanya kazi naye kwa karibu sana. Bado wanamtazama Mwalimu Nyerere kwa jicho la CCM tu. Wanasahau kwamba ni Mwalimu Nyerere alikuwa Mtanzania zaidi kuliko mwanaCCM. Ni Mwalimu Nyerere huyo huyo aliyetamka hadharani kwamba “CCM si mama yangu…”

Yawezekana, kama Mwalimu Nyerere angekuwa hai leo, asingekuwa mwana CCM. Au kama angekuwa mwana CCM, angewataka wazingatie rasimu ya Warioba, kama “alivyowalazimisha” kukubali mfumo wa vyama vingi. Na kama wangemkatalia, angeungana na wana Ukawa ili kuangusha CCM.

Bila Mwalimu Nyerere, Mzee Butiku na wenzake hawaoni umuhimu wa Tanzania bila ya CCM. Na kwa sababu hiyo, nao ni sehemu ya wazee wanaotuchelewesha. Lakini watu wa aina ya Mzee Butiku ni muhimu sana katika zama hizi. Walau wametukumbusha kile ambacho wengine wanaogopa kusema.

Vile vile kwa Mzee Mangula. Anapaswa kujua kuwa kama CCM ingekuwa binadamu, rushwa ingekuwa ndiyo mishipa ya damu. CCM haiwezi kuishi bila rushwa. Kwa miongo miwili sasa, CCM inapata viongozi kwa rushwa.

Hata wale wasiotoa rushwa wenyewe moja kwa moja, wanatumia wengine kusaka fedha za kampeni, na kuhonga ili wao wapite.

CCM inaweza kupiga vita rushwa majukwaani tu. Viongozi hawa wanaojitapa kupiga vita rushwa wamepatikana kwa rushwa. Mwalimu Nyerere alianzisha vita hii, lakini hakufaulu. Madwani hadi rais, ni mazao ya rushwa!

Kama Mangula anasema mkutano mkuu ulioazimia kushughulikia rushwa ulifanyika mwaka 2012, na kwamba uliazimia wahusika washughulikiwe haraka, alikuwa wapi katika uchaguzi mkuu wa 2015 uliosheheni rushwa nje nje?

Anachosema Mzee Mangula ni cha msingi, lakini katika siasa za CCM, hakiwezekani, hakitekelezeki. Rais Mstaafu Jakaya Kikwete mwenyewe alikemea rushwa ndani na nje ya serikali, lakini zilikuwa kauli za vikaoni na majukwaani tu.

Hata kama aliwatoa kafara mawaziri, akina Basil Mramba na Daniel Yona, ufisadi mkubwa wa kutisha uliendelea kutafuta taifa, tena mwingine ukitokea Ikulu na kwa watu wake wa karibu.

Rais Magufuli naye vivyo hivyo. Anakemea rushwa majukwaani, na anachukua hatua dhidi ya baadhi ya watendaji. Lakini kuna mazingira ambayo yamefanya wananchi waone kuwa naye atakuwa kama watangulizi wake.

Majuzi tu, ameshindwa kushughulikia sakata la Mkataba wa Lugumi an Jeshi la Polisi. Ameshindwa kutia hatiani walionunua kivuko kibovu cha Mv Dar es Salaam. Ameshindwa kutumbua waliosimamia ujenzi wa barabara zetu chini ya kiwango nchi nzima.

Ameshindwa kutumbua waliouza na kugawa nyumba za serikali zadi ya 9000. Hiki ni kielelezo dhahiri kwamba, akitaka, atachagua maofisa wa kufikisha mahakamani kisiasa, ili kujipiga kifua. Lakini rushwa kubwa kubwa zitaendelea kushamiri.

Nakubaliana na Mzee Mukama, lakini natambua kuwa bila vitisho, ujanja, ulaghai, na rushwa, viongozi hawa tulionao wasingepatikana. Na ndio hawa wanaotoa ahadi za kutokomeza rushwa. Wataaminika?

error: Content is protected !!