May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Utaratibu kumuaga Dk. Magufuli wabadilishwa

Spread the love

 

UMATI mkubwa wa waombolezaji wanaofika kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, umeifanya Serikali kutangaza utaratibu mpya wa kumuaga. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea)

Utaratibu huu umetangazwa leo asubuhi Jumatatu tarehe 22 Machi 2021, na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk. Hassan Abbas, alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari, katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Ni baada ya kile kilichotokea juzi na jana Jumapili kwa umati mkubwa sana uliojitokeza Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuuaga mwili wa Dk. Magufuli.

Kutokana na umati mkubwa huo, utaratibu ulibadilishwa na jeneza lenye mwili wa Dk. Magufuli, ukizungushwa mara tano uwanjani hapo, ili kutoa fursa kwa wananchi kumuaga na wengine walijipanga barabarani kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Tayari Uwanja wa Jamhuri, Dodoma umefungwa kuanzia saa 2 asubuhi kutokana na kujaa waombolezaji huku nje nako kukiwa na watu wengi.

Akitangaza mabadiliko yatakayoanza Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Chato mkoani Geita, Dk. Abbas amesema, “wananchi ni wengi sana wanaojitokeza kuaga mwili wa Dk. Magufuli.”

“Wananchi waliopata nafasi ya kuingia uwanjani ni wengi, kwa maana hiyo, tunatangaza utaratibu mpya ambapo jeneza lenye mwili wa Dk. Magufuli litapita karibu na maeneo waliyokaa ili wamwombee dua na kumuenzi,” amesema Dk. Abbas

“Utaratibu huu utaanza kuanzia leo na maeneo mengine. Lakini kutokana na hili, tumeongeza maeneo ambayo mwili wa mpendwa wetu, utakuwa ukipita maeneo mbalimbali ili kutoa fursa kwa wananchi kutoa heshima zao za mwisho,” amesema Dk. Magufuli

Amesema, tayari viongozi mbalimbali wameanza kuwasili nchini ambapo leo Jumatatu ni siku ya mapumziko ambapo kunafanyika shughuli ya kuuaga mwili wa Dk, Magufuli kitaifa.

Dk. Hassan Abbas, Msemaji wa Serikali

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ndiye ataongoza maelfu ya waombolezaji katika shughuli hiyo.

Dk. Abbas amesema, Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, nayo itakuwa siku ya mapumziko ambayo ndiyo hasa mwili wa Dk. Magufuli utazikwa nyumbani kwao, Chato mkoani Geita.

Dk. Magufuli alifikwa na mauti tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.

Marais waliothibitisha kushiriki ni; Uhuru Kenyatta (Kenya), Lazarus Chakwera (Malawi), Azali Assoumani (Comoro), Filipe Nyusi (Msumbiji) na Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe.

Wengine ni; Edgar Lungu (Zambia), Hage Geingob (Namibia), Mokgweetsi Masisi (Botswana), Felix Tshisekedi (Congo) na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.

Mbali na marais hao, Dk. Abbas alisema Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais wa Angola, Joao Lourenco na Rais wa Burundi, Everist Ndiyashimiye, watawakilishwa katika shughuli hiyo.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!