July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Utata ACT – Wazalendo

Spread the love

SAMSON Mwigamba, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo ameng’atuka rasmi nafasi hiyo kwa madai kuwa anaenda masomoni, anaandika Pendo Omary.

Anna Mghwira, Mwenyekiti wa chama hicho ameliambia MwanaHALISI Online kuwa, Samson Mwigamba ataanza masomo ya shahada ya Uzamili ya Biashara (MBA) katika Chuo Kikuu cha Kenyata tawi la Arusha kuanzia mwezi Mei mwaka huu.

“Kufuatia hatua hii ameomba aruhusiwe kung’atuka nafasi yake ya Katibu Mkuu wa chama. Katika kikao chake cha dharura kilichofanyika jana katika Hotel ya Kebby’s Jijini Dar es Salaam, Kamati ya Uongozi Taifa imeridhia ombi la Katibu Mkuu,” amesema Mghwira.

Mghwira amesema kufuatia hatua ya kung’atuka kwa Mwigamba, Kamati ya Uongozi ya chama hicho imeiagiza kamati ya Mafunzo na Uchaguzi ianze mchakato wa kumpata katibu mkuu mpya kwa kuzingatia katiba na kanuni za uchaguzi wa chama.

Aidha, Mwigamba amesema hatua hiyo haimzuii kushiriki katika shughuli zingine za chama atakapohitajika na akawa na muda wa kutosha.

“Mimi ni mwanachama mwanzilishi wa ACT- Wazalendo. Nikipata nafasi nitaendelea kukitumikia chama. Japo nimekuwa kiongozi wa chama katika mazingira magumu. Kuanzisha chama bila mapato inakulazimu kuchangisha watu na wakati mwingine vyama kuwekwa mifukoni mwa watu,” amesema Mwigamba.

Haya yanajiri ikiwa ni miezi takribani mitano tangu gazeti la Mawio lililofutwa na serikali kuandika juu ya uwezekano wa Mwigamba kuondolewa katika cheo hicho ili Zitto Kabwe aweze kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu kumwezesha kufanya kazi za utendaji za siku kwa siku ndani ya chama.

Iliandikwa kuwa Mkuu huyo wa chama ameandaa na kuratibu mkakati wa kumg’oa kwenye uongozi Katibu Mkuu, Mwigamba.

Taarifa zilisema kuwa Zitto anampindua Mwigamba ili achukue wadhifa huo, baada ya kubaini cheo cha kiongozi mkuu wa chama, hakina nguvu kiutendaji.

Vyanzo vyetu ndani ya ACT Wazalendo viliarifu kuwa kama mkakati huo ungefanikiwa Zitto angekuwa katibu mkuu, nafasi yake ya “ukuu wa chama” atapewa Mghwira.

Taarifa zilizoandikwa na Mawio zilidai kuwa kuwa mkakati huo ulianza katikati ya Septemba 2015 na ulipaswa kukamilika ndani ya miezi minne.

Waliopewa jukumu la kusimamia mradi huo wametakiwa kuukamilisha “mapema,” ikiwezekana na uwe tayari ifikapo Januari 2016.

Zitto alitajwa kuandaa na kuratibu mkakati huo, baada ya kubaini nafasi yake ndani ya chama (kiongozi mkuu) ambayo kazi yake ni kueneza sera na kutoa ushauri ndani ya chama, haina nguvu kama nafasi aliyonayo Mwigamba ya ukatibu mkuu.

Katibu Mkuu ndiye msimamizi mkuu wa utendaji siku katika chama.

Licha ya kutowekwa wazi, vyanzo vya taarifa viliarifu kuwa zitto akiwa Katibu Mkuu ataweza kuhusika moja kwa moja na fedha za ruzuku ambazo chama kingepata kama kingekuwa na sifa ya kupewa fedha hizo kutoka serikalini kulingana na matokeo ya uchaguzi mkuu.

error: Content is protected !!