October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Utaratibu mpya wakwamisha kesi ya Mbowe, Lissu atoa ujumbe

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na wenzake wakiwa mahakamani

Spread the love

 

TUNDU Lissu, Makamu mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania amepinga uamuzi wa kesi ya kiongozi wa chama hicho, Freeman Mbowe na wenzake kuendeshwa ‘gizani.’ Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Lissu ametoa kauli hiyo ikiwa mvutano unaendelea Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo Alhamisi, tarehe 16 Septemba 2021, baina ya upande wa Chadema na Mahakama.

Ni baada ya utaratibu mpya kutangazwa tofauti na ule wa jana Jumatano katoka kesi hiyo namba 16/2021 ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake watatu.

Utaratibu huo ni kupunguza idadi ya watu wanaoingia huku kukuwekwa zuio la wote wanaoingia ndani kutoingia na simu. Jana waliingia na simu.

Walioruhusiwa kuingia ni viongozi wa Chadema watano, mawakili pande zote 20, wageni maalum watatu, wanahabari 10.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mustapha Siyani, ilikuwa ianze saa 4:00 asubuhi kwa kuendelea na ushaidi kutolewa na Kamanda wa Polisi Kinondoni (RPC), Ramadhan Kingai, lakini hadi saa 5:35 asubuhi ilikuwa haijaanza.

Tayari RPC Kingai amekwisha kuingia pamoja na washtakiwa huku Jaji akiwa bado hajaingia na hakuna taarifa zozote.

Hii inatokana na mawakili wa upande wa utetezi ukiongozwa na Peter Kibatala kupinga utaratibu huo na kutoingia ndani ya mahakama hadi utaratibu wa kuendesha kesi ‘gizani’ ubadilishwe.

Lissu kupitia ukurasa wake wa Twiiter ameandika “Nimetaarifiwa kwamba Polisi na/au Mahakama wanazuia watu kuingia na simu mahakamani ili kudhibiti utoaji wa taarifa za yanayoendelea kwenye kesi ya uongo dhidi ya Mwenyekiti Mbowe. Haki lazima ifanyike na ionekane imefanyika. Haki haiwezi kufanyika gizani na ikaonekana imefanyika.”

Pia ameongeza “Mahakama inayoendesha kesi gizani sio mahakama huru. Mahakama inayoingiliwa na mapolisi kuhusu nani aingie na nani asiingie mahakamani kusikiliza kesi ni mahakama mateka.Tutakutana shortly na kutoa msimamo wa Chama chetu kuhusu hili. Hatutakubali kesi hii kuendeshwa mafichoni!.”

Katika viunga hivyo vya Mahakama iliyopo Mawasiliano jijini Dar es Salaam, ulinzi umeimalishwa na mvutano wa kupinga na kutetea utaratibu huo unaendelea.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali.

error: Content is protected !!