October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Utata waibuka Mwambe kuendelea kuwa ‘mbunge’

Cecil Mwambe, aliyekuwa Mbunge wa Ndanda kwa tiketi ya Chadema

Spread the love

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, ameibua hoja iliyoibua utata kuhusu Cecil Mwambe, aliyekuwa mbunge wa Ndanda, mkoani Mtwara, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Akizungumza bungeni juzi Jumatano, tarehe 6 Mei 2020, Spika Ndugai alisema, hafahamu kama Mwambe alijiuzulu ubunge.

Alitoa kauli hiyo baada ya kutumiwa barua na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, inayoelezea kuwa Mwambe siyo mbunge wa Chadema, kufuatia hatua yake ya kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Spika Ndugai amepinga barua hiyo na kusema, kwa kuwa imeandikwa “hovyo;” haionyeshi kikao gani kilimfukuza Mwambe, kilikaa lini na wapi.

Akaongeza, “mimi bado namtambua Mwambe kama mbunge halali wa Ndanda na namkaribisha bungeni wakati wowote anapotaka.”

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 71 (1) (f) ya Katiba ya 1977 inataja sababu mbalimbali za mtu kukoma kuwa mbunge ikiwamo mbunge huyo ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwemo wakati alipochaguliwa kuwa mbunge.

Ibara hiyo inapewa nguvu na maneno ya Mwambe mwenyewe ambaye tarehe 15 Februari 2020, aliutangazia umma kuwa amejiunga na CCM.

Mwambe alitangaza kuondoka Chadema katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam.

Alipopokelewa na Humphrey Polepole, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi wa chama hicho.

Cecil Mwambe (kulia) akipokea kadi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) alipokabidhiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally

Alisema, “katika kipindi chote nikiwa mwanachama wa CHADEMA, nimekuwa mbunge, mjumbe wa Kamati Kuu na mwenyekiti wa Chama Kanda ya Kusini. Kwa nyakati tofauti, nikiwa ndani ya chama hiki nimepambana kuhakikisha tunakijenga nikiwa na matarajio kwamba malengo yake ya kuwakomboa Watanzania yatafikiwa lakini kila kukicha ninaona giza mbele.”

“Leo hii, tarrehe 15 Februari 2020, kwa hiaria yangu, kwa kutumia haki yangu ya kikatiba, nimeamua mwenyewe kujiunga na Chama Cha Mapinduzi na nitagombea tena ubunge katika uchaguzi ujao, kupitia chama bora ambacho kinaheshimu demokrasia ya ndani, kina misingi imara ya uongozi, kinaheshimu wanachama na viongozi wake na kinajali maadili ya wanachama na viongozi wake na nitawaomba wananchi wangu wawe na subira na wanipokee endapo nitapewa ridhaa ya kufanya ivyo.”

Katika mkutano huo, Mwambe alisema, nataka tu niwakumbushe kwamba, ushindi wangu wa ubunge mwaka 2015 ulitokana na wakazi wa jimbo la Ndanda, ambao waliniamini, na bado ninaamini bado wapo na wako tayari kuhakikisha CCM kinashinda.

“Ninachoweza kusema, nawapenda sana na bado ninawapenda na ninawahakikishia tutaendelea kushirikiana kwa hali na mali kuendeleza yale tuliyoyaanza mwaka 2015 kuhakikisha wananchi wa Jimbo letu na mkoa kwa ujumla tunapata maendeleo tuliyoyatarajia,” alieleza Mwambe.

Mwambe alipokelewa na katibu mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally, 22 Februari 2020, akiwa ziarani mkoani Mtwara.

Mkutano wa kumpokea Mwambe ulifanyika katika jimbo la Ndanda, ambapo alitumia fursa hiyo kumkabidhi mwanachama wake huyo mpya kadi ya uanachama wa CCM.

Mwambe alichukua uamuzi huo, siku chache kupita baada ya kuwa amejitokeza kuwania uenyekiti wa Chadema kumrithi Freeman Mbowe.

Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania

Hata hivyo, Mwambe hakufanikiwa kushinda akidai kuchezewa figisufigisu za hapa na pale.

John Msafiri, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam anazungumzia suala hilo alisema, “kwa kweli, mimi hili linanichanganya. Sasa  inawezekana vipi Spika Ndugai aseme, huyu ni mbunge, wakati yeye mwenyewe alijiuzulu na tena akapewa na kadi ya uanachama hadharani?”

Alisema, “…nafikiri kuna kitu hapo. Mimi naona kama huyo Mwambe atakwenda bungeni kutakuwa na shida lakini sidhani kama atakwenda kwani atakuwa anawaona Watanzania wajinga.”

Naye Mwambe akizungumzia suala hilo, alisema kuwa amepokea kwa mikono miwili maelekezo ya Spika Ndugai, lakini bado anatafakari kurejea kwake bungeni.

error: Content is protected !!