Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Utata mtupu Nassari kuvuliwa ubunge
Habari za SiasaTangulizi

Utata mtupu Nassari kuvuliwa ubunge

Spread the love

HATUA ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutangaza kumvua ubunge mbubge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Samwel Nassari, limesheheni utata. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Ndugai alitangaza kumvua Nassari ubunge wake, kufuatia madai kuwa mbunge huyo ameshindwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo, jambo ambalo linadaiwa kuwa siyo kweli.

Akizungumza na MwanaHALIIS ONLINE kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi, Nassari anasea, “siyo kweli kwamba sijahudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge. Nimehudhuria. Hata Bunge la Septemba na Januari mwaka huu, nilikuwapo.”

Aidha, Nassari anasema, “siyo kweli pia kwamba Spika wa Bunge; na au ofisi ya Bunge, haina taarifa ya kutokuwapo kwangu bungeni.”

Ndugai aliutanganzia umma leo Alhamisi, tarehe 14 Machi 2019, kuwa ameamua kumvua ubunge Nassari kwa kuwa amekwenda kinyume na masharti ya Ibara ya 71 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri.

Amesema, tayari amemtaarifu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, juu ya hatua hiyo.

Nassari aliingia bungeni kwa mara ya kwanza, Aprili 2012, kufuatia kufariki dunia kwa aliyekuwa mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM), Jeremiah Sumari.Amekuwa mbunge wa kwanza kuondolewa na Spika kutokana na madai ya utoro.

Anasema, “napenda kukufahamisha kuwa Mheshimiwa Joshua Nassari, amepoteza sifa ya kuwa mbunge kutokana na kushindwa kukidhi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano yam waka 1977.

Kwa mujibu wa Spika Ndugai, Nassari amepoteza sifa za kuwa mbunge, kutokana na kitendo chake cha kutohudhuria Mikutano ya Bunge mitatu mfululizo.

Mikutano ambayo Nassari anadaiwa kutohudhuria, ni Mkutano wa Kumi na Mbili ulioanza vikao vyake tarehe 4 hadi 14 Septemba 2018; Mkutano wa Kumi na Tatu wa tarehe 6 mpaka 16 Novemba 2018 na Mkutano wa Kumi na Nne wa tarehe 29 Januari hadi tarehe 9 Februari 2019.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi wa Spika Ndugai, umezingatia mashati hayo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayoeleza kuwa “Mbunge atakuwa amekoma Mbunge na ataacha kiti cha chake katika Bunge, ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya Mikutano ya Bunge Mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.”

Taarifa hiyo inaeleza pia kuwa Ibara hiyo imefafanuliwa kwenye Kanuni ya 146 (1) na 2 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2016 kuwa kuhudhuria vikao vya Bunge na Kamati zake, ni wajibu wa kwanza wa mbunge.

Kanuni inasema, “Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria Mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyoletwa kwa maandishi, atapoteza Ubunge wake na Spika ataiarifu Tume ya taifa ya uchaguzi.”

Kwa mujibu wa Nassari, amehudhuria vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge katika Mkutano wa Bunge la Septemba na Bunge lililopita la Januari, na kwamba hata leo alikkuwa jijini Moshi kwenye kazi za Kamati.

“Labda kama Kamati za Bunge, siyo sehemu ya Bunge. Lakini Katiba ya Jamhuri, inaeleza vikao vya Mikutano ya Bunge. Kama vikao vya mikutano ya Bunge, maana yake, ni kwamba hata Kamati za Bunge, ni Mkutano wa Bunge,” ameeleza mbunge mmoja ambaye ni mwanasheria na mtaalamu wa mambo ya Katiba.

Mbunge huyo ambaye hakupenda kutajwa jina amesema, “…kifungu ambacho Spika Ndugai amekinakili, kinaeleza kuwa Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake akishindwa kuhudhuria vikao vya Mikutano ya Bunge. Vikao vya mikutano ya Bunge, vinaanzia kwenye Kamati.”

Alipoulizwa kutokana na mkanganyiko huo, anashauri nini kifanyike, mbunge huyo amesema, “ni mheshimiwa Nassari, kukimbilia haraka mahakamani kupinga maamuzi ya Spika na kuomba zuio la Mahakama dhidi ya Tume ya Taifa ya uchaguzi.”

“Hata kama hajahudhuria vikao na hata kama angekuwa hajatoa taarifa kwa Spika Ndugai, bado Spika alikuwa na nafasi ya kunyamazia kwa kumuomba kutoa taarifa. Mbona wabunge wa CCM wengi hawaji bungeni, lakini hakuna aliyefukuzwa,” amehoji.

