Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Utata watawala wagombea Chadema kunyimwa fomu
Habari za Siasa

Utata watawala wagombea Chadema kunyimwa fomu

Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara
Spread the love

UTATA umeibuka katika majimbo manne ya uchaguzi baada ya Wakurugenzi wa Uchaguzi, kuwanyima fomu wagombea wateule wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa zaidi zinaeleza, wateule wa Chadema wamenyimwa fomu baada ya watu ambao hawakupitishwa na chama hicho kugombea, kuchukua fomu wakiwa na barua za utambulisho kutoka kwa makatibu wa Chadema wilaya.

Majimbo kulikoibuka utata huo ni Kigamboni, Mbagala, Kibamba yaliopo jijini Dar es Salaam na Kilombero mkoani Morogoro.

Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Bara ameitaka Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), kuhakikisha wateule wake waliopitishwa na vikao halali vya chama hicho wanapewa fomu za kugombea kwa mujibu wa utaratibu unavyoelekeza.

Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu kuhusu utata huo leo Jumatano tarehe 19 Agosti 2020 amesema, chama ndio kilicho na wajibu wa kutaja jina la mgombea wake.

John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema

“Tunaitaka Tume itupatie fomu kwa sababu chama ndicho chenye wajibu wa kutafuta wagombea, na mgombea yeyote wa uchaguzi anatakiwa adhaminiwe na chama.

“Hii maana yake kinaweza kusema huyu ni mgomeba wetu na sio tume wala sio mtu yoyote anaweza kusema huyu ni mgombea wa Chadema,” amesema Kigaila.

Amesema, sababu za wagombea hao kupewa fomu kwa maelezo barua za utambulisho kutoka kwa makatibu wa Chadema wa wilaya hazina mashiko, kwa kuwa mwenye mamlaka ya kutambulisha wagombea ni Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

“Inatakiwa chama kiseme huyu ndio mgombea wetu na kama akijitokeza mtu akasema huyu ndio mgombea wa Chadema na chama kikasema sisi mgombea wetu huyu hapa, inabidi Tume ikubaliane na chama, haiwezi kukubali mgombea anayesingizia mimi mgombea wa Chadema,” amesema Kigaila.

Lakini pia, barua hizo zilizowatambulisha wagombea hao katika majimbo ya Kilombero, Kibamba, Kigamboni na Mbagala zilikuwa za kughushi na wala hazikutoka kwa makatibu wa wilaya husika.

“Nchi hii mihuri haichongwi?  Inatoka kwa Mungu?  Huyo anasema amejitambulishwa na katibu wa Chadema, Chadema ina katibu mkuu mmoja anayesema mgombea wetu ni huyu, wao huyo mgombea wanamtambuaje ana chama kingine, kusema amekuja na mihuri ya Chadema sio hoja,” amesema Kigaila.

Kufuatia sintofahamu hiyo, Kigaila amesema, uongozi wa Chadema unaendelea kupambana ili kuhakikisha wagombea wake wanapewa fomu.

 

Dk. Wilson Mahera, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC

Dk. Wilson Mahera, Mkurugenzi wa NEC amesema, Tume hiyo imepokea barua ya malalamiko hayo kutoka kwa uongozi wa Chadema, na kwamba wanayafanyia kazi.

“Chadema wameiandika barua NEC, wanaomba hizo barua zibatilishwe lakini fomu inatolewa moja kwa mgombea, kwa hiyo ni changamoto sio kwamba ni mtu feki bali anatokea kwenye chama na wanakiri katibu wanamtambua, wanacholeta barua ya kufuta barua ya katibu wa jimbo,” amesema Dk. Mahera.

Dk. Mahera amesema, changamoto iliyojitokeza ni kwamba kumetokea mkanganyiko wa wagombea ndani ya chama hicho katika majimbo hayo, na kwamba haikuwa rahisi wasimamizi wa uchaguzi kufahamu dosari hizo.

“Kwa Kilombero aliyekwenda kuchukua fomu ana muhuri wa barua ya katibu wa chama, baada ya hapo kuna kutokuelewana baina ya katibu wa chama wilaya na katibu mkuu wa taifa, katibu wilaya amepeleka mgombea sio.  Sasa hapo tatizo ni la nani?” amehoji Dk. Mahera.

“Ukija Kigamboni napo nimeongea na Kigaila kwenye simu, mgombea wa Kigamboni na Mbagala waliokuja sio waliopendekezwa na walikiri kuwa ni wagombea na wanachama wa Chadema ambao walishika nafasi za pili. Hatujui nini kilitokea kwenye chama walioshika nafasi ya pili wamekuja na barua tena ya katibu,” amesema.

Zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu za kugombea ubunge, na udiwani katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020 limeanza kuanzia tarehe 12 hadi 25 Agosti 2020.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!