July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Utata dhamana ya ‘wabakaji, ulawiti’ Dakawa

Spread the love

DHAMANA ya watuhumiwa wa ubakaji, ulawiti na usambazaji wa picha chafu katika eneo la Dakawa, Morogoro imeibua utata, anaandika Christina Haule.

Mvutano mkali umeibuka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro ambapo mawakili wa serikali na mawakili wa washtakiwa wakionesha kutokubaliana kuhusu washitakiwa hao kupewa dhamana. 

Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Ivan Msaki, mawakili wa serikali Gloria Rwakibalila, Edgar Bantulaki na Calistus Kapinga waliiomba mahakama kuendelea kuzuia dhamana kwa maandishi baada ya zuio hilo la dhamana kutolewa kwa mdomo na Elias Mwita, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Morogoro, dhidi ya washitakiwa hao tangu tarehe 18 Mei  kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo.

Wakili wa Serikali Gloria Rwakibalila aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Iddi Mabena (32) mkazi wa Njombe,  Zuberi Thabiti (30) mkazi wa Mbalali mkoani Mbeya, Rajabu Salehe, (30), Ramadhani Ally (26), Muhsin Ng’ahy (36), John Peter (24) wote wakiwa ni wakazi wa Wami, Dakawa wilayani Mvomero mkoani Morogoro.

Wakili huyo alidai kuwa, washtakiwa hao wote kwa pamoja walianza kusambaza picha hizo kati tarehe 28 hadi 30 Aprili mwaka huu katika maeneo yasiyojulikana wilayani Mvomero na mkoa mzima wa Morogoro kupitia mtandao wa kijamii.

Mawakili hao wa serikali wamesema kuwa, tukio hilo la ubakaji na unyanyasaji limegusa hisia za jamii na kusabisha hasira, vilio na udhalilishaji kwa wanawake jambo ambalo wakiwaachia washtakiwa hao kwa dhamana, linaweza kuhatarisha usalama wao na pengine kuharibu upelelezi wa kesi.

Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa vikali na mawakili wa washitakiwa Mohamed Mkali anaewatetea washtakiwa namba 1 na 2 na Ignas Punge  anayewatetea washitakiwa namba 3-6  ambao walidai kuwa, dhamana ni haki ya washitakiwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania ibara  ya  15.

Na kwamba kila mtu anayo haki kupewa dhamana kwani washitakiwa bado hawajathibitika kutenda kosa na kutiwa hatiani.

Aidha mawakili hao wamesema kuwa, kosa linalowakabili washitakiwa linadhamika na kwamba, washitakiwa wanalindwa kwa mujibu wa sheria  ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo kuwanyima dhamana ni sawa na kuwatia hatiani.

Hivyo wameiomba mahakama iwape dhamana washitakiwa kwa masharti yoyote ambayo mahakama itayatoa wanaweza kuyatimiza.

Hakimu Msaki ameahirisha kesi hadi tarehe 10 Juni mwaka huu kesi itakapokuja tena kwa ajili ya kutoa uamuzi wa dhamana,  washtakiwa hao walirudishwa rumande.

Katika kesi ya kwanza ya kubaka na kulawiti inayowakabili washitakiwa Idd Adam Mabela na Zuberi Thabit, nayo imeahirishwa mbele ya hakimu Marry Moyo hadi Juni 15 mwaka huu na kwamba, upelelezi wake umekamilika na itaanza kusikilizwa  kwa hatua ya awali.

Awali washtakiwa hao ilidaiwa kuwa, walimbaka na kumuingilia kinyume na maumbile msichana huyo tarehe 27 Aprili mwaka huu saa 1 usiku katika  nyumba  ya  kulala  wageni ya TITII iliyopo  katika Tarafa  ya  Dakawa, Wilaya  ya  Mvomero.

error: Content is protected !!