Joshua alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Arumeru Mashariki na Trasias Kagenzi, aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo, uliokuwa na ushindani mkali kati ya mgombea huyo wa Chadema na mwenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika uchaguzi huo mdogo, Nassari aliibuka kidedea kwa kumbwaga mgombea wa CCM, Sioi Sumari. Nassari wakati huo akiwa kijana mdogo wa miaka 27 alipata kura 32,972 wakati Sioi alipata kura 26,296.

Ingawa kushindwa kwa CCM) kulionekana mapema, kufuatia rais mstaafu Benjamin Mkapa kudhalilisha familia ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa kudai Vincent Nyerere siyo mwanafamilia ya Nyerere, “lakiniumahiri wa Chadema na mgombea wake Nassari, katika kujenga hoja, kulisaidia kupatikana kwa ushindi.”

Kingine kilichosababisha CCM kushindwa, ni hatua ya baadhi ya makada wake, Stephen Wassira, Mwigullu Nchemba na Livingstone Lusinde, kuamua kuendeleza mashambulizi kwa Vincent na kudai pia kuwa watu wa Arumeru hawahitaji taarifa za Nyerere ili kuondokana na shida zao za kila siku.

Vincent ndiye aliyeongoza kampeni za Chadema katika uchaguzi huo zilizomuingiza Nassari bungeni.

Akihutubia mikutano ya kampeni katika maeneo mbalimbali, Vicenti alisema, “maneno haya yangesemwa na wanasiasa kutoka vyama vingine nisingekuwa na hoja ya kuyazungumzia; lakini kwa kuwa yamesemwa na wana-CCM, nalazimika kupaza sauti.

“Nadhani watu wa Arumeru wanahitaji fikra na taarifa za Baba wa Taifa ili angalau waone kama wanaweza kupata ufumbuzi wa matatizo yao. Hii ni kwa kuwa CCM ya Nyerere iliondoka na hamasa ya wananchi kujiletea maendeleo yao wenyewe; nafasi yake ikachukuliwa na CCM inayodai kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuuza maliasili zao.

“Wananchi wa Arumeru wamenyang’anywa ardhi yao, maji yao, na utu wao kwa kisingizio cha kuwapa wawekezaji ili wawaletee wananchi maendeleo.”

Kwa hiyo, makada wa CCM wanapodai Nyerere hawezi kuwasaidia wananchi wa Arumeru, kimsingi wako sahihi, kwani kwa CCM hii ya sasa, Nyerere ni kikwazo na adui wake mkubwa.

Jitihada nyingi zimefanyika kuhakikisha fikra za Baba wa Taifa zinazimwa na watu wote wenye fikra za namna yake wanaonekana magaidi katika taifa.

Haishangazi basi, na huenda kauli na tabia za makada hao na viongozi wao, ndizo zimezaa fikra na tuhuma, “kwamba CCM na viongozi wake ndio walimuua Baba wa Taifa ili awapishe waweze kuiuza nchi hii aliyohangaika kuijenga.”

Katika kampeni za CCM ilikuwa kana kwamba ni marufuku kutamka neno “rushwa” au “ufisadi.” Wapigadebe walionywa na kuonyeka, kuwa wasithubutu kutamka maneno hayo maana yangekirudi chama katika kampeni hizo.

Uchaguzi wa Aprili 2012 uliotimiza ndoto ya Nassari ya kuwa mbunge, ndio uliyondoa uhai wa aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, Kata ya Usa River, wilayani Arumeru, Msafiri Mbwambo (38). Mbwambo ameuawa kwa kukatwa shingoni na kitu chenye ncha kali.

Kifo hicho kinadaiwa kilitokea 27 Aprili 2012, majira ya saa mbili usiku eneo karibu na uwanja wa polisi Mji Mwema, ambapo wauaji hao walimkata shingo na kitu kama shoka; kwa kuanzia nyuma na kubakiza kidogo eneo la mbele ya shingo na kumwacha akiwa amelala chini kama aliyeanguka na pikipiki.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kasekenya aipa Tanroads wiki kukarabati barabara Morogoro

Spread the loveNaibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wiki moja...

Habari za SiasaTangulizi

‘Aliyemtonya’ Lissu kuhusu rushwa arejea madarakani

Spread the loveMwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Tutaendelea kupigania malengo ya afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya Tanzania...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NHC yadai bil. 2.1 taasisi za Serikali, Waziri atoa maagizo

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii...

error: Content is protected !!